Kipeperushi kikionyesha ujumbe wa uchochezi kwa wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, kiasi cha kuwafanya baadhi yao kushikwa na hofu wakati wa uchaguzi |
Na Juma Mohamed.
IKIWA
imebaki siku moja ili ufanyike uchaguzi, hofu ya usalama kwa wananchi wa
manispaa ya Mtwara Mikindani imezidi kutanda kiasi cha kusababisha wengi wao
kuzidi kuhama mjini na kuelekea maeneo yao ya asili hasa vijijini.
Hali hiyo
ilianza kujitokeza siku nne zilizopita kwa baadhi ya wakazi wa manispaa hiyo
wengi wao wakiwa kina mama na watoto, huku ikitajwa kuwa ni hofu ya usalama wao
kutokana na kuhofia kuzuka kwa vurugu siku ya uchaguzi, Jumapili ya Oktoba 25.
Kwa mujibu
wa wananchi hao, hali hiyo imesababishwa na askari polisi na Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) kuzunguka mitaani kwa ajili ya kufanya mazoezi wakiwa na silaha
zao.
Akizungumza
katika kikao na waandishi wa habari na viongozi wa vyama vya siasa, Kamanda wa
Pilisi Mkoa wa Mtwara ASP-Henry Mwaibambe, aliwataka wananchi hao kutokuwa na
wasiwasi wowote juu ya askari kuzunguka mitaani, akisema kuwa suala la kufanya
mazoezi ni la kawaida.
Akijibu hoja
iliyotolewa na Mgombea Udiwani wa Kata ya Dihimba, Mtwara vijijini, Ismail
Liuye, ya kuwataka askari kutoa taarifa kwa wananchi wanapotaka kufanya mazoezi
au jambo lolote ambalo litawashtua wananchi ili kuhepusha wasiwasi miongoni
mwao, alisema jeshi la polisi wana haki ya kufanya hivyo lakini sio kwa JWTZ
ambao wanauwezo wa kufanya mazoezi wakati wowote na mahali popote.
“Vyombo vya
ulinzi wanapofanya mazoezi sio lazima mshirikishwe..sisi polisi kwasababu
tunamtandao mpana tuna mapolisi kata, tuna mapolisi chungu mzima kwahiyo ni
rahisi kuwaambia lakini wanajeshi hawana mamlaka hiyo, na sio lazima wewe
wakuambie kwamba leo tutakuwa Chikongola, wao taratibu zao haziwaruhusu na
wanaouwezo wa kufanya mazoezi mahali popote pale..” alisema.
Alisema,
katika usimamizi wa uchaguzi wanaohusika ni askari polisi, mgambo, askari
magereza na uhamiaji na kwamba Jeshi halina mamlaka ya kusimamia uchaguzi
kwahiyo hayo wanayoyafanya hayahusiani na uchaguzi.
Akizungumzia
suala la kuongezwa kwa magari ya Jeshi la Polisi, alisema ni jambo la kawaida
na ndio utaratibu ambao unafanyika hata katika chaguzi zilizopita, kwani ilifanyika
hivyo pia katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo yaliletwa magari 700 huku mwaka
huu yakiwa 399.
“Kwahiyo ni
utaratibu wa kawaida tu kwasababu tunahitaji kila eneo tuwe na gari..kwahiyo
naomba wananchi wetu muwaambie wasiogope kama kuna dalili zozote ambazo sio
nzuri basi tujulishane, namba za simu mmnazo na kila sehemu kutakuwa na
kiongozi lakini sio kwa ajili ya kufanya fujo.” Alisema.
Kufuatia
kusambaa kwa vipeperushi vinavyoashiria hali ya uvunjifu wa amani ambavyo
vinawashinikiza wananchi kumchagua mgombea Ubunge wa jimbo la Mtwara mjini
kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mftaha Nachuma, alisema tayari jeshi la
polisi limepata taarifa na wanavyo hivyo vipeperushi ambapo alisema wanaendelea
na uchunguzi ili kumtambua anayesamabaza.
Vipeperushi
hivyo ambavyo ambavyo vina ujumbe wa uchochezi ambao unasema “Kama amtamchagua
Maftaha Nachuma, Nyumba zenu zitachomwa moto Kazi kwenu” zinaonyesha kuzidi
kuwafanya watu waingiwe na hofu iwapo matokeo yatatangazwa tofauti na matarajio
yao.
“Alisema
sisi polisi tumepata pakuanzia kwa mara ya kwanza hiyo hiyo baada ya kupata
taarifa, na tunafahamu aliyetupigia simu kwa mara ya kwanza na tukasema kwanini
ametupigia simu yeye kwa mara ya kwanza..na vipeperushi vingi vimesambazwa
katika maeneo ya kituo cha polisi lakini tunajiuliza kwanini..” alisema
kamanda.
Kwa upande
wake, mgombea ubunge wa CUF Maftaha Nachuma, alisema anaamini hivyo vipeperushi
wanaosambaza ni wapinzani na sio watu wa Chama hicho, na wanafanya hivyo kwa
lengo la kukichafua chama na mgombea ambaye ni yeye kwasababu wanajua ndio
chama chenye nguvu katika jimbo hilo kwasasa.
“Kwahiyo
mimi naamini hawa ni wapinzani wangu wameamua kunichafua ili lengo lao wanaMtwara
ambao wanampenda Maftaha waweze kubadilisha mitazamo.” Alisema.
No comments:
Post a Comment