Saturday, August 6, 2016

Wenye watoto wa Vichwa vikubwa na Migongo wazi Mtwara washauriwa kutowaficha watoto wao.


Mmoja wa wzazi akiwa na mtoto wake mwenye tatizo la kichwa kikubwa ambaye amepatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula.



Daktari bingwa wa upasuaji kutoka MOI, Mwanahabasi Suwed.



 Na Juma Mohamed, Mtwara.

Baadhi ya wazazi wenye watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi katika mikoa ya Lindi na Mtwara wameshauriwa kuacha tabia ya kuwafungia ndani watoto wao na baadala yake wawapeleke hospitalini kwa matibabu wanaposikia ujio wa madaktari bingwa wakutibu magonjwa hayo.
Wakizungumza katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, baadhi ya kina mama wenye watoto hao waliobahatika kupata huduma za madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI), walisema awali ugonjwa huo uliwakatisha tamaa na kudhani hauwezi kutibika.
“Baada ya kukaa ndani mtoto yule ndio kuna siku nikaona kichwa kinazidi kuongezeka tu na kinaendelea tu..tukawa tumekaa ila juzi ndio tukasikia kuna watu hao wametoka huko Dar (Dar es Salaam) wamekuja Mtwara, ndio tukasema twende tukajaribu huko mamaangu akakubali tukaja nae hadi hapa wametupokea vizuri na hivi ninavyosema mtoto wangu anaendelea vizuri..” alisema Salma Ally, mkazi wa Lindi.

Salma Ally, mkazi wa Lindi ambaye mtoto wake amepatiwa matibabu ya tatizo la kuwa na kichwa kikubwa.


Naye, Zenat Ally mkazi wa Mtwara, alisema aliamua kufika hospitalini hapo baada ya kusikia matangazo juu ya kuwepo kwa madaktari bingwa wanaotoa matibabu hayo, ndipo akaona amuwahishe mwanae apate matibabu.
Daktari bingwa wa upasuaji wa vichwa, migongo na mishipa ya fahamu kutoka MOI, Mwanahabasi Suwed, alitoa ushauri kwa wanawake walio katika umri wa kushika ujauzito namna ya kujikinga ili kuhepuka na kujifungua watoto wenye matatizo hayo.
“Mara nyingi hili tatizo linasababishwa na ukosefu wa madini yanaitwa Phoric Acid ambayo tunayapata kwenye mboga za majani za kijani na matunda, kwahiyo tunashauriwa wanawake wote ambao wapo kwenye umri wa kuweza kushika mimba kuweza kupata hivi vidonge ambavyo nadhani kidonge kimoja vinauzwa sh. 50 kuwa unakunywa kila siku pamoja na kula mboga za majani na matunda..” alisema.
Afisa habari wa GSM Foundation ambao ndio wafadhili wa mpango wa kutoa huduma hizo Khalfan Kiwamba alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata matibabu hayo.
Hata hivyo, muitikio kwa wakazi wa Mtwara katika kujitokeza kupeleka watoto kupata matibabu hayo umetajwa kuwa ni mdogo tofauti na matarajio ambapo ni watoto sita pekee ndio waliopata matibabu hayo kwa muda siku Nne huku matarajio yakiwa ni watoto 40.


No comments: