Thursday, July 12, 2012

RAGE APASULIWA MGONGO INDIA


Rage kushoto; Hapa ni wakati anakabidhiwa madaraka na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu kabla yake, Mzee Hassan Daalal. BIN ZUBEIRY inamtakia kila la heri kiungo huyu wa zamani wa Simba na Tabora ''Mashujaa wa Unyanyembe, apone na kurejea kuendelea na shughuli zake za kila siku, zikiwemo za ujenzi wa taifa. Inshaallah.

Na Princess Asia
MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye pia ni Mbunge wa Tabora (CCM), jana amefanyiwa upasuaji wa mgongo jana katika hospitali ya APOLO, India.
Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, sababu ya Rage kufanyiwa upasuaji huo ni maradhi yanayojulikana kitaalamu kama Lumbar Disc Prolapse.
Dk Kapinga alisema Rage, ambaye pia ni mmiliki wa kituo cha Radio cha Voice Of Tabora (VOT) yuko kwa muda wiki moja nchini India akipatiwa matibabu na baada ya upasuaji huo wa jana, anaweza kupewa ruhusa kuanzia kesho kurejea nchini.
Kabla ya kuwa Mwenyekiti wa Simba SC, Rage alikuwa kiungo wa klabu hiyo miaka ya 1970 na miaka ya 1980 aliwahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu, wakati pia amekuwa Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (enzi za FAT), Makamu wa Pili wa rais wa TFFna Mjumbe wa Kamati mbalimbali za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

NDOO NNE ZA KAGAME ZILIVYOTUA YANGA, JE WATABEBA YA TANO 2012?


Kikosin cha mwisho Yanga kutwaa Kagame mwaka jana; Kutoka kulia waliosimama ni Yaw Berko, Davies Mwape, Chacha Marwa, Juma Kijiko, Jerry Tegete na Nadir Cannavaro. Walioinama ni kutoka kulia Oscar Joshua, Nsajigwa Shadrack, Godfrey Taita, Hamisi Kiiza na Nurdin Bakari.
Na Prince Akbar
MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, inatarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu yaani Jumamosi ijayo, kwa mabingwa watetezi, Yanga kufungua dimba na Athletico ya Burundi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga wanaodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, wanaingia kwenye michuano hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kutetea taji lao, baada ya kusajili wachezaji wapya nyota na kuajiri kocha mpya kutoka Ubelgiji, Thom Saintfiet.
Miongoni mwa wachezaji nyota waliosajiliwa Yanga ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Kelvin Yondan kutoka Simba SC, Simon Msuva kutoka Moro United, Said Bahanuzi kutoka Mtibwa Sugar, Frank Damayo kutoka JKT Ruvu, Ladisalus Mbogo kutoka Toto African na Nizar Khalfan aliyekuwa anacheza soka ya kulipwa Marekani.
Hao wanaungana na nyota wengine wa Yanga waliowezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mwaka jana kama kipa Yaw Berko kutoka Ghana, Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’, Nahodha Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Godfrey Taita, Rashid Gumbo, Jerry Tegete na Shamte Ally.
Lakini kikosini kuna Yanga kuna nyota wengine wa msimu uliopita, lakini hawakucheza Kombe la Kagame kama viungo Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Athumani Iddi ‘Chuji’.

SIRI YA JEURI YA YANGA
Yanga inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa kampuni ya Shivacom.
Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini Yanga Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Yanga, Simba SC, imekuwa ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za uendeshwaji wa klabu.
Na inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya kmaribuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu katika kipindi cha miaka mitano (2008, 2009 na 2011) sambamba na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.


ZANZIBAR MWAKA 1975:
Iliingia kama bingwa wa Tanzania baada ya kuifunga Simba SC katika fainali ya Ligi mwaka 1974 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, wakati watani wao hao waliingia kama mabingwa watetezi wa michuano.
Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Express ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia. Yanga ilianza kwa kuifunga Express FC mabao 4-0 na baadaye kutoka sare ya 1-1 na Mufulira, hivyo kuongoza Kundi hilo na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kukata tiketi ya kuingia fainali Janauri 13, mwaka huo ilipokutana na watani wao wa jadi, Simba SC.
Mabao ya Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 na taji la kwanza la michuano hiyo.

KAMPALA, UGANDA MWAKA 1993:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara na watano wao, Simba walikwenda kama watetezi wa taji na huko Yanga walipangwa Kundi A pamoja na wenyeji SC Villa na Malindi ya Zanzibar.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-1 na Villa, siku hiyo kabla ya kuibuka na kuifunga Malindi mabao 2-1, yote yakitiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Express FC na kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga fainali ambako ilikutana tena na SC Villa.
Kwa kuzingatia matokeo ya mchezo wa awali kwenye Kundi A, Yanga haikupewa nafasi kabisa ya kufurukuta mbele ya SC Villa, lakini mambo yalikuwa tofauti, mabao ya Said Mwamba na Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na taji la pili la michuano hiyo.
Marehemu Kizota aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.

KAMPALA, UGANDA MWAKA 1999:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara, ikiwa mwakilishi pekee na ilitua huko, huku mashabiki wengi wa soka Uganda wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichofanywa na klabu hiyo mwaka 1993.
Timu zilizoshiriki michuano hiyo ni Vital'O ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC Leopards ya Kenya, Kiyovu Sport, Rayon Sport za Rwanda,
Naadiga Dekedaha ya Somalia, KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya Sudan, Yanga, wenyeji Express na SC Villa za Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za mwishoni.
Kwa matokeo hayo, Kundi D ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu mbili tu, yaani mabingwa hao wa Bara na mabingwa watetezi.
Mechi ya kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na ziliporudiana siku mbili baadaye, Yanga walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia, mabao ya
Sekilojo Chambua dakika ya 23 na 57 na Kali Ongala dakika ya 59.
Katika Robo Fanali, Yanga ilikutana na Al Hilal Januari 10 na kushinda mabao 2-1, wafungaji Salvatory Edward dakika ya 14 na Edibily Lunyamila dakika ya 89 kwa penalti.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi Januari 13 na kushinda mabao 3-2, wafungaji Kally Ongara dakika ya 16, Bakari Malima dakika ya 78 na Said Mhando dakika ya 90.
Hivyo kwa mara ya pili, Yanga ilikutana na SC Villa kwenye fainali kukumbushia vitu vya mwaka 1993 na safari hii mambo yalikuwa mazito zaidi, kwani dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 Lunyamila akiisawazishia Yanga dakika ya 42, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kufunga dakika ya saba tu ya mchezo huo.
Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Manyika Peter akaingia kwenye orodha ya makipa hodari wa kupangua penalti baada ya kupangua mikwaju miwili, Yanga ikishinda kwa penalti 4-1, Uwanja wa Nakivubo.

DAR ES SALAAM 2011:
Yanga ilifanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Simba bao 1-0, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah aliyefunga bao hilo, pekee dakika ya 108, akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa kitaalamu na kiungo Rashid Gumbo.
Kabla ya taji hilo walilotwaa Jumapili sambamba na dola za Kimarekani 30, 000, sawa na Sh. Milioni 45 za Tanzania, Yanga walitwaa tena Kombe hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1975 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, wakiifunga Simba mabao 2-0 na baadaye mara mbili mjini Kampala, Uganda mwaka 1993 na 1999, mara zote wakiifunga SC Villa ya huko.
Ulikuwa mchezo mgumu ambao ulidumu kwa dakika 120, timu zikionyesha kucheza tahadhari, kabla ya Asamoah kumaliza kazi.
Kikosi kilichoipa Yanga kombe la nne la Kagame kilikuwa; Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’/Rashid Gumbo, Godfrey Taita/Julius Mrope, Nurdin Bakari, Davies Mwape, Jerry Tegete/Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
Yanga iliyokuwa Kundi B la michuano ya mwaka huu, ilifuzu kama kinara wa kundi baada ya kujikusanyia pointi saba kutokana na kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.
Katika Robo Fainali, Yanga ilikutana na Red Sea ya Eritrea na kushinda kwa penalti 6-5, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na St George ya Ethiopia na kushinda tena kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120, kabla ya kuiteketeza Simba SC katika fainali.
Ikumbukwe katika michuano ya mwaka huu, Yanga iliingia kama ‘viti maalumu’, kwani Simba SC ndio walikuwa wawakilishi halisi kama mabingwa wa Bara.
Ili kushiriki mashindano ya mwaka huu, ilibidi Yanga wailipe CECAFA dola za Kimarekani 20,000 kama faini ya kugomea mechi ya mshindi wa tatu wa michuano hiyo, mwaka 2008 mjini Dar es Salaam.
Yanga ilitakiwa kucheza na Simba mwaka huo kuwania nafasi ya tatu, ikiwa chini ya Mwenyekiti aliyekuwa na misimamo mikali, Wakili Imani Omar Madega, Yanga iligoma kwa sababu hawakukubaliana na TFF juu ya mgawanyo wa mapato ya milangoni.
Hivyo ndivyo Yanga ilivyotwaa mataji yake manne ya Kombe la Kagame- na Jumamosi wanaanza changamoto ya kuifukuza rekodi ya watani wao wa jadi, Simba SC waliotwaa taji hilo mara sita, je wataweza? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.


 

NDOO SITA ZA KAGAME ZILIVYOTUA MSIMBAZI, WATABEBA YA SABA 2012?


Kikosi cha mwisho Simba SC kutwaa Kombe la Kagame mwaka 2002, kutoka kulia waliosimama Shekhan Rashid, Boniface Pawasa, Selemani Matola, Geoffrey Mhando, Madaraka Selemani, Joseph Kaniki. Waliochuchumaa Sekelo Barnabas, Qureish Ufunguo, Mwameja Mohamed na Steven Mapunda Garrincha.

Na Mahmoud Zubeiry
WAKATI michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Simba SC wamepania kutwaa taji la saba.
Simba wanataka taji la saba na kwa sababu hiyo wako kwenye maandalizi ya uhakika ili michuano hiyo ikianza wawe imara waweze kutimiza ndoto zao, ambazo mwaka jana zilishindikana.
Mwaka jana, michuano hiyo ikifanyika Dar es Salaam, Simba ilimkosakosa kidogo tu mwali wa Kagame, baada ya kufungwa 1-0 katika fainali na watani wao wa jadi, Yanga katika fainali, ambayo huwezi kukosea kusema walitawala mchezo, lakini kama ilivyo ada ya soka, bahati haikuwa yao.
Simba SC imeweka kambi Zanzibar ambako pia wanashiriki michuano ya kukipima kikosi chake, Kombe la Urafiki.
Chini ya kocha wake Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick, Simba SC imeimarisha kikosi chake kwa kusajili nyota wapya kadhaa, wakiwemo nyota kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Patrick Kanu Mbivayanga anayecheza nafasi ya kiungo na beki wa kati Lino Masombo.
Simba pia imemsajili kiungo bora Afrika Mashariki na Kati, Mussa Mudde ambaye pia anaweza kucheza kama beki wa kati, wakati imesajili wazawa kama Juma Jebba kutoka Azam FC, Abdallah Juma kutoka Ruvu Shooting, Kiggi Makassy kutoka Yanga, Salim Kinje aliyekuwa anacheza Kenya sambamba na kuwarudisha kikosini wachezaji wake iliyowatoa kwa mkopo msimu uliopita Haruna Shamte na Amri Kiemba.
Kuchanganya na nyota wake wa msimu uliopita kama kipa bora Afrika Mashariki na Kati, Juma Kaseja, mwanamichezo Bora Tanzania, Shomary Kapombe, viungo wenye vipaji vya hali ya juu Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Uhuru Suleiman na washambuliaji tishio Felix Mumba Sunzu kutoka Zambia na Emmanuel Okwi kutoka Uganda, Wekundu wa Msimbazi wana uwezo wa kutimiza ndoto zao.

SIRI YA JEURI YA SIMBA SC:
Simba SC inajivunia udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake, Kilimanjaro Premeum Lager, ambao ni wa kwanza tangu wapoteze udhamini wa Mohamed Enterprises Limited.
Ikumbukwe, Kilimanjaro Premium Lager ilianza kuidhamini Simba Agosti 18, mwaka 2008, katika mkataba uliosainiwa kwenye hoteli ya Movenpick (sasa Serena), mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager, ambao ni wadhamini wakuu wa wapinzani wa jadi wa Simba, Yanga SC, imekuwa ikihakikisha udhamini wake unafika maeneo yote muhimu katika shughuli za uendeshwaji wa klabu.
Na inaaminika udhamini huo ndiyo chachu ya mafanikio ya miaka ya karibuni ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili katika kipindi cha miaka mitano (2010 na 2012) sambamba na kufika Fainali ya Klabu Bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.
Hadi sasa kwenye kabati la mataji la Simba SC, pale makao makuu ya klabu yao, kuna mataji sita ya Kombe la Kagame, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko klabu nyingine yoyote kwenye historia ya michuano hiyo, je ilitwaa vipi mataji hayo?

MWAKA 1974:
Hizi zilikuwa fainali za kwanza rasmi za michuano hiyo na zilichezwa kwa mtindo wa ligi mjini Dar es Salaam.
Simba iliipiku timu tishio enzi hizo Afrika Mashariki na Kati, Abaluhya FC ya Kenya, sasa AFC Leopards kwa kumaliza na pointi tano dhidi ya tatu za vigogo hao wa soka ya Kenya.
Ilikusanyaje pointi hizo? Ilianza kwa kuifunga 1-0 Abaluhya kabla ya kuifunga 1-0 Navy FC ya Zanzibar, kabla ya kuifunga 1-0 Abaluhya na kumaliza kwa sare ya bila kufungana na Simba FC ya Uganda.
Kikosi cha Simba wakati huo, kilikuwa kinaundwa na wakali kama Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Shaaban Baraza, Mohamed Kajole ‘Machela’ (sasa marehemu), Aloo Mwitu/Mohamed Bakari ‘Tall’, Omar Choggo (sasa marehemu), Athumani Juma Kalomba (sasa marehemu), Khalid Abeid, Martine Kikwa, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid ‘Muchacho’, Adam Sabu (sasa marehemu), Abdallah Kibadeni, Saad Ally na Abbas Dilunga.
Ni wakali hawa hawa ambao pia waliifikisha Simba SC Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika, mwaka 1974 na kutolewa na Mehallal El Kubra ya Misri, wakitoka kuitoa timu ngumu na tishio barani enzi hizo, Hearts Of Oak ya Ghana.

MWAKA 1991
Simba ilishindwa kutetea taji hilo mwaka 1975 baada ya kufungwa na wapinzani wao wa jadi, Yanga katika fainali visiwani Zanzibar na wakalazimika kusubiri hadi mwaka 1991 ili kupata taji la pili la michuano hiyo katika fainali nyingine zilizofanyika Dar es Salaam.
Walibebaje taji? Simba ilianzia Kundi A mjini Dar es Salaam ambako waliongoza na kufanikiwa kuingia Nusu Fainali, ambako walikutana na Gor Mahia ya Kenya na kushinda 1-0, hivyo kutinga fainali.
Katika fainali, Wekundu wa Msimbazi walikutana na SC Villa ya Uganda, iliyokuwa tishio ikiongozwa na mshambuliaji bora zaidi kuwahi kutokea Uganda, Majjid Musisi Mukiibi na kushinda mabao 3-0, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ na Kocha Mchezaji Hassan Afif waking’ara mno na kuwa chachu ya ushindi.
Siku hiyo, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ alikuwa ana kazi moja tu- kumdhibiti Musisi (sasa marehemu), asilete madhara na akafanikiwa. Ilikuwa hadi Musisi anakunywa maji, Julio anamsubiri arudi uwanjani aanze kutembea naye tena.
Kikosi cha Simba kilichotwaa taji hilo, kilikuwa kinaundwa na wakali kama Iddi Pazi ‘Father’, Mavumbi Omar, Raphael Paul (sasa marehemu), Twaha Hamidu ‘Noriega’, Jamhuri Kihwelo, Method Mogella (sasa marehemu), Iddi Suleiman ‘Meya, Issa Kihange, Bakari Iddi, Ayoub Mzee/Hassan Afif, Zamoyoni Mogella, Itutu Kiggi ‘Road Master’/Khalfan Ngassa, Hamisi Thobias Gaga ‘Gaga Rhino’, Frank Kasanga ‘Bwalya’ na Gebo Peter.

MWAKA 1992:
Simba ilifanikiwa kutetea taji hilo katika fainali zilizofuata visiwani Zanzibar, ikiwa imeboresha zaidi kikosi chake kwa kuingiza nyota wapya kama kipa Mwameja Mohamed, beki George Masatu na kiungo Hussein Aman Marsha.
Simba iliyokuwa katika Kundi B, katika mechi ya kwanza iliifunga 1-0 Bata Bullets FC ya Malawi, mechi ya pili iliifunga 2-0 Jamhuri SC ya Pemba kabla ya kumalizia kwa sare ya bila kufungana na El Hilal ya Sudan, hivyo kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba ilikutana na Small Simba SC ya Zanzibar na kushinda 1-0, hivyo kutinga Fainali, ambako ilikwenda kukutana na watani wao wa jadi, Yanga SC na kushinda kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Amaan.

MWAKA 1995:
Simba ilishindwa kutetea taji mjini Kampala, Uganda ingawa bahati nzuri Kombe lilipakizwa kwenye ndege kurudishwa Dar es Salaam na watani wao, Yanga. Kutoka hapo, Wekundu wa Msimbazi walilazimika kusubiri hadi mwaka 1995 kutwaa taji lingine la michuano hiyo.
Ilikuwa ni katika michuano mingine iliyofanyika Dar es Salaam na Simba tena walipangwa Kundi A na katika mechi ya kwanza walitoka sare ya 1-1 na Express FC ‘Red Eagles ’ ya Uganda, mechi ya pili waliichapa 3-1 Morris Supplies ya Somalia kabla ya kuitandika 4-1 Adulis ya Ethiopia na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba ikiwa inaundwa na idadi kubwa ya nyota wake walioifikisha timu Fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, iliifunga 1-0 El Mourada ya Sudan na kuingia Fainali.
Katika Fainali, Simba ilikutana na Express ‘Red Eagles’ na kushinda kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, siku hiyo George Magere Masatu akijifunga na kuwasawazishia bao Tai Wekundu dakika ya 53, yaani dakika mbili tu tangu Hussein Amaan Marsha aifungie Sijmba bao la kuongoza dakika ya 51.

MWAKA 1996:
Simba ilifanikiwa kwa mara ya pili na ya mwisho kihistoria kutetea taji hilo, mwaka 1996 katika fainali zilizofanyika Tanzania tena, kwenye miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Simba ilipangwa tena katika Kundi A mjini Dar es Salaam na katika mechi ya kwanza, iliifunga 2-0 Small Simba ya Zanzibar, kabla ya kulala 1-0 mbele ya APR FC ya Rwanda na kumaliza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Kwa matokeo hayo, Simba ilishika nafasi ya pili katika kundi hilo kwa pointi zake sita, ikizidiwa pointi moja tu APR iliyoongoza kundi hilo, hivyo kutinga Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Gor Mahia, bao pekee la Bitta John hivyo kutinga fainali, ambako ilikutana na APR na kulipa kisasi kwa ushindi wa 1-0, bao pekee la George Magere Masatu dakika ya 115.

MWAKA 2002:
Mwaka 1997 michuano hiyo haikufanyika na mwaka 1998, Simba ilishindwa kutetea taji, baada ya kuchukuliwa na Rayon Sport ya Rwanda visiwani Zanzibar. Mwaka 1999, taji lilichukuliwa na Yanga mjini Kampala, Uganda na 2000 na 2001 Simba hawakupata tiketi ya kucheza michuano hiyo, hadi 2002 katika fainali zilizofanyika visiwani Zanzibar.
Naam, Simba waliandika historia ya kuwa timu inayoongoza kutwaa taji hilo, ilikuwaje?
Simba ilipangwa Kundi B na katika mchezo wa kwanza, ililazimishwa sare ya bila kufungana na vibonde Elman ya Somalia, kabla ya kuzinduka kwenye mechi ya pili na kuifunga Prince Louis ya Burundi, mabao 2-1, wafungaji wake Emmanuel Gabriel dakika ya 27 na Yussuf Macho dakika ya 78, na baadaye kuirarua Forodha ya Zanzibar mabao 3-1, wafungaji Joseph Kaniki ‘Golota’ dakika ya 22, Steven Mapunda ‘Garrincha’ dakika ya 65 na Macho ‘Musso’ dakika ya 90 na mechi ya mwisho, bao la kujifunga la Kevin Malumbe dakika ya 88 liliwapa Wekundu wa Msimbazi ushindi wa 1-0 dhidi ya Tusker ya Kenya.
Kwa matokeo hayo, Simba iliongoza Kundi hilo kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Prince Louis iliyovuna pointi saba, Tusker pointi tano sawa na Elman, wakati Forodha ilitoka patupu kabisa.
Katika Nusu Fainali, Simba ilikutana na mabingwa wa Zanzibar enzi hizo, Mlandege na kushinda 2-0, mabao ya Yussuf Macho ‘Musso’ dakika ya 37, na Shekhan Rashid Abdallah kwa penalti dakika ya 90.
Katika fainali, Simba ilikutana tena na Prince Louis na bao pekee la Nteze John Lungu dakika ya sita, lilitosha kuwafanya Simba waitwe mabingwa wa Kombe la Kagame mara nyingi zaidi hadi sasa.
Kikosi cha Simba siku hiyo kilikuwa; Mohamed Mwameja, Said Sued, Ramadhan Wasso/Majuto Komu dk 35, Amri Said, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Stephen Mapunda ‘Garrincha’/Joseph Kaniki dk 74, Shekhan Rashid, Yussuf Macho, Nteze John/Emmanuel Gabriel dk 6 na Mark Sirengo.
Naam, hivyo ndivyo namna ambavyo Simba SC walivyobeba ndoo sita za Kombe la Kagame na katika fainali za mwaka huu, wanaingia kusaka ndoo ya saba ili kudhihirisha umwamba wao katika soka ya Afrika Mashariki na Kati, nani atawazuia, Yanga tena? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.

MAXINSURE WAISAIDIA TWIGA STARS VIFAA VYA M NA UPUUZI


Na Prince Akbar
KAMPUNI ya bima ya Maxinsure imetoa vifaa vya mazoezi kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) vyenye thamani ya sh. milioni 1.3.
Vifaa hivyo ambavyo ni jezi, bukta na soksi 20, vizibao (bibs) 20 na mipira miwili vimekabidhiwa leo (Julai 12 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Amisa Juma.
Akikabidhi vifaa hivyo, Amisa amesema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii lakini vilevile wameamua kuiunga mkono timu hiyo ambayo wanajua haina mdhamini kutokana na vipaji na uwezo ambao umekuwa ukioneshwa na wachezaji wake.
Pia amezitaka kampuni, taasisi, watu binafsi na Serikali kuiunga mkono timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali inayotarajia kushiriki.

TEMEKE NA MWANZA NUSU FAINALI COPA COCA COLA KESHO


Na Princess Asia
TEMEKE na Mwanza zinapambana kesho (Julai 13 mwaka huu) katika nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 itakayochezwa saa 2.30 asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya pili itaanza saa 9.30 mchana kwenye uwanja huo huo ikizikutanisha timu za Morogoro na Tanga.
Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya michuano hiyo zitachezwa Jumapili (Julai 15 mwaka huu). Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 5 asubuhi na kufuatiwa na fainali ambayo itafanyika kuanzia saa 9 kamili alasiri.
Mwanza ilipata tiketi ya nusu fainali kwa kuifunga Kinondoni 3-1 huku Temeke ikitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Mjini Magharibi. Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mara ndiyo ulioipa Morogoro tiketi ya nusu fainali wakati Tanga yenyewe iliilaza Dodoma bao 1-0.

CECAFA YATAJA VIINGILIO KAGAME


Mashabiki wa Yanga

Na Princess Asia
KIINGILIO cha chini katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) vitakuwa sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na sh. 2,000 kwa mechi ambazo hazihusishi timu hizo. Yanga ni bingwa mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa mtetezi.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mechi zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa ni viti vya bluu na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, viti vya VIP C sh. 10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti vya VIP A ni sh. 20,000.
Wambura amesema kwamba, siku ambazo Simba na Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh. 10,000 kwa viti vya VIP B na sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki akikata tiketi moja anaona mechi zote mbili; mechi ya saa 8 na ile ya saa 10.
Amesema timu za El Salam Wau ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar es Salaam jana usiku (Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo wakati nyingine zote zilizobaki kutoka nje zinawasili leo katika muda tofauti.
CECAFA leo imetangaza marekebisho madogo ya ratiba ya michuano hiyo na mechi ya Simba na URA ya Uganda iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa itafanyika Jumapili (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
CECAFA imefanya mabadiliko hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Kutokana na mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10 kamili jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa Chamazi.
Pia siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi nyingine itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu za Azam ya Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mechi za ufunguzi wa mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi ya kwanza saa 8 mchana itakuwa kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni Yanga itaoneshana kazi na Atletico ya Burundi.
 

SIMBA NA URA SASA JUMAPILI TAIFA KAGAME


Musonye kulia, kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah


Na Prince Akbar
BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limerekebisha ratiba ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na sasa mabingwa wa Tanzania, Simba SC watacheza na URA Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, badala ya Jumatatu.
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mechi ya Simba imerudishwa Jumapili, baada ya fainali ya Copa Coca Cola kuhamishiwa Uwanja wa Karume siku hiyo, tofauti na awali ilipangwa kufanyika Uwanja wa Taifa hivyo kusababisha mechi ya Simba na URA isogezwe mbele.
Kwa mabadiliko hayo, sasa Jumapili kutakuwa kuna mechi tatu za Kagame, mechi ya Simba na URA Uwanja wa Taifa itatanguliwa na mechi kati ya Vita Club ya DRC na Ports ya Djibouti, wakati Chamazi Azam itamenyana na Mafunzo ya Zanzibar.

RATIBA KOMBE LA KAGAME:
Julai 14, 2002
1 APR vs WAU SALAAM Uwanja wa Taifa (Saa 8 mchana)
2 YANGA vs ATLETICO Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)

Julai 15, 2002
3 AZAM vs MAFUNZO Chamazi (saa 8 mchana)
4 VITA CLUB vs PORTS Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)
5 SIMBA vs URA Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)

Julai 17, 2012
6 ATLETICO vs APR Uwanja wa Taifa (saa 8 mchana)
7 WAU SALAAM vs YANGA Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)
Julai 18, 2012
8 VITA CLUB vs URA Uwanja wa Taifa (saa 8 mchana)
9 PORTS vs SIMBA Uwanja wa Taifa (saa 10jioni)
Julai 19, 2012
10 ATLETICO vs WAU SALAAM Uwanja wa Taifa (saa 8 mchana)
11 MAFUNZO vs TUSKER Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)

Julai 20, 2002
12 PORTS vs URA Uwanja wa Taifa (saa 8 mchana)
13 YANGA vs APR Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)

Julai 21, 2012
14 AZAM vs TUSKER Uwanja wa Taifa (saa 8 mchana)
15 SIMBA vs VITA CLUB Uwanja wa Taifa (saa 10 jioni)

Julai 22m, 2012 (MAPUMZIKO)

ROBO FAINALI
Julai 23, 2012
16 B2 vs C2
17 A1 vs C3

Julai 24, July
18 C1 vs A2
19 B1 vs A3

Julai 25, 2012 (MAPUMZIKO)

NUSU FAINALI
Julai 26, July
20 Winner 16 vs Winner 17
Julai 26, 2012
21 Winner 18 vs Winner 19

Julai 27, 2012 (MAPUMZIKO)

FAINALI NA MSHINDI WA TATU
Julai 28, 2012
22 Loser 20 vs Loser 21
23 Winner 20 vs Winner 21
 

MTAKATIFU TOM AWATEMA DAMAYO, MSUVA, NSAJIGWA KIKOSI CHA KAGAME, YONDAN NDANI


Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet katikati akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, Jangwani mchana wa leo, kutaja kikosi cha Kombe la Kagame. Kulia ni Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa na kushoto Mwakilishi wa Kilimanjaro Beer, wadhamini wakuu wa klabu hiyo, Oscar Shelukindo

Na Prince Akbar
KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amewaacha kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kuanzia Jumamosi wachezaji watatu nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo kwa sababu watakuwa na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana huu, makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Saintfiet alisema kwamba wachezaji hao watakuwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29 dhidi ya Nigeria.
Mtakatifu Tom anasoma majina
“Kwa mujibu wa kanuni natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi wanacheza na Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo watakuwa kwenye maandalizi ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao hata kwenye Nusu Fainali, kwa sababu hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia Nahodha wa klabu hiyo, Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji 20, lakini amesema mchezaji huyo ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi Kuu.
Amewataja wachezaji aliowateua baada ya kushauriana na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani kuwa ni; makipa Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa Assenga, Hamisi Kiiza na washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Yanga, ambao ndio mabingwa watetezi wa Kagame, watafungua dimba na mabingwa wa Burundi, Atletico FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

KIKOSI CHA YANGA KAGAME;
Makipa; Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji; Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.
Mtakatifu Tom akizungumza na Waandishi hapo

 

AZAM ACADEMY WACHEZA MBELE YA RAIS BURUNDI LEO

TIMU ya soka ya vijana ya Azam FC, maarufu kama Azam Academy leo inacheza mechi ya kukamilisha ratiba kwenye michuano ya Rollingston inayoendelea nchini Burundi, katika mechi ambayo mgeni rasmi atakuwa rais wa Burundi, Perre Nkurunziza.
Azam tayari imekwishafuzu Robo Fainali, baada ya kushinda mechi zake mbili za awali 1-0 dhidi ya Kyazanga FC ya Uganda na 3-0 dhidi ya Nyirakongo Academy ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika mchezo huo, kikosi cha Azam kinatarajiwa kuwa; Aishi, Mgaya, Shabalala, Dizana, Mkomola, Reyna, Mudathiri, Kaijage, Machuppa, Kelvin na Kimwaga.
Simba na Yanga zilialikwa pia kwenye michuano hiyo, ila zote zimejitoa dakika za mwishoni

No comments: