Thursday, June 30, 2016

Mkoa wa Mtwara wakamilisha madawati kwa zaidi ya asilimia 100.



Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akiwa amekaa katika dawati ikiwa ni katika moja ya ziara zake za kukagua zoezi la uchongaji wa samani hizo.


Juma Mohamed, Mtwara
Ikiwa leo ndio mwisho wa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli juu ya kumaliza changamoto ya uhaba wa madawati nchini kwa shule za msingi na sekondari, mkoa wa Mtwara umefikia na kupitisha lengo kwa asilimia 2.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alisema awali mkoa ulikuwa na hitaji la madawati 28,890 ambapo mpaka kufikia leo jumla ya madawati 29,333 yametengenezwa na kufanya kumaliza tatizo kwa asilimia 100.
“Kwahiyo tumetimiza lengo kwa asilimia 100 na tuna madawati yaliyobaki ziada 443..kwa upande wa shule za msingi tuna ziada ya madawati 215 na upande wa sekondari tuna ziada ya madawati 228..ninaamini ndani ya wiki mbili zijazo ziada itaongezeka kwasababu yapo madawati mengine tunaendelea kupokea kutoka kwa wadau mbalimbali.” Alisema Dendego mbele ya waandishi wa habari.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego akiwa katika moja ya ziara zake za kukagua madawati. Kushoto ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa.

Aidha, aliwataka wakuu wa shule na walimu wakuu kuhakikisha wanayatunza vizuri madawati hayo na kuongeza kuwa hatokuwa na huruma kwa yeyote ambaye atabainika kuwa na ufujaji wa samani hizo.
“Lakini niwaagize pia wakuu wa shule kuhakikisha madawati haya wanayatunza, wakati tunaanza zoezi hilo mkoa ulikuwa una upungufu wa madawati Zaidi ya elfu 50 lakini pia tuliangalia upungufu mwingine ulitokana tu dawati limetoka mbao moja au mbili kwahiyo na wenyewe wawe na tabia ya kurekebisha pale yanapoharibika kuliko kuacha yaharibike kabisa..” aliongeza.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego.

Kwa upande wao, wanafunzi, walimu na wazazi mkoani humo wamepongeza jitihada za serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali kwa kukamilisha suala hilo ambalo wanaamini litasaidia kuhamasisha wanafunzi kupenda shule pamoja na kukua kwa taaluma.
Adam Mtavangu, ambaye ni mwalimu katika shule ya sekondari ya Shangani, licha ya kuipongeza serikali ya mkoa na wadau wake kwa kufanikisha zoezi hilo, anawataka wananchi kutokuwa na tabia ya kuiachia serikali pekee katika masuala ya kimaendeleo kama hayo.

Mwalimu katika shule ya sekondari ya Shangani manispaa ya Mtwara Mikindani, Adam Mtavangu.

“Suala la utengenezaji wa madawati lisiachiwe tu kuwa suala la serikali, tatizo hili lilikuwa dogo hapo mwanzo lakini liliachwa hadi kufikia kuwa kubwa kiasi kwamba likaleta mtazamo kwamba litazamwe kitaifa zaidi..” anasema.
Agizo la kutatua uhaba wa madawati nchini kwa shule za msingi na sekondari lilitolewa na Rais Magufuli mwezi machi mwaka huu.

No comments: