Sunday, April 17, 2016

Wakulima watahadharishwa uwepo wa gonjwa hatari la kuuwa mikorosho.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma, akizungumza na waandishi wa habari katika kikao maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Mnyausho uliolikumba zao la korosho.



Mtafiti kiongozi wa zao la korosho kutoka Taasisi ya Utafiti Naliendele, Mtwara, Prof. Peter Masawe, akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari juu ya uwepo wa ugonjwa wa Mnyausho ambao umelikumba zao la korosho



Na Juma Mohamed, Mtwara.

WAKULIMA wa zao la korosho nchini wametahadharishwa juu ya uwepo wa ugonjwa wa Mnyauko ambao unatajwa kuwa ni hatari zaidi katika kuuwa Mikorosho kwa kipindi kifupi mara baada ya kupata maambukizi.
Hadhari hiyo imetolewa na mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma, wakati wa utambulisho wa ugonjwa huo kwa waandishi wa habari ambao kwa kutumia vyombo vyao wakulima watapata fursa ya kuufahamu ugonjwa na kujua dalili zake.
Kutokana na ugonjwa huo kuenezwa na vimelea aina ya Uyoga vinavyojulikana kama Fusarium oxysporum vinavyojificha katika udongo wa Mikorosho iliyoathirika, mkurugenzi huyo aliwataka wakulima kusafisha majembe yao baada ya kuyatumia pamoja na kutopanda miche kutoka katika mashamba mengine.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma, akizungumza na waandishi wa habari katika kikao maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Mnyausho uliolikumba zao la korosho.


“Kwahiyo udongo wa eneo lililoathirika usihamishwe kwenda katika sehemu nyingine, na ndio maana nikasema kama mtu analima katika eneo ambalo limeathirika atoke na jembe ambalo ni safi, asije kuhamisha udongo wa sehemu moja kwenda sehemu nyingine ugonjwa utaenea eneo hadi eneo kwasababu ugonjwa upo ndani ya udongo..” alisema.
Alisema jitihada zinafanyika baina ya bodi kwa kushirikiana na wataalamu wa magonjwa ya Mikorosho kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele mkoani hapa kwa ajili ya kupata viwatilifu vya kuutokomeza na kuikinga Mikorosho.
Kwa upande wake, mtafiti mstaafu kutoka katika taasisi ya Naliendele, Dk. Shamte Shomari, alizitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mjani katika baadhi ya matawi ya mkorosho kupoteza rangi yake ya kawaida ya kijani na kubadilika kuwa njano na baadae kuwa kahawia.
Aliitaja dalili nyingine kuwa ni mkorosho ulioathirika ukitazamwa toka mbali unaonekana kama kuwa na mchanganyiko wa majani ya kijani, njano na kahawia pamoja na sehemu ya kati ya mizizi ya Mikorosho iliyoshambuliwa kuwa na rangi ya kahawia.

Mtafiti mstaafu wa Taasisi ya Utafiti ya Naliendele, Mtwara, Dkt. Shamte Shomari, akiulezea ugonjwa wa Mnyausho uliolikumba zao la korosho.


Aidha, alibainisha athari zinazotokana na vimelea hivyo kuwa ni pamoja na kuziba mirija inayopitisha maji na virutubisho toka ardhini kwenda katika majani na kuziba mirija inayopitisha chakula toka kwenye majani na kusambazwa katika sehemu mbalimbali za mkorosho kiasi cha kupelekea mkorosho kufa.
Alisema, mkorosho baada ya kupatwa na ugonjwa huo na kushindwa kupatiwa tiba ya haraka, utadumu kwa kipindi cha miezi mitatu na baada ya hapo unakufa.
Ugonjwa huo ulifahamika rasmi kwa mara ya kwanza mwaka 2012 katika kijiji cha Magawa wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, kabla ya mwaka 2014 kuonekana katika kata za Nanganga na Nangoo wilaya ya Masasi mkoani hapa na kijiji cha Mnongodi halmashauri ya wilaya ya Mtwara, huku ikisemekana kuwa upo katika baadhi ya maeneo katika mkoa wa Ruvuma.



No comments: