Wednesday, October 21, 2015

Kuelekea uchaguzi- Wananchi Mtwara waanza kukimbia mji kuhofia usalama wao.


Mmoja wa wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Shabia Liwowa, akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya hofu iliyoanza kutanda kwa baadhi ya wananchi wa manispaa hiyo kuelekea uchaguzi mkuu kiasi cha kupelekea wengine kukimbia mji.




Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya kudumisha hali ya amani na utulivu kuelekea katika uchaguzi mkuu.


Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego.



Na Juma Mohamed.

KUFUATIA kutoelewana kati yaTume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na baadhi ya vyama vya siasa juu ya suala la kusimama umbali wa mita 200 kutoka eneo la kupigia kura, baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani wameanza kushikwa na hofu juu ya usalama wao kiasi cha kulazimika kukimbia mji.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliopo katika kituo kikuu cha mabasi mkoani hapa, wamesema kuanzia juzi asubuhi kumekuwa na idadi kubwa ya wasafiri wanaotoka mjini Mtwara kuelekea sehemu mbalimbali hasa wilayani, kuliko wanaingia mjini.
Wakizungumza na Nipashe jana kwa nyakati tofauti, wananchi hao wakiwamo madereva wa mabasi ya wilayani walisema, kati ya wasafiri idadi kubwa imeonekana ni kina mama.

Mwananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani, Ally Njaru, akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya hofu iliyoanza kutanda kwa baadhi ya wananchi wa manispaa hiyo kuelekea uchaguzi mkuu kiasi cha kupelekea wengine kukimbia mji.

“Hata hizi gari za Newala leo nimeona zimeondoka na abiria ni wengi mno kupita maelezo, kwahiyo kwangu mimi naweza nikasema sijui wanachoenda kufanya huko waendako lakini naweza nikasema hili sio swala la kawaida kwasababu sio siku zote inakua hivi ni siku hizi mbuli tatu tu kuelekea uchaguzi..na wengi wanaoondoka ni kina mama pamoja na watoto wadogo..” alisema Ali Njaru, ambaye ni dereva wa mabasi yanayotoka Mtwara kwenda Kirambo, mpakani mwa Msumbiji na Tanzania.
Naye, Shabia Liwowa, alikiri kushuhudia magari ya askari polisi na ya Jeshi yakipita katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mtwara huku mengine yakipiga ving’ola, jambo ambalo limepelekea kuwatisha wananchi na kusababisha baadhi yao kuamua kuondoka mjini.

Mabasi yanayokwenda wilaya mbalimbali za mkoa wa Mtwara.

“Kura hii ipite kwa amani na kwa utulivu, ili aliyekua na motto amtunze motto wake na aliyekua na nyumba atunze nyumba zake..tunachoomba sisi hao askari wanopita wapiti tu kwa amani..kama wanapita wanazunguka basi watuambie kama wanapita tu kwa amani..” alisema.
Alisema, katika nyumba yake anayoishi, wapo baadhi ya watu walioondoka kuelekea vijijini kutokana na woga wa kuhofia kuzuka kwa vurugu siku ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na mama mmoja ambaye hakumtaja jina aliyeambatana na watoto wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara (RPC) Henry Mwaibambe, alipotafutwa kwa simu ili aweze kuzungumzia hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego.

Awali akizungumza katika kiako na waandishi wa habari juu ya kuwahamasisha wananchi kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliwataka wananchi kuondoa hofu juu ya kutokea kwa vurugu, na kukiri kuwa na taarifa za baadhi yao wanahama mji, ambapo alisema mkoa kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama wamejipanga vyema kuhakikisha usalama unakuwepo kwa wananchi wake.
Aidha, alisema wamebaini kuwepo kwa makundi mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya kufanya vurugu na kuzuia watu kwenda kupiga kura, katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara.
“Mfano maeneo ya Mkanaledi, Mikindani-Mtwara, Tandahimba na Ndanda..aidha, zipo taarifa za makundi hayo kujiandaa na silaha za jadi kushambulia vyombo vya dola, na uchomaji moto majengo ya serikali, nawatahadharisha wale wote wenye nia hiyo waache mara moja kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamevunja sheria na mkono wa dola hautawaacha.” Alisema.

Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego.

Alisema, serikaliya mkoa na wilaya zote wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinatawala kwa kipindi chote cha upigaji kura hadi utoaji wa matokeo.
Aliwasisitiza kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kupiga kura kwasababu ni haki na wajibu wa kila mtu kumchagua kiongozi anayemtaka.
“Nategemea wale wote waliojiandikisaha watafuata taratibu zote zilizowekwa na tume kwenda kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kwenda kupiga kura kwa utulivu mkubwa.” Aliongeza.
Aliahidi kuhimarisha ulinzi kwa waaandishi wa habari ambao watakuwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa katika kutekeleza majukumu yao katika kipindi cha uchaguzi, ambapo unaandaliwa utaratibu wa kuwapatia vitambulisho na mafulana yatakayowatambulisha kuwa ni waandishi.

No comments: