Wednesday, July 6, 2016

RPC MTWARA awataka madereva Bodaboda kushiriki kutokomeza uhalifu.




Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, ACP-Henry Mwaibambe, akiongea na madereva Bodaboda baada ya ufunguzi wa semina kwa madereva hao iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PPF)


Mwaibambe na Madereva Bodaboda



Na Juma Mohamed, Mtwara.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Kamishina Msaidizi wa Polisi Henry Mwaibambe amewataka madereva Bodaboda mkoani humo kushirikiana vyema na jeshi la polisi katika kutokomeza uhalifu ikiwa ni pamoja na wizi wa pikipiki.
Akizungumza katika semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Nchini (PPF) kwa madereva Bodaboda wa manispaa ya Mtwara Mikindani, alisema uhalifu wa wizi wa pikipiki umefanikiwa kutokomezwa katika wilaya zote mkoani humo lakini bado changamoto imebaki katika wilaya ya Mtwara.
“Tushirikiane naomba sana, vinginevyo hapo ‘trend’ itaendelea..nyie ndio wenye Mtwara sisi tunapita tu mnajuana vizuri, kitu hicho mimi ndio kinaniekera kidogo yani ukikaa wiki mbili Pikipiki moja inanisumbua, lakini Masasi tulishawaweza vizuri wale vijana..” alisem.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, ACP-Henry Mwaibambe, akiwa katika picha ya pamoja na madereva Bodaboda na watendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Nchini (PPF).



Kwa upande wao madereva Bodaboda, walikiri kuwapo kwa vitendo vya uhalifu ambapo wameahidi kushirikiana vyema na jeshi hilo kuutokomeza huku meneja wa PPF kanda ya kusini Kwame Temu akieleza lengo la semina hiyo pamoja na manufaa watakayopata madereva hao kupitia mfumo mpya wa Wote Scheme.
Khamisi Abdallah, alisema anaungana na Kamanda huyo kwa kulikemea suala hilo na kuwataka wenzake kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa mapema mara baada ya kubaini kutokea kwa uhalifu huku akiliomba jeshi hilo kutopuuzia taarifa pindi watakapopatiwa.
Aidha, wengine waliupongeza mfuko wa PPF kwa kuwapatia semina ambayo wanaamini kutokana na shughuli zao kuwa miongoni mwa vipaumbele vilivyopo katika mfumo wa Wote Scheme, wameona itakuwa ni msaada mkubwa sana kwao.
“Kutokana na shughuli zetu hizi kwasababu hatuna bima ambayo inaweza kutuongoza katika mazingira haya ya matizo yanapokuwa yametukuta, kwahiyo mimi kwanza napongeza PPF kwa kuweza kuliangalia hili kwa kuliangalia kwa mapana na kuweza kutuunganisha sisi madereva bodaboda ili watupe elimu kwa maana ya sisi wenyewe tukishapokea basi tutakuwa rasmi kujiunga na mfuko huu..” alisema Omary Mbonde.

Meneja wa PPF kanda ya Kusini, Kwameh Temu, akiongea na wanabarai (hawapo pichani) baada ya ufunguzi wa semina kwa madereva Bodaboda.



Naye, meneja wa PPF kanda ya Kusini, Kwameh Temu, aliezea lengo la semina hiyo kuwa ni pamoja na manufaa watakayopata madereva hao kupitia mfumo mpya wa Wote Scheme.
“Tumeandaa semina hii kwa ajili ya vijana wa Bodaboda mkoa wa Mtwara ili kuweza kuwapa elimu juu ya mfumo wetu mpya wa Wote Scheme ambao tuliunzisha mwaka jana..kupitia mfumo huu tunaweza kuandikisha watu ambao wapo katika sekta isiyo rasmi Wavuvi, Wakulima, Mamalishe..kwahiyo tuliona ni muhimu kuanza na kundi hili la waendesha Bodaboda kwasababu ni watu ambao wanazalisha kipato na kupata faida nyingi mbalimbali..” alisema Temu.



No comments: