Friday, April 22, 2016

Kamati ya uchaguzi MTWAREFA yaahidi kutenda haki.


Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Hussein Kingi (Kulia) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu taratibu za uchukuaji na kurejesha fomu za uchaguzi. Kushoto ni mjumbe wa kamati hiyo, Selemani Kachele.


Ratiba ya uchaguzi



Na Juma Mohamed, Mtwara.

KAMATI ya uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), imeahidi kutenda haki na kufuata kanuni na sheria zilizopo katika katiba ya chama hicho na vyama vingine vya juu, ili mchakato wa uchaguzi ulioanza juzi umalizike salama.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika ofisi za Mtwarefa, mwenyekiti wa kamati hiyo, Hussein Kingi, alisema kamati itahakikisha inafuata yale yaliyoelekezwa kwenye katiba na kanuni za uchaguzi na kwamba kitendeo cha kukiuka hayo ni kukaribisha malalamiko kutoka kwa wagombea yatakayopelekea watu kukata rufaa na kuweka mapingamizi.
“Kwahiyo tunawathibitishia ndugu zetu, hatutakenda nje ya kanuni na katiba ya Mtwarefa na TFF, CECAFA mpaka CAF na FIFA..sisi katiba na kanuni kama hazifanyi kazi za wilaya zinafanya kazi za mkoa, kama za mkoa hazifanyi kazi zinafanya kazi za CECAFA, kama za CECAFA hazifanyi kazi zinafanya kazi za CAF na kama za CAF hazifanyi kazi zinafanya kazi za FIFA..” alisema Kingi.
Alisema, tangazo la uchaguzi huo utakaofanyika Mei 29 mwaka huu limesambazwa katika halmashauri zote za mkoa wa Mtwara na kwamba kila mwanamichezo aliye na vigezo anawajibu wa kugombea nafasi anayohitaji.
“Kila mgombea anaetaka fomu katika ngazi ya Mtwarefa basi anatakiwa kujaza fomu ambaye ataipata kwa katibu wa Mtwarefa aliyeanza kuzitoa kuanzia leo (Juzi) lakini humo ndani kuna mtiririko ambao mjazaji anatakiwa awe na picha mbili (Passport size) ambazo moja itabandikwa kwenye fomu ile lakini vilevile anatakiwa ajaze kwa maandishi yake mwenyewe..” alisema.
Naye, mjumbe wa kamati hiyo Selemani Kachele, akizungumza kwa niaba ya katibu wa kamati, Baraka Kagema, alizitaja nafasi zinazogombewa kuwa ni nafasi ya mwenyekiti na makamu wake, katibu na makamu wake, mweka hazina, mwakilishi wa mkutano mkuu wa TFF na mwakilishi wa vilabu katika mkutano mkuu wa TFF.
Alisema, nafasi hizo ada yake ya kuchukulia fomu ni sh. 300,000 huku akitaja nafasi nyingine Tatu za wajumbe wa kamati ya utendaji ambazo ada yake ni sh. 200,000.
“Sifa za wagombea, kwanza awe raia wa Tanzania, awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha Nne na cheti cha elimu ya sekondari, awe za uzoefu wa mpira wa miguu uliothibitishwa wa angalau miaka Mitatu, asiwe na hatia ya kosa la jinai la kuhukumiwa kifungo bila ya uchaguzi wa faini..” alisema.
Aliongeza kwa kutaja vigezo vingine kuwa ni pamoja na mgombea awe na umri unaoanzia miaka 21 na kuendelea, awe amewahi kuwa mchezaji wa mpira wa miguu, kocha, mwamuzi au kushiriki katika uendeshaji wa mpira wa miguu.
Aidha, zoezi la uchukuaji na kurudisha fomu za uchaguzi huo limeanza juzi Aprili 21 na litafikia mwisho Aprili 24 mwaka huu saa 10:00 jioni.



No comments: