Wednesday, October 21, 2015

Watatu Azam kuikosa Ndanda kesho-VPL Nangwanda, Mtwara..Timu za tambiana ushindi



Wachezaji wa timu ya soka ya Azam Fc ya jijini Dar es Salaa, na makocha wao wakiwa katika mazoezi ya mwisho leo jioni katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, tayari kwa kuwakabili wenyeji wao Ndanda Sc kesho katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara.







Basi la Azam Fc, likitoka ndani ya uwanja wa Nangwanda Sijaona baada ya kumaliza mazoezi ya jioni



Na Juma Mohamed
Timu za soka za Ndanda Sc na Azam Fc, kila moja imetamba kuibuka na ushindi katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara unaotarajiwa kuchezwa kesho, katika dimba la Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.

Msemaji wa Azam Fc, Jaffer Idd, akizungumza na NEWS ROOM juu ya maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya mchezo wa kesho dhidi ya Ndanda Sc.

Akizungumza leo na NEWS ROOM, msemaji wa Azam Fc ya jijini Dar es Salaam, Jaffer Idd Maganga, amesema wanafahamu ugumu wa mchezo huo kutokana na timu zote kuhitaji alama tatu ambazo walizikosa katika michezo yao iliyopita, lakini kikosi chao kipo imara kwa ajili ya kuondoka na ushindi.

Alisema, licha ya upana wa kikosi chao kilichosheheni wachezaji mchanganyiko wa ndani na nje ya nchi, bado wanawaheshimu Ndanda kutokana na upinzani wanaoupata pindi wanapokuta.
Aidha, aliwataja wachezaji watatu ambao watakosekana katika mchezo huo muhimu ambao wanahitaji alama tatu kuweza kuendelea kuwakaba koo Yanga walio kileleni, kuwa ni Abuubakar Salum 'Sure Boy' mwenye kadi tatu za njano, Marick Farid na Mudathir Yahaya ambao ni majeruhi.

Kwa upande wake, kocha wa Ndanda Sc, Amimu Mawazo, amesema pamoja na mapungufu yaliyopo katika kikosi chao hasa katika eneo la kiungo, lakini amewaandaa vizuri vijana wake na kuahidi kuendeleza ubabe wao mbele ya wanalambalamba hao katika uwanja wa nyumbani.

Aidha, mashabiki wa Ndanda wamesema bado wanaimani na timu yao kuwa itaibuka na ushindi hapo kesho, licha ya kutopata matokeo mazuri katika michezo yao iliyopita hasa ya ugenini.

No comments: