Thursday, May 26, 2016

Wagonjwa Kitere wakosa huduma za upasuaji kwa uhaba wa madaktari.


Wagonjwa katika kituo cha afya cha kata ya Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara wakisubiri kupata huduma za matibabu kutoka kwa daktari.



Mganga mkuu wa kituo cha afya cha Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Dkt. Dickson Hokololo, akisoma taarifa ya kituo hicho mbele ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego ambaye alifanya ziara ya kikazi kituoni hapo.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

UHABA wa watumishi, dawa pamoja na ukosefu wa maji ni miongoni mwa changamoto zilizopo katika kituo cha afya cha kata ya Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara, kiasi cha kusababisha kushindwa kutoa huduma za upasuaji.
Wakizungumza kituoni hapo, wananchi wa kata hiyo walisema bado hawajajua kwanini kituo hicho hakina maji wakati tayari kuna kisima, huku wengine wakidai kuwa wanapata adha ya usafiri wakati wa kwenda kujifungua mjini Mtwara kutokana na miundombinu mibovu ya barabara.
“Sisi bwana tuna tatizo la maji, maji kama ingekuwa wakati wake hakika kukupa unywe utashindwa jinsi ya kufanya..leo hii mwanamke anaweza kuzaa hapa akapata mashaka maji aende akachote Mmambi ili apate huduma ya maji, sisi tunashida ya maji..kwanza kuna maji yanayosukumwa kutoka Lilido hayatakiwi mashine..” alisema Mohamed Kalias, mkazi wa Kitere.
Amina Mohamed, alisema suala la kukosa huduma za upasuaji kituoni hapo kunahatarisha uhai wa kina mama na watoto kutokana na umbali uliopo kutoka Kitere mpaka hospitali ya rufaa ya Ligula iliyopo mjini Mtwara na miundombinu duni ya usafiri.
Mganga mkuu wa kituo hicho, Dkt. Dickson Hokololo alimweleza changamoto hizo mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, ambaye amefika kituoni hapo kukagua utendaji kazi na kusikiliza changamoto zilizopo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akiwa katika jengo la upasuaji katika kituo cha afya cha Kitere, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, na kutoa maagizo kwa uongozi wa kituo hicho pamoja na wa halmashauri kuhakikisha jengo hilo ambalo limekamilika linaanza kutumika kutoa huduma za upasuaji.



“Tuna uhaba wa dawa, vifaa tiba na upungufu wa watumishi..changamoto nyingine ni tatizo la upatikanaji wa maji hasa baada ya msimu wa masika kumalizika na huduma ya gari la wagonjwa kutokuwa na uhakika..” alisema.
Hata hivyo mkuu wa mkoa alitoa siku 20 kwa uongozi wa kituo hicho kuhakikisha kinaanza kutoa huduma hizo na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kina mama wajawazito kufuata huduma za upasuaji mjini Mtwara.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego akiwa katika ziara ya kikazi katika kituo cha afya cha Kitere, halmashauri ya wilaya ya Mtwara kwa ajili ya kukagua utendaji



“Tukashirikiane wote kuhakikisha madaktari wanakuja, hatuwezi kusamehewa kwa hili DMO (Mganga mkuu wa wilaya) mimi sidhani kama ningelala usingizi mnajua kabisa Kitere kituo kizuri kama hiki alafu mnakaa tu mnaongeaa hamlet madaktari kwanini msihame nyie mkahamia huku..mimi matarajio yangu nitakapoondoka hapa zisizidi siku 20 hiki kituo kiwe kimeanza kufanya kazi..” alisema.
Kituo cha afya cha Kitere ni tegemeo kwa wananchi wote wa kata hiyo na vijiji jirani ambapo chumba cha upasuaji kimekalika na kina vifaa vyote vinavyohitajika isipokuwa huduma zinashindikana kutolewa kutokana na kukosa wataalamu.

 



No comments: