Sunday, April 17, 2016

Mbunge Mtwara apingana na TPDC mradi wa kusambaza gesi majumbani.

Mbunge wa Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, akiwahutubia wananchi wa Mtwara mjini walijitokeza katika uwanja wa Mashujaa kumsikiliza katika mkutano wa kuwapongeza kwa kumchagua kuwa mbunge





Mbunge wa Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, akiteremka kwenye moja ya magari yake aliyonunua kwa ajili ya kubebea wanafunzi na kuwapeleka shule na kuwarudisha, ambayo aliyatambulisha katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara. 


Mbunge wa Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, akiwahutubia wananchi wa Mtwara mjini walijitokeza katika uwanja wa Mashujaa kumsikiliza katika mkutano wa kuwapongeza kwa kumchagua kuwa mbunge


Wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara kwa ajili ya kumsikiliza Mbunge wao Maftaha Nachuma (CUF) ambaye alifanya mkutano wa kuwapongeza kwa kumchagua kuwa mbunge



Na Juma Mohamed, Mtwara.

MBUNGE wa Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, amepingana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) juu ya mikoa ya Mtwara na Lindi kuwepo katika mradi wa kusambaza gesi majumbani unaotarajiwa kutekelezwa na shirika hilo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuwapongeza wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge ulioambatana na zoezi la kutambulisha magari ya kubebea wanafunzi katika uwanja wa Mashujaa mjini hapa, alisema amepitia mpango wa shirika hilo na kujiridhisha kuwa mikoa hiyo haipo katika mradi huo.

Hotuba

Alisema, katika mpango wa mwaka 2016/2017 wa TPDC unaonesha mkakati wao wa kuongeza megawati za umeme ambazo zitatumika Tanzania nzima kupitia mradi wa bomba la gesi linalotoka Madimba mpaka Kinyerezi, Dar es Salaam lakini katika mpango wa pili ambao ni wa kusambaza gesi majumbani mikoa hiyo haipo.
“Lakini cha ajabu katika mpango wa serikali ndugu zangu pamoja na kwamba huu mkakati na utekelezaji unaanza baada ya bajeti ya mwezi wa saba mwaka huu, kusambaza mabomba ya gesi majumbani, Mtwara na Lindi ambako gesi inatoka, haipo ndugu zangu..Mtwara na Lindi inakotoka gesi kwenye ule mpango haijawekwa kwamba wanamtwara na sisi tuweze kutumia gesi kwa ajili ya kupikia na mambo mengine tuhepukane na kuni haijawekwa ndugu zangu ni mambo ya kusikitisha kwakweli..” alisema.

Nyomi


Hata hivyo, kauli hiyo ya Mbunge inapingana na maelezo yaliyotolewa na mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, James Mataragio, ambayo alimweleza Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alipofanya ziara katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba mkoani hapa Februari 27 mwaka huu kwamba “Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa na TPDC ni pamoja na mradi wa uagizaji wa mafuta ya hifadhi ya taifa, mradi wa usambazaji gesi majumbani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam..”.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) James Mataragio, akiwasilisha taarifa ya shirika hilo kwa waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, alipofanya ziara katika kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba, Mtwara.


Mbali na maelezo hayo ya mkurugenzi, Meneja wa biashara ya gesi wa shirika hilo, Emmanuel Gilbert, aliwahi kuwaeleza waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa semina ya siku moja kwa waandishi juu ya kuwajengea uwezo wa masuala ya mafuta na gesi, kuwa shirika lipo katika mchakato wa ujenzi wa mradi huo na kwamba tayari upembuzi ya kinifu katika mikoa ya Lindi na Mtwara umekamilika.

Waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akiongea jambo na mkurugenzi mtendaji wa TPDC, James Mataragio.


Alisema, mradi huo ambao utatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Lindi kwa sasa zinasubiriwa fedha kutoka serikalini kwa ajili ya kuanza zoezi la usanifu wa michoro katika maeneo yatakayopitiwa na miundombinu hiyo.
Kwa mujibu wa Gilbert, mtandao wa kutandaza mabomba wa mradi huo utakuwa na urefu wa Km 17 kwa mkoa wa Mtwara ambapo unatarajiwa kuunganisha nyumba 11,000 na magari 4,000 ambayo yatakuwa na yanauwezo wa kuamua kutumia nishati ya gesi au mafuta, na Km 11 kwa mkoa wa Lindi.

Mabasi aina ya Toyota Coaster ambayo yamenunuliwa na Mbunge wa Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, kwa ajili ya kubebea wanafunzi kuwapeleka shule na kuwarudisha.




No comments: