Monday, July 18, 2016

Kero ya maji yawatesa wakazi wa kijiji cha Hiyari, Mtwara.




Boza ambalo linatumiwa na wakazi wa kijiji cha Hiyari, halmashauri ya wilaya ya Mtwara kwa ajili ya kuuziwa maji kwa matumizi mbalimbali.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Hiyari wanaokabiliwa na uhaba wa Maji wakiwa katika shughuli zao za kila siku.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

Adha ya uhaba wa maji safi na salama ni moja ya changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wananchi wa kijiji cha Hiayari, halmashauri ya wilaya ya Mtwara hali ambayo inawalazimu kununua Ndoo moja kwa shilingi Miatano.
Wakizungumza na Juma News kijijini hapo, wananchi hao wameiomba serikali kufanya jitihada za dhati kutatua tatizo hilo ambalo linawafanya washindwe kuoga na kufanya shughuli zingine zinazo hitaji huduma hiyo.
“Hapa sisi tuna shida ya maji ndoo moja sh. 500, tunashindwa kuoga na unaweza ukakaa kutwa maji hayajaletwa, maji tunanunua kwenye maboza kwahiyo unaweza ukakaa mpaka yaje maboza ndio tupate maji..” alisema Mariam Hemed.
Naye, Matonya Peater, alionesha kushangazwa na kijiji hicho kukosa maji wakati kuna kiwanda kikubwa cha Saruji cha Dangote Industries Limited jambo ambalo lingesaidia kuondoa kero mbalimbali za kijamii kwa wananchi wake.

Miongoni mwa wazee wanaokabiliwa na uhaba wa maji katika kijiji cha Hiyari.



Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohamed Namkopa amesema kuwa tatizo hilo linatokana na uchakavu wa mitambo ya mradi wa Maji wa Mbuo-Mkunwa ambao awali ulikuwa unahudumia vijiji vichache kabla ya kufikia kutoa huduma kwenye vijiji 14.
“Sasa hivi kuna changamoto ambazo zipo, changamoto ya kwanza ni huu mradi wa muda mrefu, una muda mrefu haujafanyiwa matengenezo..changamoto ya pili ni ongezeko la watu wapo wengi..” alisema Namkopa.
 Naye afisa habari wa halmashauri ya wilaya hiyo Isack Bilali alisema kuwa halmashauri imeshatambua changamoto hiyo na kwamba bado inaendelea na mikakati ya kutatua tatizo hilo.
“Sisi kama halmashauri tumeliona hilo na katika mipango yetu tunaendelea kuhakikisha tunaimarisha upatikanaji huo wa maji na unaendelea kuwa bora kama ilivyokuwa zamani.” Alisema.
Kijiji hicho kimezunguka kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited ambacho kuwapo kwake kimetoa matumaini makubwa kwa wananchi juu ya kupata ajira pamoja na kuondokana na kero mbalimbali za huduma za kijamii.

No comments: