Wednesday, June 29, 2016

Polisi Mtwara wamfikisha mahakamani mkazi wa Kimara kwa kutaka kuiibia Benki.




Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe


Na Juma Mohamed, Mtwara.

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemfikisha mahakamani John Venans mkazi wa Kimara jijini Dar Es salaam, kwa makosa ya kughushi nyaraka mbalimbali na kujaribu kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, katika benki ya Posta wilayani Masasi mkoani humo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Henry Mwaibambe,  mapema leo amewaambia waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo akiwa na nyaraka za bandia alikwenda katika Benki hiyo kwa lengo la kupatiwa mkopo wa sh. Milioni 9 akitumia majina ya Abel Nchaila, ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari.
"Akiwa na nyaraka za bandia alienda katika benki ya Posta tawi la Masasi, kwa ajili ya kupewa mkopo wa sh. Milioni 9 akijifanya yeye ni mwalimu aitwaye Abel Mrahasi Nchaila ambaye ni mwalimu wa shule sekondari Mangaki wilaya ya Masasi..aliwasilisha hizo documents zikiwa na vielelezo vyote pamoja na 'salary slip', barua kutoka kwa afisa utumishi na barua kutoka kwa mkuu wa shule ya sekondari ya Mangaki.." alisema.
Aidha, Mwaibambe amewataka watumishi wa serikali na taasisi za kifedha kuwa waangalifu katika kuhakiki nyaraka za watumishi ili kuhepukana na matukio kama hayo ambayo matokeo yake ni kuisababishia hasara serikali.
"Ni vyema mtu aneomba mkopo, wahusika 'Bankers' wafanye utafiti je huyo anaeomba kweli ni mtumishi halali wa serikali?..sio suala la barua ya utambulisho, barua ya utambulisho kwenye suala la huyu John Venans ina muhuri kabisa wa mkurugenzi lakini ni fojari, 'signature' fojari.." aliongeza Mwaibambe.
Mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 24 amefikisha mahakamani June 24 na kwamba kesi yake inatarajiwa kuanza kusikilizwa Julai 11 mwaka huu.



No comments: