Monday, April 16, 2012

Monday, April 16, 2012

LAMPARD: TUTAKOMAA NAO NA MESSI WAO

Lampard
KIUNGO wa Chelsea, Frank Lampard amesema kwamba kuifunga Barcelona katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Jumatano itakuwa changamoto kubwa zaidi katika maisha yake soka.
Lampard amekutana na Barca mara kadhaa na pia amecheza dhidi ya timu nyingine nyingi kubwa Ulaya katika maisha yake ya soka, lakini anaamini timu hiyo ya Hispania kwa sasa inatisha na atakuwana na timu bora zaidi tangu aanze soka.
Wachambuzi wengi wanaipa nafasi timu ya Pep Guardiola kuingia fainali itakayochezwa mjini Munich na pia Lampard anazimikia vipaji vya wachezaji wa wapinzani hao kama Lionel Messi, Xavi na Andres Iniesta.
Chelsea inajiandaa kwa mechi ya kesho Uwanja wa Stamford Bridge ikitoka kushinda 5-1 dhidi ya Tottenham katika Nusu Fainali ya Kombe la FA Uwanja wa Wembley, lakini Lampard amesema hakuna kulala hata kidogo katika usiku watakaoivaa timu bora, Barca.
"Nafahamu watu wanasema sisi ni ‘wahanga’ kwa sababu kila mmoja anahisi Barcelona anaweza kupita kwa kila mmoja. Ni sawa, kuwa na mchezaji kama (Lionel) Messi, wanaweza kufanya hivyo," alisema Lampard.
"Barcelona hawawezi kutudharau sisi, lakini kuwafunga Tottenham si onyo kwao. Wametengeneza timu waliyonayo.
"Wazi ni changamoto kubwa ambayo sijawahi kukutana nayo,”alisema.
Ikiwa na Muargentina, Messi anayeogelea kwenye moja ya misimu ya mafanikio makubwa katika historia ya soka, ni wazi ndiye anayetia ganzi matumaini ya Chelsea kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili.
Na Lampard amesema Messi amempiku hata Muargentina mwenzake Diego Maradona kama mchezaji bora daima kuwahi kutokea.
"Amekuwa bora zaidi tangu tumecheza nao mwaka 2009 na alikuwa mchezaji mzuri wakati huo.
Kiwango alichofikia kisoka ni kitu ambacho sijawahi kuona kabla," alisema Lampard.
"Nimekuwa wakati wa Maradona. Alikuwa kioo change na nafikiri Messi amevuka kiwango chake.
"Kukaribia mabao 70 ni wazimu. Anastahili. Ni mchezaji bora duniani."
Lakini licha ya kuwatukuza nyota wa Barca na staili yao ya kucheza, Lampard amesema hivi karibuni Chelsea imezinduka chini ya kocha Roberto Di Matteo na kuonyesha kwamba wanaweza kuwatia misukosuko mabingwa hao wa Hispania.
"kama tutacheza kama tulivyocheza leo (dhidi ya Spurs) kwa kujituma na nguvu tuliyonayo kwenye timu, tunatakiuwa kuamini tuna nafasi," alisema Lampard.
"Tupo kwenye Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa. Hatuwezi kuonyesha woga sana dhidi yao. Tunatakiwa kuwaheshimu, lakini pia kushuka nao uwanjani na kucheza kwa aina yetu.
"Ninapowaangalia Barcelona, natarajia wao watashinda, lakini unatakiwa kujiamini mwenyewe. Tumewahi kuwapa wakati mgumu kipindi kilichopita na tuko tayari kujaribu kufanya hivyo tena."
Lampard pia alisema kwamba hakuna mvuto wa ziada kutokana na kipigo walichokipata mwaka 2009 dhidi ya Barca, siku ambayo Chelsea walinyimwa penalti kabla ya Iniesta kufunga bao la ushindi dakika za lala salama na wakafuzu kwa faida ya bao la ugenini.
"Hiyo kwa kweli haipo tena katika fikra zetu," alisema Lampard. "Wamepiga hatua kutoka miaka mitatu iliyopita nasi tumebadilika pia."
Lampard na wachezaji wenzake wamebakiza siku mbili tu za kujiandaa kuivaa Barca, lakini nyota huyo wa England mwenye umri wa miaka 33 hana shaka watakuwa tayari baada ya safari ya Spurs.
"Nafikiri ilikuwa ni ishara nzuri kwa Chelsea katika ubora wetu na watu wanavyofahamu jinsi tulivyuo sasa," Lampard alisema.
"Tulikuwa wa nguvu Uwanja mzima baada ya kipindi cha kwanza kigumu. Kipindi cha pili kilikuwa kizuri kama tulivyocheza msimu wote. Tuna kikosi kizuri na wote tulikuwapo wakati huo.
"Kama hauwezi kuchangamsha akili na mwili wako kwa ajili ya Barcelona, sijui wakati gani utafanya. Siwezi kuomba kupumzishwa kwenye mchezo huo kwa kwa kweli!"

CHACHA MARWA AONDOKA KAMBINI YANGA, THEO RUTTA ASAFIRISHWA, KUZIKWA JUMATANO

Chacha kulia
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam imezidi kuingia katika wakati mgumu, baada ya beki wake tegemeo, Chacha Marwa kuondoka kambini Mwanza leo baada ya kufiwa na mtoto wake.
Chacha amepanda ndege leo mjini Mwanza kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya msiba wa mwanawe, wakati timu inaelekea Kagera kwa ajili ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara, ikitoka kufungwa 3-2 na Toto African mjini Mwanza jana.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia bongostaz.blogspot.com mchana huu kwamba, Chacha anarejea Dar kwa mazishi ya mwanawe na kufanya mwendelezo wa kipindi kigumu kwa klabu yao.
“Kama inavyofahamika tupo kwenye msiba wa Mjumbe wa Kamati yetu ya Utendaji (Theonist) Rutashoborwa ambaye atazikwa Jumatano Bukoba.
Hatujamaliza hilo, linakuja na hili na Chacha kufiwa na mwanawe, kwa kweli hiki ni kipindi kigumu kwa klabu yetu,”alisema Sendeu.
Chacha anaacha pigo kubwa kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, ambayo kwa sasa inamkosa beki wake mahiri wa kati, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ anayetumikia adhabu.
Maana yake sasa, zaidi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyerejeshwa kwenye ulinzi kutoka kiungo, mabeki wa kati Yanga wanabaki wawili tu na ambao wote si chaguo la kwanza, Bakari Mbega na Job Ibrahim.
Yanga jana imeliweka rehani taji lake la ubingwa wa Ligi Kuu, kufuatia kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Toto African mjini Mwanza na hivyo kuziachia Simba SC na Azam FC mbio za ubingwa.
Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 53, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 50 wakati Yanga ni ya tatu kwa pointi zake 43, ingawa iko nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya timu hizo mbili zilizo juu yake.  
Yanga pia inategemea kushinda rufaa iliyokata kupinga kupokonywa pointi tatu ilizopata kwenye mechi dhidi ya Coastal Union wiki mbili zilizopita mjini Tanga, ili angalau kurejesha matumaini ya kutetea ubingwa.
Yanga ilipokonywa pointi hizo baada ya kumtumia beki Cannavaro, wakati alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Lakini klabu hiyo imeikatia rufaa hiyo, kwa sababu inadai iliruhusiwa kumtumia beki huyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Alfred Tibaigana.
Wakati huo huo: Mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Theonist Rutashoborwa umesafirishwa leo kwenda Bukoba kwa mazishi yatakayofanyika Jumatano.
Sendeu alisema baada ya sala na kuagwa kwa mwili huo leo, umesafirishwa na mazishi yatafanyika Jumatano.
Rutta atakumbukwa sana Yanga, hasa kutokana na jitihada zake zilizoisaidia klabu hiyo kupata ufadhili wa Yussuf Manji mwaka 2006. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.

SOMA KISA CHA OLIECH KUJITOA HARAMBEE STARS, NI KITAMU ILE MBAYA

Oliech
MWENYEKITI wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) amesikitishwa na kitendo cha Nahodha wa Harambee Stars, Dennis Oliech kustaafu soka ya kimataifa.
Oliech alitangaza kustaafu kupitia facebook, lakini watu walio karibu na mchezaji huyo, wameiambia SuperSport.com na bongostaz.blogspot.com ikatufikia kwamba mshambuliaji huyo wa Auxerre ya Ufaransa amekasirishwa na kitendo cha Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL) kutumia picha yake kwenye tangazo bila ridhaa yake.
Nyamweya pia amejipa matumaini ya kumaliza mgogoro huo kwa kutaka pande zote zitulie suluhu ikitafutwa.
"Kama unavyofahamu, hatuwezi kuchukua hatua bila kusubiri majibu ya wanasheria, ambao wamekuwa wakijadili suala lililowasilishwa na Oliech na tumeamua kutulia juu ya hili tangu mkataba umesainiwa tukiwa hatupo ofisini," alisema Nyamweya.
"Sitaki kuzungumzia zaidi, lakini tutasubiri hadi tukipata mawasiliano rasmi na mchezaji mwenyewe, kabla ya kuamua kuchukua hatua," alisema.
Oliech amekuwa hana furaha tangu picha yake kutumika kwenye tangazo bila kuhusishwa kwa lolote, japokuwa katika mkataba wa udhamini, Bodi ya Utawala ya Harambee Stars, imeipa EABL haki zote za kutumia picha za timu ya taifa katika promosheni zao.
“Ni siku ya machungu kwa soka ya Kenya,” aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook mshambuliaji huyo wa zamani wa Nantes.
“Kwa moyo mzito, natangaza kustaafu kwangu timu ya taifa mara moja. Ingawa nahisi sijatimiza malengo yangu katika kiwango hiki kwangu binafsi na kwa timu, imekuwa heshima ya juu kuvaa jezi ya timu ya taifa na kuiwakilisha nchi yangu. Pamoja na hayo, naitaikumbuka heshima hiyo.”
“Ningependa kuwashukuru wachezaji wenzangu na viongozi kwa sapoti waliyonipa miaka iliyopita. Siwezi kusahau hasa sapoti niliyokuwa ninapewa na mashabiki kwangu na kwa timu.
Nawashukuru kwa mchango wao na ninaungana nao kuwa nyuma ya timu na kuiombea dua Harambee Stars katika changamoto zilizo mbele yao,”alisema.
Tangu aanze kuichezea Stars akiwa kinda mwaka 2002, Oliech amekuwa tegemeo la safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Alifunga bao la ushindi lililoipa Kenya taji la michuano ya CECAFA Challenge akiwa ana umri wa miaka 19  mwaka 2002, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Harambee ikiwafunga wenyeji Tanzania Bara 3-2.
Alifunga pia bao la ushindi, Stars ikiifunga Cape Verde 1-0 na kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 nchini Tunisia. Oliech alipewa Unahodha wa timu mwaka 2010.
Hatua hii inakuja kiasi cha miezi kama miwili tangu MacDonald Mariga naye aisuse timu ya taifa kwa kutolipiwa gharama zake za kujiunga na timu kwa ajili ya mechi ya kuwania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani, dhidi ya Togo.
Mapema mwaka huu, kipa Arnold Origi alitangazaa kustaafu kuchezea timu hiyo kabla ya kurejea baada ya mazungumzo na kocha Francis Kimanzi na anatarajiwa kuichezea tena Stars Juni.

RUGE, SHIGONGO, ASHA BARAKA WAKABILIWA NA KASHFA YA KUCHAKACHUA FEDHA ZA MICHANGO MSIBA WA KANUMBA

Ruge kushoto na Shigongo kulia, kweli Kamati yao imechakachua fedha za msiba wa Kanumba?
MAJINA ya watu mashuhuri nchi hii, Erick James Shigongo na Rugemarila ‘Ruge’ Mutahaba- wote wakiwa ni wadau wa tasniya ya Habari yako hatarini kuingia doa.
Kwa nini? Hiyo inatokana na kuwamo kwao kwenye Kamati ya mazishi ya mwigizaji Steven Charles Kanumba, ambayo imeingia kwenye kashfa ya kuchakachua michango ya msiba.
Baadhi ya vyombo vya habari nchini leo vimeripoti kuwa, habari kutoka ndani ya familia ya Kanumba, imeituhumu Kamati hiyo kufanya uchakachuaji wa michango hiyo inayokadiriwa kuwa mamilioni ya fedha, achilia mbali vitu kadhaa, yakiwemo magunia 32 ya mchele.
Kamati ya Mazishi ilikuwa inaundwa  na Mwenyekiti Gabriel Mtitu, Makamu Mwenyekiti, Jacob Steven ‘JB’, Katibu, William Mtitu na Wajumbe Issa Mussa ‘Cloud’ (Mweka Hazina), Kimosa, Vincent Kigosi ‘Ray’, Single Mtambalike ‘Richie’, Dilesh Solanki, Millenne Happiness Magesse, Adele Kanumba (dada wa marehemu), Hartman Mblinyi, Ruge, Ally Choky, Simon Mwakifamba, Eric Shigongo, Steve Nyerere, Mahsein Awadh ‘Dk Cheni’ na Mama Nassor, mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Kanumba.
Je, ukweli ni upi. Ni matarajio sasa wahusika wataibuka kujibu tuhuma hizi, hasa ikizingatiwa Kamati iliundwa na watu watu wazito kama Eric Shigongo, mmiliki wa Global Publisher, Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Clouds Media Group.

JERRY SANTO AREJEA SIMBA SC NANE BORA CAF

Jerry Santo
KIUNGO wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo amesema yuko tayari kurejea klabu yake ya zamani ya Simba, iwapo itafuzu kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika mahojiano maalum (online) na bongostaz, Santo amesema kutoka Nairobi kwamba aliondoka Simba ili akacheze Albania lakini hakufanikiwa na wakati huo usajili wa Bara ulikuwa umekwishafungwa.
Alisema aliondoka Simba vizuri Novemba mwaka jana, baada ya kumaliza mkataba wake akiwa na lengo la kwenda kujiendeleza zaidi kisoka, lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa.
“Yalitokea mabadiliko ya uongozi katika klabu ambayo nilikuwa nakwenda, wale viongozi walionitaka waliondolewa madarakani, kwa hiyo ikashindikana mimi kucheza.
Nikarudi Nairobi, kwa bahati nzuri usajili wetu ulikuwa haujafungwa na mimi nikasajiliwa na timu yangu ya zamani, Tusker na nipo nacheza hapa sasa,” alisema.
Alipoulizwa kama uongozi wa Tusker utamruhusu kuondoka, alisema hilo halina tatizo kabisa kulingana na makubaliano na klabu hiyo wakati anasaini mwaka huu.
Aidha, Santo aliipongeza Simba kwa kufanikiwa kutinga hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ikiitoa timu ngumu ya ES Setif ya Algeria katika hatua ya 32 Bora.
Alisema atafurahi kuungana tena na wachezaji aliokuwa nao Simba kama mshambuliaji Emmanuel Okwi, kipa Juma Kaseja na wengine wote.
“Simba ni timu nzuri ambayo niliitumikia kwa uaminifu mkubwa na haikuwa na tatizo kuniruhusu kuondoka nilipopata nafasi Albania. Sioni kwa nini nisirudi wakinihitaji,”alisema kiungo huyo ambaye wakati anaondoka ‘aliwaliza’ Simba wengi.
Nafasi ya Santo kurejea Simba ipo kwa sababu hivi sasa klabu hiyo japokuwa ina wachezaji watano wa kigeni wanaokamilisha idadi kulingana na kanuni za usajili wa wachezaji wa kigeni Tanzania, lakini ni watatu tu wanaoingia kwenye kikosi cha kwanza chini ya kocha Mserbia, Milovan Cirkovic ambao ni Okwi kutoka Uganda, Patrick Mafisango kutoka Rwanda na Mzambia Felix Sunzu.
Mganda Derrick Walullya anayecheza nafasi ya ulinzi hana nafasi kabisa, wakati Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati anayecheza nafasi ya ushambuliaji, zaidi hutokea benchi na wakati mwingine huishia kuwa mtazamaji dakika zote 90.
Lakini pia Simba inasumbuliwa mno na nidhamu ya Mafisango anayecheza nafasi moja na Santo na mapema mwezi huu ilimsimamisha kabla ya safari ya kwenda Algeria kurudiana na Setif.
Na japokuwa ilielezwa Mafisango aliomba radhi akasamahewa na kusafiri na timu Algeria, lakini ukweli ni kwamba uongozi wa Simba ulimsamehe kwa kuzingatia umuhimu wake katika nafasi hiyo.
Santo hucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi, lakini utapenda umakini wake uwanjani- utoaji wa pasi za uhakika hasa ndefu- na zaidi anapoamua kusaidia mashambulizi.
Kiungo hodari, mwenye kipaji, anayejituma- ndivyo unavyopaswa kumzungumzia Santo ambaye kwa sasa anaibeba klabu iliyomuinua kisoka, Tusker.

Sunday, April 15, 2012

CHELSEA WAHARAKISHA TEKNOLOJIA KWENYE GOLI ENGLAND

Spurs wakimlalamikia refa Atkinson
Ekotto akikzuia shuti la Mata kabla halijavuka mstari
JARIBIO la mwisho la kutumia teknolojia kwenye mstari wa goli, litafanyika baadaye mwezi huu kabla ya watengeneza sheria wa FIFA kutoa uamuzi Julai, mwaka huu, bongostaz imeipata hiyo kutoka FIFA baada ya utata mwingine mkubwa kujitokeza jana.
Chelsea imetinga fainali ya Kombe la FA kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Tottenham, huku marudio ya kamera yakionyesha shuti la Juan Mata lililoipatia Chelsea bao la pili halikuvuka mstari.
''Tumekuwa tukililia teknolojita kutumika kwenye mstari wa goli kwa muda mrefu sasa,'' alisema beki wa Chelsea, John Terry. ''Acha tutumai sasa watu watachukua uamuzi sahihi.''
Bodi ya Vyama vya Soka ya Kimataifa, Bodi ya Kutunga Sheria za Mchezo, mwezi uliopita waliafiki mifumo miwili kuingia katika awamu ya pili ya jaribio la teknolojia kabla haijaruhusiwa kutumika katika kikao cha Julai 2.
''Kikao cha mwisho kilipangwa kufanyika Ijumaa, na awamu ya pili ya jaribio itafanyika mwishoni mwa Aprili, na itaendelea hadi Mei,'' imesema FIFA katika taarifa yake iliyoifikia bongostaz.   
IFAB lazima ijiridhishe na kasi na ufasaha wa kifaa cha Hawk-Eye au GoalRef kabla kuamua viwe msaada kwa marefa katika uamuzi juu ya mabao yenye utata wa kuvuka au kutovuka mstari.
Kamera aina ya Hawk-Eye ya Sony Corp ni kamera inayoendana na kasi ya mpira na inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuaminika katika tenisi na Kriketi. GoalRef, inamilikiwa na kampuni ya Mjerumani Denmark, ambayo wataalamu wengi wanaamini inaweza kuwa suluhisho.
Mifumo yote miwili inatoa jibu kwa refa ndani ya sekunde tu kuhusu mpira kama umevuka mstari wa goli, ambayo itatoa nguvu ya kutoa uamuzi wa mwisho.
Katika mechi ya Jumapili, Uwanja wa Wembley, marudio ya Televisheni mara moja yalionyesha kwamba shuti la Mata mwanzoni mwa kipindi cha pili, halikuvuka mstari wa goli na lilizuiwa vema na beki wa Tottenham, Benoit Assou-Ekotto kwa umahiri mkubwa.
Hata wachezaji wa Chelsea, baadaye walikiri bao hilo halikupaswa kukubaliwa.
FIFA iliamua kuunga mkono teknolojia kwenye mstari wa goli baada ya tukio la kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 lililoihusisha timu ya Terry, England na kumshawishi rais Sepp Blatter kwamba usumbufu huo ni vema ukaepukwa katika michuano mikubwa.
Shuti la kiungo wa Chelsea, Frank Lampard katika mechi na Ujerumani kwenye Fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini liligonga mwamba wa juu na kuangukia ndani ya mstari wa goli, lakini halikuhesabiwa kama bao na England ikatolewa mashindanoni.
FIFA inatumaini mojawapo ya mifumo hiyo itakuwa tayari kutumika Desemba katika Klabu Bingwa ya Dunia nchini Japan.
Lakini kwa Ligi Kuu, matumaini ni kwamba itawekeza mfumo huo kwenye viwanja vyake 20 kabla ya kuanza msimu mpya Julai.
IFAB inaundwa na vyama vitatu vya soka Uingereza jumlisha wajumbe wanne wa FIFA, na kura sita ndizo zitaamua juu ya mabadiliko hayo.
Martin Atkinson, refa mwenye heshima kubwa FIFA, ambaye alitoa bao hilo la utata jana katika Nusu Fainali ya FA, atakuwa mmoja wa wasaidizi wa Howard Webb katika teknolojia ya bao kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Ulaya, Euro 2012 inayoanza Juni 8 hadi Julai 1, mwaka huu.

CHELSEA YATUMA SALAMU BARCA, YAUA 5-1 NA KUTINGA FAINALI FA

Didier Drogba (wa tatu kushoto) akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kufunga kwenye Uwanja wa Wembley, London leo. Chelsea ikishinda 5-1 dhidi ya Spurs Nusu fainali ya FA
KLABU ya Chelsea usiku huu imeitandika Tottenham Hotspur mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Wembley na kutinga fainali ya Kombe la FA ambako itamenyana na Liverpool.
Shukrani kwao Didier Drogba, Juan Mata, Ramires, Frank Lampard na Florent Malouda waliofunga mabao hayo, yanayoiwezesha Chelsea kucheza fainali ya nne ya Kombe la FA ndani ya miaka sita.
Bao pekee la Tottenham lilifungwa na Gareth Bale.
Ushindi huo unakuja wakati Chelsea inaelekea kwenye mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona Uwanja wa nyumbani, Stamford Bridge Jumatano.

MAN UNITED KAMA SIMBA BONGO





KLABU ya Manchester United imejiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya England, kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa Old Trafford, Manchester.
Hadi mapumziko, Man United walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Wayne Rooney kwa penalti dakika ya saba na Danny Welbeck dakika ya 43.
Rooney aliwainua tena vitini mashabiki wa Man U dakika ya 73 alipofunga bao la tatu na Nani akafunga la nne dakika ya 90.
United sasa ina pointi 82, baada ya kucheza mechi 34, sawa na wapinzani wao Man City wenye pointi 77.
Arsenal ni ya tatu kwa pointi zake 64, Spurs ya nne kwa pointi zake 59 sawa na Newcastle ya tano, wakati Chelsea yenye pointi 57 ni ya sita.  

MAMA KANUMBA ATOA WOSIA

Mama Kanumba na Asha Baraka kulia
MAMA Mzazi wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba amewataka wasanii wanachama wa Mtandao wa Wasanii Tanzania
(SHIWATA) kuendeleza ushirikiano alioacha mwanae.
 Akizungumza katika ibada ya kumuombea mwanae iliyoandaliwa na (SHIWATA) leo  Dar es Salaam, Mama Kanumba alisema amefarijika kuona
wasanii wanaendelea kumuombea mwanae kila kona ya nchi.
"Nawashukuru SHIWATA kwa moyo wa ipendo na ushirikiano mlionesha kwa familia yangu, naomba muendeleze ushirikiano mliokuwa nao wakati mwanangu akiwa nanyi, endeleeni kushirikiana" alisema Mama Kanumba.
Katika ibada hiyo iliyoongozwa na mchungaji wa Kanisa la Elim Pentekoste Ilala Bungoni, Mchungaji Livingstone Mwaitela alisema wasanii na familia ya Kanumba wasisononeke kwa sababu Mungu alimpenda mtoto wao huyo zaidi.
 Alisema wasanii waendelee kumkumbuka mwenzao kwa kubadili mambo yasiyompendeza Mungu badala yake wajiandae kwa kufanya mambo ambayo
yanampendezesha na kujiweka tayari siku akiwaita wawe tayari.
Mwenyekiti wa SHIWATA,Caasim Taalib alisema Kanumba alikuwa mwanachama wao namba 648 akiwa mmoja wa waliojitokeza kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga nyumba za wasanii kutoka Bagamoyo, Kisarawe na hatimaye kufanikiwa kupata eneo Mkuranga.
Marehemu Kanumba alifariki Aprili 5, wakati akikimbizwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kuanguka nyumbani kwake
Sinza kufuatia ugomvi wa mapenzi na msanii mwenzake Elizabeth Michael (Lulu).
 

MGAMBO, POLISI HAKUNA MBABE

Fainali ya 9- Bora ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao imeendelea kushika kasi leo (Aprili 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro kwa Mgambo Shooting ya Tanga kuvutwa shati.Mgambo Shooting ambayo hadi kabla ya mechi za leo (Aprili 15 mwaka huu) ilikuwa ikiongoza kwa pointi 11 imelazimishwa sare ya mabao 2-2 na Polisi Tabora ambayo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Mabao ya Polisi Tabora yalifungwa dakika ya tano na Ernest Nkandi kwa shuti kali lililomshinda kipa Kulwa Manzi. Keneth Masumbuko aliifungia Polisi Tabora bao la pili dakika ya 40.
Mgambo Shooting inayofundishwa na beki wa zamani wa Taifa Stars, Joseph Lazaro ilikianza kipindi cha pili kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao dakika ya 58 lililofungwa kwa shuti kali nje ya eneo la hatari na Salum Kipaga.
Dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho, Juma Mwinyimvua aliipatia Mgambo Shooting bao la kusawazisha akimalizia pasi ya Fully Maganga kutoka wingi ya kushoto.
Fainali hiyo inashirikisha timu tisa ambapo tatu za kwanza zitafuzu kucheza VPL msimu ujao. Timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ni Rhino Rangers ya Tabora, Trans Camp ya Dar es Salaam, Mbeya City, Tanzania Prisons ya Mbeya na Mlale JKT ya Ruvuma.

 

SIMBA YAZIDI KUPAA LIGI KUU, YANGA YAKALISHWA NA TOTO LAKE KIRUMBA

Simba SC
SIMBA SC wamejiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kufuatia ushindi wa 1-0 jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Ruvu Shooting.
Shukrani kwake kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 80.
Simba sasa ina pointi 53, tatu zaidi dhidi ya azam FC inayoshika nafasi ya pili.

CCM KIRUMBA MWANZA
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, wenyeji Toto African walifanya kile ambacho hakikutarajiwa na wengi.
Toto wamewafunga ‘baba zao’ Yanga mabao 3-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mabao ya Toto inayopigana kuepuka kushuka daraja, yalitiwa kimiani na Mussa Said aliyefunga mawili dakika ya 18 na 39, Kulwa Mobbi dakika ya 24 Iddi.
Hamisi Kiiza aliifungia Yanga mabao mawili dakika ya 43 na 65.
Yanga inabaki na pointi zake 46 katika nafasi ya tatu, dhahiri sasa inaelekea kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu.
Kocha Mserbia, Kosradin Papic alizomewa na mashabiki wa Yanga mjini Mwanza kutokana na kiwango kibovu ambacho timu hiyo inacheza hivi sasa.
Kipigo cha leo kinamaanisha Yanga imepoteza mechi mbili mfululizo, kwani mechi iliyopita na Coastal Union mjini Tanga, japokuwa walishinda 1-0, lakini walipokonywa pointi hizo na Kamati ya Ligi Kuu.

AZAM, CHAMAZI, DAR ES SALAAM
Villa Squad nayo iliitandika Coastal Union ya Tanga mabao 4-2 kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.

MGAMBO NA POLISI NANI ZAIDI LEO?

LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Mgambo Shooting ya Tanga na Polisi Tabora Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mgambo ndio inaoongoza ligi hiyo kwa pointi zake 11 wakati Polisi Tabora ina pointi nne. Mechi ya pili itakuwa kati ya Polisi Morogoro yenye pointi kumi na Polisi Dar es Salaam yenye pointi sita.
Mechi ya pili itakuwa kati ya Polisi Morogoro yenye pointi kumi na Polisi Dar es Salaam yenye pointi sita.
Jana Tanzania Prisons ya Mbeya na Mlale JKT ya Ruvuma zimetoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa fainali za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) uliochezwa leo (Aprili 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini hapa.
Kwa sare hiyo Tanzania Prisons imefikisha pointi nane wakati Mlale JKT inazo tano. Timu tatu za kwanza katika fainali hiyo ya 9 bora zitapanda kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao.
Mlale JKT ndiyo walioanza kufunga dakika ya 61 kwa mpira wa adhabu uliopigwa nje ya eneo la hatari na mshambuliaji Edward Malimi katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Shabani Shata kutoka Kigoma.
Dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho beki Richard Mwakalinga aliisawazishia Tanzania Prisons inayofundishwa na Stephen Matata baada ya kufanya shambulizi kubwa langoni mwa Mlale JKT.
Hadi tuna kwenda mitamboni, mechi ya pili kati ya Rhino Rangers ya Tabora na Mbeya City ya Mbeya ilikuwa ikiendelea huku Rhino Rangers ikiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 18 na kiungo Salum Tabayi.

MISS UTALII KINONDONI KUFANYIKA SAN SIRRO

Warembo Miss Utalii Kinondoni msimu uliopita
Shindano la kumpata Binti wa Utalii Kinondoni 2011/2012(Miss Utalii Kinondoni 2011/2012 ngazi ya wilaya limepangwa kufanyika katika ukumbi wa kisasa na Club ya kimataifa ya San Siro, iliyoko Shekilango Sinza.Shindano hilo limepangwa kufanyika siku ya Ijumaa tarehe 25 Mei 2012 na kushirikisha mabinti 25 kutoka katika majimbo yote ya wilaya ya Kinondoni.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa Miss Tourism Tanzania Organisation wilaya ya Kinondoni Pius Yalula,ambao ndio waratibu na waandaaji wa shindano hilo, washiriki wote wanatarajia kuanza kambi ya mazoezi katika ukumbi huo siku ya Jumatatu Mei 1,2012. Miss Utalii Kinondoni 2010/2011 Sophia Dioa ambaye pia ni Miss Utalii Dar es Salaam 2010/2011 na Miss Utalii Tanzania 2010/2011.

Piusi Yalula alibainisha kuwa ni mpango mkakati wa Miss Tourism Tanzania organisation mwaka huu, wa kuwafuata watanzania hususani vijana katika maeneo yao ya burudani,ili kuwahamasisha juu ya utalii wa ndani. Ndio maana fainali za mwaka za Miss Utalii Kinondoni ,tumeamua kuzifanyia katika Club ya Sunciro, ambako tunaamini kuwa vijana na watu wa rika mbalimbali wanapenda kwenda katika kumbi na club za aina hiyo kwa ajili ya burudani na mapumziko ya wikendi. Utafitin uliofanywa na kitengo chetu cha masoko umebaini kuwa ili dhana ya utalii wa ndani iweze kufanikiwa ni lazima tuanze na watu hususani vijana ambao tayali ni wapenzi wa burudani na wako tayali kutumia sehemu ya pato lao kwaajili ya burudani na mapumziko ya mwishoni mwa wiki. Tutatumia shindano hili la Miss Utalii Kinondoni 2010/2012 kuwahamasisha wapenzi wa burudani, vijana na watu wa rika zote kujenga tabia ya kwenda kuembelea vivutio vya utalii nchini ,hususani vya wilaya ya kinondoni na pia kuwaelimisha wao na jamii kuwa Utalii na Burudani kama zilivyo burudani nyingine na ni fulsa nzuri ya mapumziko ya mwishoni mwa wiki, tena wakati mwingine kwa garama ndogo,kwani Serikali na mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) wameweka bei isiyo zidi shilingi 1500 kwa mtu mzima na shilingi 500 kwa watoto.
Fomu kwaajili ya kushiriki shindano hilo zinapatikana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Sunsiro Club Shekilango, Zizzu Fashion Victori,Sea Boys Magomeni,BM Saloon Kinondoni, Dar es Salaam City Collage Kimara,Chicken Hut mlimani City, Angel Saoon Sinza,Coco Beach OyterBay na katika ofisi za Miss Tourism Tanzania Organisation zilozoko Ilala Bungini na Kimara Dar es Salaam.
Pous aliongeza kuwa fainali za mwaka huu za Binti/Miss Utalii kinondoni 2011/12 zitakuwa ni za kipekee kutikana na kamati ya maandalizi kujipanga vilivyo ,ili kuhakikisha huwa taji la Miss/Binti Utalii Dar es Salaam linabaki kinondoni na pia kuhakikisha tunachukua taji la taifa la Miss /Binti Utalii Tanzania 2011/12 mwaka huu. Sifa za kushiriki shindano la Miss /Binti utalii Tanzania ni pamoja na Elimu isiyo pungua kidato cha sita au yenye kulingana nayo, uwezo wa kuzungumza kiswahili fasaha,urefu wa angalau setimita 160 au zaidi, raia wa tanzania, ngozi na rangi asili,jinsia halosi ya kike, umri usio pungua miaka 18 wala kuzidi miaka 27 na awe ni mwenye tabia na mwenendo ,tabia njeama na mfano wa kuigwa katika jamii.
Asante,
Pius Yalula
Mkurugenzi Miss Utalii Kinondoni
Miss Tourism Tanzania Symbol Of National Heritage - Do Value Added Pageant
"Lets Visit & Promote Tanzania National Parks -Tourism is Life ,Culture is Lining"
Regard,
Gideon E.G. Chipungahelo
PRESIDENT / C.E.O
Hotline: + 255 - 715/754/773 - 318 278.

KWA NINI MAREFA WA AZAM WANAPIGWA SANA?

Kinatra wa mabao wa Azam FC, John Bocco kushoto
KWA mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili, jana refa aliyechezesha mechi iliyoihusisha Azam FC alipigwa na mashabiki baada ya mechi.
Azam ilishinda 1-0, beo pekee la beki wake wa kati wa kimataifa wa Tanzania, Aggrey Morris Ambroce dakika ya 83 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi Dodoma.
Ushindi huo, unaifanya Azam itimize pointi 50, sawa na Simba SC ambayo sasa inaongoza ligi hiyo kwa mabao tu zaidi ya kufunga.
Yanga inabaki nafasi ya tatu kwa pointi zake 44 na haitaweza kupanda hata ikishinda leo dhidi ya Toto Africa mjini Mwanza.
Simba inaweza kuiacha Azam kwa pointi tatu, iwapo itaifunga Ruvu Shooting leo Uwanja wa Taifa.
Katika mchezo wa jana, Polisi Dodoma, ilipata pigo baada ya beki wake, Bakari Omari kutolewa nje kwa kadi nyekundu, dakika ya 57 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Refa  wa mchezo huo alipigwa na mashabiki kwa madai ya kuwapendelea Azam, baada ya mpambano kukamilika, lakini askari walifanikiwa kumuokoa asipokee kipondo zaidi.
Mwezi uliopita, refa aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Azam, Israel Nkongo alipigwa na Stefano Mwasyika na angeweza kupigwa pia na mashabiki wa Yanga.
Kwa nini apigwe? Kisa kutuhumiwa kuipendelea Azam. Mechi zinazochezwa kwenye Uwanja wao, timu nyingi zimekuwa zikilalamika Azam inabebwa.
Kwa muda mrefu wapenzi wa soka Tanzania wamekuwa wakilalamikia desturi ya klabu kongwe nchini Simba na Yanga kutamba nyumbani, kudaiwa kushinda kwa kununua mechi.
Hii inasababisha timu zetu zinakuwa dhaifu kwenye michuano mikubwa na ndiyo maana zinashindwa japo kucheza hatua ya makundi tu ya michuano ya Afrika.
Watu wanataka timu ishinde kwa uwezo, ili idhihirishe ubora ambao utakwenda kuifanya ishiriki vyema michuano ya Afrika.
Kwa sababu hiyo, ujio wa Azam FC timu inayomilikiwa na Milionea Said Salim Bakhresa ulipokewa kwa furaha na wadau wa soka nchini, wakijua amepatikana mkombozi wa kweli.
Azam imewekeza fedha nyingi kuanzia kwenye usajili, ajira za makocha, Uwanja wake kule Chamazi- na kwa ujumla ni timu ambayo ukiangalia inapoelekea unajenga matumaini.
Azam haina wanachama wa kuleta mizengwe ya kuvuruga timu, wanaweza kujivuruga wao kwa wao tu.
Mchezaji wa Azam hachezi kwa presha ya kutukanwa na mashabiki akikosea kama mchezaji wa Yanga au Simba. Azam imesajili wachezaji nyota kuanzia ndani na nje ya nchi.
Azam inaongoza kutumia fedha nyingi na kusajili wachezaji bora nchini. Hivyo timu hii inastahili kuwa bingwa wa nchi kulingana na jinsi ilivyowekeza.
Lakini wasiwasi ni kwamba, mechi zao zinatiliwa shaka sasa nao kama wanatumia mbinu chafu ikiwemo kuhonga marefa ili kushinda.
Kama kweli watakuwa wanafanya hivyo, ina maana watakuwa wanaiga Simba na Yanga, ambazo kimsingi zinanyooshewa kidole kwa kudumaza maendeleo ya soka ya nchi hii.  
Kama Azam wanaiga Simba na Yanga kununua mechi, wanaweza wakafanikiwa kuwa mabingwa, lakini swali la kujiuliza soka ya Tanzania itakuwa kweli imepata mkombozi?
Napata shaka sana juu ya mustakabali wa soka ya nchi hii, ikiwa Azam nayo inakuja kwa staili hii- dhahiri  bado tuna kazi ngumu na safari ndefu kufikia japo karibu na mafanikio.
Kwa sababu mchezaji akishajua kwamba kuna unafuu katika mchezo kutokana na mabosi wao kuhonga, hawezi kujituma tena kwa sababu anajua ushindi upo tu.
Mwaka 2007, baada ya Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Esperance ya Tunisia, aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Ivo Mapunda aliwashauri viongozi wa klabu yake wakati huo, wawe wanafanya mipango na marefa kurahisisisha mechi.
Tayari mchezaji kujenga dhana hiyo- inamaanisha amefikia mwisho wa uwezo wake, wakati suluhisho ni kufanyia kazi mapungufu ili wakati mwingine ufanye vizuri.
Mwaka juzi, Simba ilifungwa 5-0 na Haras El Hodood nchini Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho,  mwaka ilifungwa 3-0 na Wydad Cassablanca, mara zote ikitolewa katika michuano ya Afrika.
Mwaka huu, imefungwa 3-1 ikitoka kushinda 2-0 nyumbani na ES Setif moja ya timu tishio tu Afrika na kuingia hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho.
Hii nini maana yake? Simba imefanyia kazi mapungufu kutoka kufungwa 5-0, 3-0 na 3-1 sambamba na kusonga mbele.      
Lakini desturi ya kutaka kurahisisisha kazi kwa kununua mechi- maana yake hatuwezi kufanyia kazi mapungufu.
Kweli wapenzi wa soka Tanzania wanaitegemea Azam iijengee heshima nchi hii katika michuano ya Afrika, lakini kwa staili ambayo wanataka kwenda nayo. Hakuna hakika kama watafanikiwa.
Yapo maneno tayari yanasemwa semwa kuhusu Azam na harakati zao za ubingwa na mbinu wanazodaiwa kutumia hadi watu wanaodaiwa kutumiwa kutoka kwenye mamlaka husika- japo kwa sasa tunayachukuliwa kama maneno ya mtaani tu, lakini ipo haja ya kuiangalia Azam kwa jicho la tatu.
Na tufanye hivyo zaidi kwa maslahi ya Azam yenyewe na mustakabali wa soka yetu kwa ujumla- kwani wakubwa hawana cha ziada zaidi ya kufikiria kuchukua chao mapema- lakini inayosulubika ni soka yetu. Tunasemaje sasa?
Tuendelee kufurahia Azam ikishinda marefa wa mechi zao wakisulubiwa, au tuambiane ukweli mambo yaende? Tutafakari kwa makini.

Saturday, April 14, 2012

MESSI AMKAMATA RONALDO, BARCA, REAL ZOTE ZAUA LA LIGA

Messi
MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Lionel Messi amefunga bao la penalti dhidi ya Levante usiku huu na kufikia rekodi ya Cristiano Ronaldo katika Ligi Kuu ya Hispania ya kufunga mabao 41 msimu mmoja, aliyoiweka saa chache kabla.
Messi alitumbukiza mkwaju wake wa penalti dakika ya 72 na kuipa Barcelona ushindi wa 2-1 na kumfikia Ronaldo, ambaye aliweka rekodi hiyo kwa bao la dakika ya 74 la kichwa katika ushindi wa Real Madrid wa 3-1 dhidi ya Sporting Gijon.
Madrid imeendelea kuongoza La Liga kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya mabingwa watetezi mara tatu, Barcelona kabla ya mechi baina ya timu hizo, maarufu kama El Clasico wiki ijayo, ambayo itatoa picha yam bio za ubingwa msimu huu zikiwa zimebaki mechi nne ligi kufikia tamati.

No comments: