Tuesday, May 29, 2012

THOMAS ULIMWENGU KUTOENDA KUWAA AKINA KOLO TOURE

Zikiwa yamebaki masaa kadhaa kabla ya timu ya Taifa ya Tanzania kusafiri kwenda kuwavaa Ivory Coast - taarifa rasmi kutoka kambi ya timu hiyo zinasema kwamba mshambuliaji Tom Ulimwengu hatosafiri na timu hiyo.

Ulimwengu, mshambuliaji chipukizi wa timu ya soka ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ameshindwa kupona maumivu ya kifundo cha mguu aliyopata akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Mbali na Ulimwengu Taifa Stars pia itakuwa bila ya kiungo wa kutumainiwa wa Yanga Nurdin Bakari ambaye pia ameshindwa kupona maumivu ya nyama za paja yaliyokuwa yanamkabili. Ulimwengu na Nurdin wote walikosa mchezo wa kirafiki ulioisha kwa sare ya bila kufungana dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi uliochezwa Uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita.


Ofisa wa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) alisema jana kuwa amepata taarifa kutoka kwa daktari wa timu ya taifa Mwanandi Mwankemwa kuwa wachezaji hao hawatasafiri na kikosi cha timu hiyo kinachotarajiwa kuondoka keshokutwa alfajiri kwa ndege ya Shirika la Kenya kuelekea Ivory Coast. Hata hivyo kocha wa Stars Kim Poulsen amesema hatoita wachezaji wengine badala yake waliopo watajaza nafasi za nyota hao.


Katika mchezo uliopita wa kirafiki dhidi ya Malawi Kim alimchezesha nyota wa TP Mazembe Mbwana Samatta na kiungo mchezeshaji wa Simba Haruna Moshi ‘Boban’ kwenye nafasi ya ushambuliaji, huku Shaabani Nditi wa Mtibwa Sugar, Mwinyi Kazimoto wa Simba na Franka Domayo wakicheza kwenye nafasi ya kiungo.


Katika mechi hiyo kocha Kim alifanya badiliko moja kwa kumpumzisha beki wa kushoto wa Azam Waziri Salim na nafasi yake kuchukuliwa na Amiri Maftaha aliyeonekana kidogo kuubadili mchezo huo.


Hata hivyo Kim baada ya mechi hiyo alikiri kuwa anaweza kukifanyia mabadiliko kikosi cha timu hiyo kilichocheza dhidi ya Malawi lakini alisema hilo litategemea na namna atakavyoona wachezaji wake wanavyocheza mazoezini katika siku hizi zilizosalia kuelekea mchezo huo.



IVORY COAST WAMTIMUA KOCHA ZIKIWA ZIMEBAKI SIKU CHACHE KABLA YA KUWAVAA STARS

ZIKIWA zimesalia siku nne kabla ya kumenyana na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Kocha wa Ivory Coast Francois Zahoui ametimuliwa kazi. Stars inatarajiwa kusafiri keshokutwa kuelekea Abidjani kwa ajili ya kumenyana na Ivory Coast katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe Dunia itakayochezwa Juni 2.

Habari kutoka Ivory Coast zilisema jana Shirikisho la Soka la nchi hiyo (FIF) limemfuta kazi kocha huyo saa 24 baada ya timu yake kunyukwa mabao 2-1 na Mali katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Ufaransa.


Mchezaji wa zamani wa Ufaransa Sabri Lamouchi ndio ametangazwa kuwa kocha mpya wa Tembo hao ambaye ataiongoza timu hiyo katika mechi za kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 pamoja na ile ya Kombe la Mataifa Afrika 2013.


Uteuzi wa kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 ambaye amewahi kuwa kiungo wa Auxerre, Monaco, Inter na Marseille umeshtua wengi kwasababu hakuwa kwenye orodha ya waliokuwa wakitarajiwa kuchukua nafasi hiyo kama ilivyokuwa kwa kocha wa zamani wa Senegal Bruno Metsu, Eli Baup, Antoine Kombouaré na kocha wa zamani wa England Sven Goran Eriksson.


Lamouchi alistaafu kucheza soka ya kimataifa mwaka 2001 baada ya kucheza mechi 12 tu dhidi ya Les Bleues na kufunga bao moja, hajawahi kuifundisha timu yoyote ya taifa.

No comments: