Saturday, April 16, 2016

Ndanda Fc yazidi kutakata Nangwanda mbele ya mkuu wa wilaya.

Wachezaji wa Ndanda Fc wakishangilia bao la pili kwa staili ya aina yake baada ya kuifunga Kagera Sugar kwa jumla ya mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopigwa jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.



Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akisalimiana na waamuzi wa mchezo wa Ndanda Na Kagera Sugar


Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akisalimiana na Nahodha wa Ndanda Kigi Makassy kabla ya kuanza kwa mchezo wao na Kagera


Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akisalimiana na mchezaji wa Kagera Sugar.





Wachezaji wa Ndanda Fc wakishangilia bao la pili baada ya kuifunga Kagera 2-0


Jackson Chove akitoka kushangilia bao


 Na Juma Mohamed, Mtwara.

TIMU ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani hapa imeendelea kuwapa raha mashabiki wake baada ya jana kuibugiza Kagera Sugar mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, na kushuhudiwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally.
Ushindi huo uliotakana na mabao mawili ya dakika za 75 na 79 ya mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo Atupele Green, unakuwa ni wa pili mfululizo baada ya wiki iliyopita kuisambaratisha Mwadui Fc ya Shinyanga mabao 2-1 katika uwanja huo na sasa kufanikiwa kufikisha alama 33 katika msimamo wakiwa nafasi ya Nane.
Mchezo wa jana uliochezeshwa na mwamuzi Endrew Shamba kutoka mkoani Pwani, ulikuwa ni wakushambuliana zamu kwa zamu katika kipindi cha kwanza ambacho kilimalizika kwa suluhu huku Ndanda wakikosa kutumia nafasi kadhaa walizozipata langoni mwa Kagera.

Kiungo wa Ndanda Fc, Bryson Raphael akijaribu kumtoka mchezaji wa Kagera Sugar.


Kipindi cha pili Ndanda walionekana kuubadilisha mchezo na kucheza kwa kasi ambapo mwalimu Malale Hamsini alifanya mabadiliko ya kuwapumzisha Salum Minelly na Bryson Raphael na nafasi zao kuzibwa na Ahmad Msumi na Omega Seme huku mwalimu Adolph Rishard wa Kagera akimpumzisha Ramadhani Kipalamoto ambaye alimpisha Rashid Simba.
Mabadiliko hayo yaliinufaisha Ndanda ambao walijipatia mabao mawili ya haraka yakipachikwa na Atupele ambaye alizitendea haki krosi za Bryson Raphael na Kigi Makassy ambapo mpaka dakika zote 90 zinamalizika ni Ndanda ndio waliibuka wababe kwa ushindi huo wa 2-0.

Bryson Raphael, akishangilia bao la Ndanda Fc katika mchezo wao dhidi ya Kagera walioibuka na ushindi wa 2-0


Kimsingi, Ndanda haijawahi kupoteza mchezo wowote mbele ya mkuu wa wilaya katika mechi zote tatu alizohudhuria katika mzunguko wa pili wa VPL ambapo mchezo wa kwanza ulikuwa dhidi ya Prisons uliomalizika kwa suluhu ya 0-0 kabla ya kuwashuhudia wakiiangamiza Mwadui 2-1 na hapo jana kuigalagaza Kagera 2-0.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akisalimiana na golikipa wa akiba wa Ndanda, Jackson Chove kabla ya kuanza kwa mchezo wao na Kagera


Baada ya mchezo huo, Juma News ilifanikiwa kuzungumza na walimu wa timu zote mbili kutaka kujua tathmini yao, ambapo mwalimu wa Kagera Sugar, Adolph Rishard alisema timu yake ilijaribu kutengeneza nafasi kadhaa lakini wachezaji hawakuweza kuzitumia huku wapinzani wao wakitumia makosa mawili yaliyofanywa na wachezaji wake na kuweza kupata ushindi.

Jackson chove na Kigi Makassy


Kuhusu mustakabali wa timu yake katika kusalia au kushuka daraja katika ligi kuu, alisema bado wanayo nafasi ya kuweza kupigania kubaki kwasababu wana michezo mitatu ambayo watacheza nyumbani hivyo anatarajia kupata matokeo mazuri.

Mussa Mbaya, ambaye ni kocha msaidizi wa Ndanda Fc, alisema siri ya mafanikio ambayo yanapatikana kwa timu yake ni umoja ulipo baina ya wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki ambao wamekuwa wakiunga mkono timu yao hata pale inateleza na kukosa matokeo.
alisema, katika mchezo huo kwa mara ya kwanza walilazimika kumtumia kijana wao waliompandisha kutoka kikosi cha vijana wa Under 20, Riphati Msuya, ambaye alionesha kiwango kizuri na kuwaondoa hofu mashabiki na wadau wengine ambao walimuona kwa mara ya kwanza akivaa jezi ya Ndanda.
"Ukiangalia mchezo wa leo kwenye 'Sub' tulikuwa na watu watatu tu wachezaji wengi ni majeruhi, na tumesajili wachezaji 21 na kama ukiangalia leo tumechezesha mchezaji mdogo kuliko wote nafikiri katika msimu wa ligi kuu..watu wengi hawakuamini kama anaweza kucheza lakini amecheza kwa dakika zote 90.."
Aidha, mfungaji wa magoli ya mchezo huo Atupele Green, alionesha kufurahishwa na kitendecho kufunga magoli mawili katika mchezo huo ambayo yamemfanya sasa kufikisha magoli 10 katika michezo yote aliyochezea Ndanda msimu huu.
Kutokana na kufikisha idadi hiyo ya mabao hadi sasa, mchezaji huyo aliyesajiliwa akitokea Kagera Sugar msimu uliopita, anaonekana kupata mafanikio mara mbili ya yale aliyopata akiwa na Kagera kwasababu huko alimaliza msimu akiwa na jumla ya magoli Matano pekee.
“Kiukweli nilikuwa na hamu sana ya kuifanya timu iwe salama katika kipindi hiki na ndio maana nimejitolea nimejituma na mwenyezi Mungu amenisaidia nimeweza kufunga magoli mawili namshukuru sana..sasa hivi nina magoli 10 kiukweli mimi ‘Striker’ na nimejitambua nimejua kazi ya ‘Striker’ ni kufunga, ili uweze kuuzika na uwe na maisha bora lazima ufunge magoli..” alisema.

Kiungo wa Kagera Sugar, Erick Kyaruzi akimtoka mshambuliaji wa Ndanda Fc, Atupele Green.


Alisema, malengo yake katika mechi tatu zilizobaki ni kuweza kufunga angalau magoli matatu huku akihitaji goli moja kwa kila mechi ili afikishe idadi ya magoli 13 na kwamba anatarajia kutimiza malengo hayo.
Baada ya mchezo wa leo, Kagera wanasalia katika nafasi ya 12 wakiwa na alama 25 katika michezo 27 waliocheza, huku Ndanda Fc wakirejea katika nafasi ya Nane baada ya kufikisha alama 33 katika michezo 27 waliocheza.
Ndanda watakuwa na mapumziko ya takribani wiki mbili kabla ya kukutana tena Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya JKT Ruvu utakaofanyika Mei 7 mwaka huu katika uwanja wa Mabatini, huku Kagera wakiwasubiri Azam siku hiyo hiyo huko Kaitaba mkoani Kagera.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja utakaopigwa katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam pale Simba Sc watakapowakaribisha Toto Africans ya Mwanza.
Matokeo ya mechi nyingine za vpl hii leo:
Yanga 1-0 Mtibwa
Coastal Union 1-0 JKT Ruvu


No comments: