Sunday, October 25, 2015

Vyama vitatu vyakosa mawakala Mtwara..Chadema 'wachakachuliwa' mawakala.


Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani wakiwa katika foleni ya kusubiri kupiga kura kuwachagua wagombea wa Ubunge, Udiwani na Rais katika kituo cha Ligula C-2



Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani wakiwa katika foleni ya kusubiri kupiga kura kuwachagua wagombea wa Ubunge, Udiwani na Rais katika kituo cha Shule ya Msingi Kambarage, ambako amepigia kura mgombea Ubunge wa chama cha ACT-Wazalendo, BakariMchira



Na Juma Mohamed.

WAKATI zoezi la upigaji kura likiwa linaendelea katika vituo mbalimbali hapa manispaa ya Mtwara Mikindani, baadhi ya vyama vimekumbwa na changamoto ya kukosa mawakala katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Wkizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wagombea Ubunge wa vyama vitatu ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi wamekiri kukumbwa na changamoto hiyo kwa sababu zinazotofautiana.
Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha shule ya msingi Kambarage, mgombea Ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Bakari Mchira, alisema vipo baadhi ya vituo ambavyo wamekosa kuwa na mawakala ikiwa ni pamoja na kituo ambacho amepigia kura.

S/M Kambarage


Alisema, hali hiyo imesababishwa na kukosa kuapishwa kwa mawakala wao kutokana na wahusika wa suala hilo kuwa kwenye semina ya siku mbili juu ya uchaguzi, jambo ambalo liliwafanya wakose barua za kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi za kuwatambua kama mawakala.
“Havizidi vituo vitano ambavyo mawakala hawajaapishwa, tatizo limekuwa ni kuapishwa..na sio uzembe kwasababu walikwenda ila watendaji walikosekana, unajua wakati wa kuapa watendaji wa kata ndio wanahusika, sasa siku za mwanzo kulikuwa na watu wengi maana ni kama inavyokuwa siku za kupiga kura, mtu anakuja anaona kuna watu wengi anaamua kurudi kwa kujua atakuja siku inayofuata..” alisema
Alisema ili kutatua changamoto hiyo, wanashirikiana na vyama vingine vya upinzani ambavyo pia vimekosa mawakala ili kusaidiana majukumu ya kulinda kura.
Naye, mgombea Ubunge wa chama cha NCCR-Mageuzi, Uledi Hassan Abdallah, alisema, wanashirikia kwa karibu na Chadema katika kusaidia kuweka mawakala, kwahiyo pale ambapo hakuna wakala wa NCCR, wakala wa Chadema anahusika kulinda kura zao na hivyo hivyo kwa Chadema.
Kwa upande wao, Chadema, kupitia mgombea wao wa Ubunge, Joel Nanauka, alikanusha kuwa na ushirikiano wa vyama vingine katika kuweka mawakala na kusema kuwa mawakala wao wanatekeleza majukumu kwa upande wa Chadema pekee.

Ligula C-2


Aidha, walilalamikia kitendo kilichojitokeza katika baadhi ya vituo kuwa na mawakala wa Chadema ambao hawatambuliki na mgombea huyo ambao walipewa barua na uongozi wa chama wilaya.
“Kuna mawakala ambao wanaonekana kuwa na barua za Chadema, lakini mimi kama mgombea na hata msimamizi mkuu wa mawakala hatuwafahamu, lakini wamejitambulisha na wameruhusiwa kuingia kwenye vituo lakini nafikiri ni jambo la kisheria zaidi, na najaribu kulitatua..” alisema Joeli.
Alikiri kuwa na mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama lakini hakutaka kuuzungumzia kiundani kwasababu ni swala la kiuongozi, huku akidai kuwa na watu ambao waliwapeleka mawakala kinyume na taratibu na kuwapatia barua za utambulisho.
“Kwahiyo tuliwakuta kwenye vituo na wale ambao waliwapokea walishindwa kuwatofautisha kuwa yupi ni yupi halisi, kwahiyo tumekumbwa na changamoto hiyo na ni maeneo mengi na mimi nawafahamu mawakala wangu, lakini nikienda nakuta wakwangu wamezuiwa wale wengine wameruhusiwa na wanabarua za utambulisho..” aliongeza.
Mkuu wa mawakala wa chama hicho, ambaye pia ni mwanasheria wa mgombea huyo, Raymond Edward, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo moja ya eneo linalikubwa na changamoto hiyo ni kituo cha Mingano, na kwamba wakala wake alionyesha barua aliyopewa na Chadema mkoa.
“Lakini kitaratibu, kiongozi wa mkoa hawezi kutoa barua ya wakala kwenye kata Fulani, isipokuwa wilaya husika ndio wanatoa..nilitafuta hekima kwa baadhi ya watu akiwemo afisa uchaguzi (Msaidizi) anaitwa Kambili, tulipowasiliana naye alikiri kuuona huo mkanganyiko mapema, lakini walichoamua ni kumpokea Yule wakwanza kupeleka barua kutoka wialayani au mkoani na anyechelewa hawapokei.” alisema
Alisema, kwasasa wanajaribu kuwasiliana na uongozi wa chama wa ngazi za juu ili kuwaeleza hali ilivyo, huku wakijaribu kuwapaelekezo mawakala wale waliopo ili kujua namna ya kufanya na mambo mengine ya kisheria.
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Mtwara mjini, Limbakisye Shimwela, alikiri kutambua utata huo huku akihusisha na mgogoro wa ndani ya chama kati ya uongozi wa wilaya na mkoa, ambao manispaa haiwezi kuingilia.
“Sisi hatukumuapisha mtu ambaye hakuletwa na chama, barua ililetwa ambaye ilisainiwa na katibu wao wa chama wa wilaya, kwahiyo kama kuna maeneo mengine wanasema sio mawakala wao, labda sio kwasababu ya makundi yao ndani ya chama ambayo sisi hatuwezi kuyaingilia.” Alisema.
Aidha, alisema hali ya uchaguzi inaendelea vizuri katika jimbo hilo ambapo katika baadhi ya vituo ambavyo ametembelea amekuta hari ya utulivu huku sehemu nyingine zikiwa na watu wachache na nyingine kuwa na idadi kubwa ya watu.



No comments: