Tuesday, May 3, 2016

MTPC yakumbushia ujenzi wa kituo cha Polisi Mtwara.

Waandishi wa habari wa Mtwara wakifanya usafi katika eneo litakalojengwa kituo cha Polisi, Msijute, Mtwara


Waandishi na usafi





Baada ya kazi, waandishi wakisubiri Chakula


Waandishi wakisubiri chakula kwa pozi tofauti





Hatimaye muda wa chakula ukawadia..hapo mwenyekiti wa MTPC, Hassan Simba akijipatia chakula 


Hassan Simba kazini



Na Juma Mohamed, Mtwara.

KATIKA kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (Media Day), Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) kimeungana na baadhi ya wadau wake kufanya usafi katika eneo linalotarajiwa kujengwa kituo cha polisi lililopo kijiji cha Msijute jirani na kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Ltd.
MTPC iliungana na viongozi wa kiwanda hicho, jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa vijiji vyote vinavyozunguka kiwanda cha Dangote katika kutekeleza shughuli hiyo ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuzikumbusha mamlaka husika umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa kituo hicho ambacho jiwe la msingi liliwekwa toka mwaka 2014.

Waandishi wa Mtwara kazini-Media Day


Akizungumza katika eneo hilo, mwenyekiti wa MTPC Hassan Simba, alisema uamuzi wa shughuli hiyo kufanyika katika eneo hilo ni kwa ajili ya kulikumbusha jeshi la Polisi na uongozi wa Dangote ambao ndio ulitoa ahadi ya kujenga kituo hicho kwamba kuna umuhimu wa kuharakisha ujenzi huo ambao kukamilika kwake kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa kiwanda pamoja na jamii ya vijiji jirani.
“Kuna umuhimu sasa wa kuharakishwa ujenzi wa hiki kituo hapa, kwasababu sisi tumekuwa tunazunguka huko mitaani na tunaona wenzetu wa jeshi la polisi wanavyohangaika kukimbia na vijana wachache ambao sio waaminifu huko mapolini wanaoiba vitu..kwahiyo tunaamini kituo kikiwa hapa kwao wao itakuwa kazi nyepesi na wataweza kufanya kazi zao vizuri..” alisema.
Katibu wa chama hicho, Bryson Mshana, akizungumzia uhuru kwa wanahabari wa Mtwara, alisema waandishi kwa kiasi kikubwa wamejenga mahusiano mazuri na jamii pamoja na taasisi mbalimbali zikiwemo za kiusalama ambapo ukiachiliambali baadhi ya waandishi waliopata misukosuko wakati wa vurugu za gesi mwaka 2013, hakujawahi kutokea kadhia yoyote kwa waandishi na wadau wao.

Katibu wa MTPC Bryson Mshana akielezea jambo


“Waandishi wana uhusiano nzuri na jeshi la polisi na ndio maana tumewashirikisha katika tukio hili lakini pia Mtwara waandishi hawana tatizo na wawekezaji, wawekezaji wamekuwa wakitoa ushirikiano na nafikiri kuna taratibu za kufika katika eneo la uwekezaji kwahiyo wamekuwa wakituruhusu na jeshi la polisi pia..sio kwamba hatupati misukosuko na jeshi la polisi lakini wamekuwa waki ‘react’ haraka inapotokea pale mwandishi amepatwa na tukio..” alisema.
Mwakilishi Mkazi wa Dangote Industries Ltd, Esther Baruti, aliwaondoa hofu wakazi wa vijiji hivyo na Mtwara kwa ujumla kwa kuwaambia kuwa tayari ramani kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho imekabidhiwa kwa jeshi la polisi ambao wanasubiri kibali kutoka makao makuu ili ujenzi uanze.

Mwakilishi Mkazi wa Dangote Industries Ltd, Esther Baruti, akiongea jambo


“Kwahiyo naomba majirani zetu na watu wote turudishe ushirikiano uliokuwepo, tusikubali watu wanaoingia katikati kuvuruga amani ya huku na kitu kingine mkumbuke Alhaj Dangote alitoa ahadi mbalimbali hizo ahadi atazitekeleza baada ya uzalishaji kukamilika rasmi, kwasababu sasa hivi bado kiwanda hakijakamilika kipo kwenye majaribio na bado ujenzi wa ‘power plant’ unaendelea..” alisema.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, George Salala, akieleza jambo


Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, George Salala, akizungumza kwa niaba ya kamanda wa mkoa ACP-Henry Mwaibambe, aliwaashukuru wanahabari kwa kutambua umuhimu wa kuwapo kwa maendeleo na usalama kwani mambo hayo hayapaswi kwenda tofauti, huku akiwasifu kwa namna wanavyokuwa wepesi katika kutekeleza majukumu yao na kushiriki shughuli za kijamii pale inapobidi.

Kaimu kamanda wa polisi George Salala akijipatia chakula




No comments: