Thursday, October 22, 2015

Mashabiki: Bora kufungwa na Azam kuliko kusuluhu na Toto.


Mlinzi wa Azam Fc, Pascal Wawa, akiruka juu kuwania mpira dhidi ya mshambuliaji wa Ndanda Fc, Atupele Gree, katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliochezwa jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. Azam walishinda kwa goli 1-0.


Kikosi cha Ndanda Fc kilichoanza katika mchezo dhidi ya Azam Fc jana.


Wachezaji wa Azam Fc wakiwasalimia mashabiki wao waliosafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Mtwara kwa ajili kuishangilia timu yao, walipomenyana na Ndanda Fc ya Mtwara



Nahodha wa Azam Fc, Himid Mao, akichuana na Nahodha mwenzie wa Ndanda Fc, Kiggi Makassy 


Na Juma Mohamed.

LICHA ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Azam Fc ya jijini Dar es Salaa kwa goli 1-0, mashabiki wa timu ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani hapa wameonyesha kufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji ambao walionekana kucheza kwa kujituma zaidi.
Akizungumza baada ya kumalizika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara kati ya timu hizo uliochezwa jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani hapa, shabiki aliyejitambulisha kwa jina moja la Magita, alisema matokeo hayo sio mabaya kwa mashabiki ukilinganisha na matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Toto Africans ya mwanza.
Alisema, Azam walistaili kupata matokeo ya ushindi kutokana na ubora wa timu yao na aina ya wachezaji walionao, lakini Ndanda walipaswa kuwafunga Toto Africans kutokana na kuwa ni timu ngeni katika ligi ambayo wachezaji walionao hawanatofauti na wa timu ya Ndanda.

Heka heka katika lango la Ndanda.


“Matokeo siyo mabaya lakini tunaulaumu sana uongozi wetu kutokana na kuelekeza nguvu nyingi kwenye timu kubwa lakini zinapokuja timu ndogo tunatoka nao droo (sare) au wanakuja kutufunga hapa..yani mimi kama mdau, viongozi wa Ndanda wanavyofanya sio vizuri..” alisema.
Alisema, Ndanda wanapaswa kutumia vema michezo wanayocheza katika uwanja wa nyumbani kwa kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi, kwasababu viwanja vya ugenini vigumu kufanya hivyo.
Akizungumza baada ya kumalizika mchezo huo, kocha wa Ndanda, Hamimu Mawazo, alisema hakufurahishwa na matokeo waliyopata, lakini bado anaimani na kikosi chake na kukiri licha ya mapungufu yaliyopo katika baadhi ya maeneo hasa katika umaliziaji, walicheza vizuri na walionekana kutoa upinzani hasa katika sehemu ya kiungo.
“Haya ni moja ya matokeo ya mpira, lakini tuliweza ‘ku dominate’ kwenye uwanja kwa muda mrefu na tulikuwa na mashambulizi ya kutosha katika goli lao, lakini hatukuweza kuzitumia vizuri nafasi hizo huku wenzetu waliitumia nafasi moja basi ndio mpira..sina kwa kulalamikia wala kusikitikia kwasababu ndio mchezo umekwisha na tumepoteza..” alisema.

Mashabiki waliojitokeza kutazama mechi ya Ndanda na Azam, Nangwanda Sijaona, Mtwara


Alisema, kumekuwa na utofauti kati ya kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji katika mchezo uliopita na Toto Africans ambao walilazimishwa sare na mchezo dhidi ya Azam huku akikiri kuwa na tatizo katika idara ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na Atupele Green.
Aliutaka uongozi wa timu hiyo kujitahidi katika usajili ujao wa dirisha dogo ili kuongeza nguvu katika idara hiyo ambayo inaifanya timu kuwa na ukame wa mabo.
Kwa upande wake, kocha msaidizi wa kikosi cha Azam Fc ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Ndanda msimu uliopita, Benis Kitambi, alikiri kuwa na changamoto ya ufungaji wa magoli mengi katika timu yao kiasi cha kuwafanya vinara wa ligi hiyo Yanga Sc kuwazidi kwa idadi ya magoli na wao kusalia katika nafasi ya pili.

Mshambuliaji wa Ndanda Fc, Atupele Green akikimbilia mpira.


Alisema, benchi la ufundi tayari wameshaliona hilo na sasa linafanyiwa kazi ili kuhakikisha katika michezo inayofuata wanapata magoli mengi hasa wanapokutana na timu dhaifu, kama ilivyo kwa Yanga ambao waliwafunga magoli 4 Toto Africans.
“Hilo tumekiri kwamba inabidi tulifanyie kazi, utofauti uliyopo kati yetu na Yanga ni kwamba wao wanapocheza na timu dhaifu niseme, wanapata magoli mengi kwahiyo na sisi kama leo tumepata nafasi nyingi lakini hatukuweza kuzitumia..” alisema.
Kuhusu ushindi wa kwanza katika uwanja wa Nangwanda, alisema ni jambo la kawaida kwasababu Ndanda sio kwamba wameshinda michezo mingi dhidi yao katika uwanja huo lakini ni mchezo mmoja pekee katika msimu uliopita ambapo hata na wao walishinda waliporudiana katika uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar es Salaam.
Ndanda watacheza na Stand United ya Shinyanga katika mchezo unaofuata na wataendelea kusalia katika uwanja wa Nyumbani huku Azam wakitarajiwa kupambana na JKT Ruvu huko Chamanzi.



No comments: