Thursday, April 21, 2016

Kampuni ya uajiri Dangote yatuhumiwa.

Mwanasheria wa kampuni ya Unique Consultant Company Ltd (UCC), Robert Makwaia, akijibu hoja za wananchi



Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akiongea na wajumbe wa kikao cha ujirani mwema kilichowahusisha viongozi wa vijiji, kata na tarafa ya Mayanga, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, chenye lengo la kujenga mahusiano mazuri baina ya wananchi wanaoishi katika vijiji jirani na kiwanda cha Saruji cha Dangote, viongozi wao na uongozi wa Kiwanda hicho.


Wajumbe wa kikao cha ujirani mwema 



Na Juma Mohamed, Mtwara.

KAMPUNI ya Unique Consultant Company Limited (UCC) inayofanya kazi ya kuajiri watu katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Industry Limited mkoani hapa imelalamikiwa na wananchi kutoa ajira kwa ubaguzi na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Wakizungumza katika kikako cha ujirani mwema kilichoitishwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, ambaye aliwaita viongozi wa kiwanda hicho kwa ajili ya kujibu hoja za wananchi, walisema vijana wengi wanaoishi katika vijiji jirani na kiwanda hicho wananyimwa fursa za kuajiriwa kwa kigezo cha kutojua lugha ya kiingereza.
Kigezo cha kutojua lugha hiyo ambacho ni miongoni mwa sababu zilizoelezwa na mwanasheria wa UCC, Robert Makwaia, kilipingwa vikali na wananchi hao na kudai kuwa wapo Wachina ambao wameajiriwa huku wakiwa hawajui kiingereza wala Kiswahili.
“Nasema kwamba pale ajira zinatolewa kama sio kwa upendeleo basi kwa kutumia rushwa, kwasababu vigezo vilivyoelewa na mwanasheria wa UCC kwamba mtu anashindwa kuajiriwa eti kwasababu anakosa vigezo fulani ikiwemo kutojua lugha, sisi tumeshuhudia Wachina Mhe. Mkuu wa wilaya wamekuja pale gari wanajifunzia kwenye hii ‘High Way’ (Barabara kuu) mimi nakaa Mbuo pale..”alisema John Ngaeje, kaimu mtendaji wa kijiji cha Mbuo.
Alisema wataalamu wengi katika vitengo mbalimbali kiwandani hapo ikiwa ni pamoja na wahandisi, ni raia wa Kichina ambao awali walikuwa wanajua lugha ya Kichina pekee, wamejifunza lugha za kiingereza na Kiswahili wakiwa kazini jambo ambalo linaweza kufanyika pia kwa wakazi wa maeneo hayo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naumbu Kusini, Rashid Abdelleman akichangia mada.


Rashid Abdelleman, ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Naumbu Kusini, alisema kampuni hiyo haifai tena kuwepo kiwandani hapo kwasababu ya kutotenda haki huku akidai kuwa matangazo ya ajira kwa wakazi wa Mtwara yatolewa muda mfupi kabla ya siku ya kuanza usaili huku maeneo mengine ya nje ya Mtwara yanatolewa mapema.
“Kwahiyo kampuni hii haifai kabisa na kama watakuwa wanang’ang’ania kuna mapungufu fulani, tunaweza kwenda kiwandani ugonvi wetu ukaishie pale, waitwe wafanyakazi wote tujue kampuni ile ina wafanyakazi wangapi sasa hivi, wafanyakazi hao kulingana na idadi yao, Naumbu Kusini wangapi mimi watu wangu wote nawajua kama mwenyekiti, wa Mgao wapo wangapi..kwahiyo watu wengi wanaofanya kazi pale hawatokei kwetu..” alisema.
Ally Ahmad, alisema wakati anakaimu nafasi ya mtendaji wa kata, aliwahi kufuatwa na watu kutoka Dar es Salaam ambao walitaka kumkabidhi bahasha yenye pesa ndani kwa ajili ya kutaka awathibitishe kuwa ni wakazi wa kijiji cha Hiyari, ili waweze kupata ajira kirahisi kiwandani hapo huku wakidai kuwa wameagizwa na watu wa UCC na afisa muajiri wa kiwanda (H/R).

Meneja rasilimali watu na utawala wa kampuni ya Saruji ya Dangote Industry Ltd Mtwara, Gervacy Chapalwa, akifafanua jambo.


“Hilo suala la kuonekana hawachukui rushwa, mimi nimelishuhudia mwenyewe nakabidhiwa bahasha ya pesa na nikaikataa nikasema ndugu zangu hawajapata ajira, ninakukabidhije wewe barua ya kukuthibitisha kwamba wewe ni mzawa wa hapa wakati hauna kitambulisho chochote cha kuonesha wewe unatoka wapi, unaishi sehemu gani na unautaratibu gani..” alisema Ahmad.
Akijibu hoja hizo, Mwanasheria huyo alisema suala la kigezo cha lugha ni sehemu tu ya vigezo vinavyohitajika na kwamba vipo vingine vingi vinavyohitajika ambapo hata hivyo hakuweka wazi vigezo gani vingine vinavyohitajika.
“Tunapokuwa tunafanya ‘interview’ jamani, sio kwamba ile barua inavyokuja mtu unajua kwamba huyu anatoka kijiji fulani hapana, inakua tu imekaa pale barua unaiangalia na CV yake wewe unaendelea na ‘procedure’ zingine..kwahiyo tukisema tuchague kwa kijiji kwamba tumchukue fulani na tumuache fulani hapana hatutaweza kufka hivyo..” alisema Makwaia.
Kuhusu tuhuma za rushwa, alisema hazina ukweli na kwamba mtoa hoja inawezekana ametunga tu katika kikao hicho kwasababu alikuwa na uwezo wa kwenda kuthibitisha katika ofisi za UCC kwakuwa alikua na bahasha yenye pesa hizo.
“Alitakiwa hata kuja ofisini kuja kujihakikishia kabisa kwamba je huyo mtu alidhamiria hapa na huyo mlengwa ni huyu hapa UCC?..kwahiyo anachokisema naweza kusema kwamba ni porojo tu, kaka ofisini tu yeye mwenyewe au katunga tu hapa..” alisema.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa miongoni mwa wananchi juu ya kuwapo kwa vitendo vya rushwa kiwandani hapo na kudai kuwa vitendo hivyo vipo pia katika ngazi za vijiji, kata mpaka tarafa ambapo aliahidi katika kiako kijacho cha tarafa atamwalika kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mtwara kwa ajili ya kutoa elimu ya kuripoti vitendo vya rushwa.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally.

“Ninaamini timu yangu ya TAKUKURU itahamia huku Chapalwa (Menejea rasilimali watu), kwasababu hizi tuhuma za rushwa sisi kama serikali hatuwezi kuziacha hivihivi lazima tutazifanyia kazi..lakini taarifa ambayo nimeipokea ni kwamba rushwa haipo kiwandani tu, mpaka kwa watendaji, nimepokea kwa maandishi mjumbe mmoja mwema ameniandikia..” alisema mkuu wa wilaya.





No comments: