Tuesday, March 1, 2016

Serikali mkoani Mtwara yasema uwekezaji utawanufaisha wananchi wake.


Katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda, akifunua kitambaa kilichofunikwa katika jiwe la msingi la ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhia vifaa vitakavyotumiwa na makampuni ya utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi mkoani Mtwara.


Katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhia vifaa vitakavyotumiwa na kampuni za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi mkoani Mtwara, kinachojengwa katika eneo la Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji





Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI mkoani hapa imesema inamatumaini makubwa kwa wananchi wake kuwa watanufaika na shughuli za uwekezaji zinazoendelea kufanyika kwa kujishughulisha na njia mbalimbali za kujiingizia kipato kitakachotokana na fursa za uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego katika zoezi la uzinduzi wa kituo kikubwa cha uwekezaji cha kuhifadhia vitendea kazi mbalimbali vitakavyotumiwa na makampuni yanayofanya shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luwanda, alisema mahitaji ya bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuku na mbogamboga yatakuwa makubwa hivyo ni fursa kwa wananchi kuweza kuzitumia.
“Tunapoona makampuni yanakuja kwa wingi, hawa watahitaji chakula, watahitaji mbogamboga, watahitaji matunda na vingine..sasa hivi vitu kama havitokuwepo katika maeneo haya watakaonufaika watakuwa ni watu wengine..kwahiyo sisi kama mkoa tuligemea kuona wawekezaji zaidi kutoka nje wakija kuwekeza katika shughuli au masuala yanayoendana na gesi..” alisema.
Alisisitiza kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana katika kuwaandaa wananchi kifikra na kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kuwa na uelewa zaidi juu ya namna watakavyonufaika na rasiimali hizo ambazo faida yake huchukua muda mpaka mwananchi kuanza kuiona.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA), Kanali Mstaafu Joseph Simakalia, alisema kituo hicho kinachojengwa katika eneo hilo kitatumiwa na makampuni yanayojihusisha na shughuli hizo kutoka katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati na zile za ukanda wa SADC isipokuwa nchi ya Angola.
Alisema, hatua ya kituo hicho kuja kujengwa Tanzania imetokana na makubaliano ya nchi hizo kutokana na kufanya tathmini ya kupata eneo ambalo litakuwa la katikati kwa nchi zote na lenye mahitaji muhimu kutokana na shughuli zao ikiwa ni pamoja na bandari ya uhakika na rasilimali za gesi na mafuta.
‘Kwahiyo Tanzania imekaa katikati, kwamba tukiweka kituo kikubwa cha kudumu Tanzania kwamba mahitaji yote yanawekwa pale alafu anaehitaji kwa kiasi anachotaka anapelekewa ikaonekana ni Tanzania na sehemu yenyewe ni Mtwara, kwasababu bidhaa nyingi zitakuja kwa bahari na zitasafirishwa majini na Mtwara kuna bahari alafu vilevile Mtwara yenyewe ina gesi..kwahiyo ni kama Mungu amependelea Mtwara ina kila sababu ya hicho kituo kiwekwe hapa..” alisema.
Alisema, kwa uwepo wa lituo hicho, mkoa utanufaika kwa kujiongea makusanyo ya mapato yatokanayo na bandari kwasabau bandari itatumika zaidi kuliko ilivyo sasa, na kuongezeka kwa ajira katika bandari hiyo ambayo ndio itatumika kwa meli kubwa zitakazo beba vifaa hivyo.
Eneo hilo ambalo ni mali ya EPZA lina ukubwa wa heka 3.5 na kwamba ujenzi wake unatarajiwa kuanza wiki hii.



No comments: