Monday, February 29, 2016

Tanzania yaokoa dola Bil. 1 kutokana na matumizi ya gesi asilia.


Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akielekezwa jambo na mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) James Mataragio, alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichopo Madimba, Mtwara



Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akiwa katika ziara ya kuzunguka sehemu mbalimbali za kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichopo Madimba, Mtwara kujionea namna ambavyo shughuli za uzalishaji zinavyofanyika katika mitambo hiyo. 



Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali, wabunge na wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) baada ya kumaliza ziara ya kuzunguka sehemu mbalimbali za kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichopo Madimba, Mtwara kujionea namna ambavyo shughuli za uzalishaji zinavyofanyika katika mitambo hiyo.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

KUTOKANA na matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme, Tanzania inaokoa matumizi ya fedha za kigeni dola Bilioni 1 kwa mwaka ambazo zilikuwa zikitumika kununulia mafuta mazito kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme.
Hayo yemeelezwa na mkurugenzi mtendaji wa Shrika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio, wakati akitoa taarifa ya utendaji ya shirika hilo kwa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, alipotembelea katika kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Madimba mkoani hapa.
Alisema, uzinduzi wa miundombinu hiyo ambao ulifanywa mwezi Oktoba mwaka jana na Rais wa awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, umekuwa ni suluhisho la upatikanaji wa nisahti ya umeme hapa nchini kwani asilimia 60 ya umeme unaozalishwa unatokana na gesi asilia.
“Kwa sasa tunazalisha wastani wa futi za ujazo milioni 45-50 kwa siku hapa Madimba..hata hivyo uwezo wetu ni kuzalisha futi za ujazo milioni 130 kwa siku kutoka katika visima Vitano vya gesi asilia vilivyopo eneo la Mnazi Bay.” Alisema Mataragio na kuongeza:
“Ujio wa mradi huu umetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 170 ambapo kati ya hizo 100 ni za wazawa toka mikoa ya Lindi na Mtwara, aidha kampuni zote zinazohusika katika kutoa huduma ni za Kitanzania zenye matawi/ofisi hapa Mtwara..” aliongeza.
Alisema, mradi mwingine mkubwa unaotekelezwa na TPDC kwa sasa ni ule wa kujenga mtambo wa kusindika gesi asilia nchi kavu kwa ajili ya matumizi ya ndani na kusafirisha nje ya nchi (LNG).
Alisema, mradi huo unajengwa katika eneo la Likong’o mkoani Lindi na kwamba baada ya kupatikana kwa ardhi, TPDC, wawekezaji na Serikali kupitia wizara ya Nishati na Madini wanaendelea na hatua mbalimbali zitakazowezesha kufanikisha mradi kwa lengo la kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kwa ajili ya soko la nje na sehemu ya gesi nyingine kutumika nchini.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akiwa katika ziara ya kuzunguka sehemu mbalimbali za kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichopo Madimba, Mtwara kujionea namna ambavyo shughuli za uzalishaji zinavyofanyika katika mitambo hiyo. 


“Hii itafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Tanzania na hasa kwa wakazi wa Mtwara na Lindi..wawekezaji katika mradi huu wa aina yake hapa nchini unakadiriwa kutumia takribani dola za Marekani bilioni 30-40 ambapo umelenga kuendeleza gesi asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha bahari (47.O8 TCF)..alisema.
Waziri mkuu ambaye alizunguka sehemu mbalimbali za kiwanda hicho kujionea namna ambavyo shughuli za uzalishaji zinavyofanyika, aliwapongeza viongozi wa TPDC na wafanyakazi wa kiwanda hicho na kusema kuwa serikali inatambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa katika sekta ya hiyo huku juhudi zao zikionekana.
“Jitihada za kuzalisha umeme kupitia gesi ni kubwa sana ambazo mnazifanya na tuna matumaini makubwa..haya yote ambayo tunayangumza kwenye majukwaa ya kuwahakikishia Watanzania kwamba watapata umeme eneo kubwa ambalo tunalizungumzia ni hili la gesi ambayo tunayo na imeshaanza kwenda Kinyerezi na niseme tu kwamba wananchi hawa sasa wanafarijika..” alisema.




No comments: