Thursday, October 22, 2015

Waandishi Mtwara wahakikishiwa usalama katika Uchaguzi.


Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akizungumza na wadau wa habari, katika mkutano wa wadau ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), kwa ajili ya kujadiliana kwa pamoja masuala mbalimbali yanayoihusu tasnia hiyo kwa lengo la kuiboresha. Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Parishi, mkoani hapa


Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego



Picha ya pamoja kati ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, aliyekaa katikati, na wadau wa habari wa mkoa wa Mtwara.

Na Juma Mohamed.

WAANDISHI wa habari mkoani hapa wametakiwa kufanya kazi zao kwa kujiamini na kwa kufuata maadili yao, wakati wa kuandika habari katika kipindi cha uchaguzi.
Akizungumza jana katika ufunguzi wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Chama cha Waaandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alisema mkoa unatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari, hivyo umejipanga kuhakikisha usalama unakuwa wakutosha kwao.
Alisema, toka amewasili mkoani hapa miezi kadhaa iliyopita, amekuwa akishirikiana vema na wanahabari, jambo ambalo linamfanya aamini kuwa ni wadau muhimu kwake na kwa mkoa kwa ujumla.
Aidha, alitumia fursa ya kuzungumza katika mkutano huo kuwataka wananchi zaidi ya 700,000 wa mkoa wa Mtwara waliojiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura, kwenda kupiga kura siku ya Jumapili ya Oktoba 25, kwani wajibu wao.
“Tumepita katika kipindi cha kampeni, na sasa tunaelekea katika uchaguzi..nawaomba wajitokeze wale wote waliojiandikisha waende wakatendee haki nafsi zao, wakachague viongozi ambao wanaamini watawavusha katika kipindi cha miaka mitano..” alisema.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego


Aliwaondoa hofu wananchi juu ya wasi wasi uliopo kuhusu uvunjifu wa amani, na kusema kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vyema kuhakikisha amani inatawala katika kipindi cha uchaguzi mpaka wakati wa kutangaza matokeo kama ilivyokuwa katika wakati wa kampeni ambazo zinaelekea mwisho.
Kwa upande wake, Shekh mkuu wa mkoa wa Mtwara, Shekh Nurdin Abdallah Mangochi, akizungumza kama mdau wa habari, alisema anaimani na waandishi wa habari katika kutenda haki na kuhakikisha amani inaendelea kutawala ndani ya mkoa.
Alisema, waislamu kawaida yao ni kuswali swala tano kila siku na kwamba anaimani kama ilivyo kwake, na wengine hufanya ibada kwa kumuomba mungu juu ya kutawala amani katika uchaguzi ili zoezi hilo liweze kupita kwa amani.

Wadau wa habari wakiwa katika mkutano wa wadau, ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), kwa ajili ya kujadiliana kwa pamoja masuala mbalimbali yanayoihusu tasnia hiyo kwa lengo la kuiboresha. Mkutano ulifanyika katika ukumbi wa Parishi, mkoani hapa.


Naye, mwenyekiti wa Chama cha Wazee na Wastaafu (CHAWAMU) mkoa wa Mtwara, Robert Maganga, alisema, uchaguzi wa mwaka huu umekuwa na msisimko mkubwa kwa wananchi hasa vijana, lakini wanaimani kubwa juu ya mchango wa vyombo vya habari katika kuandika habari zenye kuleta masilahi kwa taifa ambazo haziwezi kuwa na upendeleo wa upande wowote.
Alisema, wazee wanakuwa katika wakati mgumu ikitokea kuna hari ya uvunjifu wa amani ktokana na wengi wao kukosa nguvu kama ilivyo kwa vijana, jambo ambalo linapelekea kudhulika kirahisi kwa kushindwa kujiokoa.
Mwandishi wa habari mwandamizi na mwanachama wa MTPC, Philipo Lulale, aliwaasa wanahabari kutoonyesha upenzi wao wa kisiasa katika chama chochote ili kuhepusha kutofautiana na wananchi.

Alisema, uchaguzi wa mwaka huu ni mgumu kutokana na ushindani uliopo hasa kwa wagombea wawili wa nafasi ya Urais, ambao ni Mhe. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mhe. Edward Lowassa, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiungwa mkono na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

No comments: