Friday, March 4, 2016

MKUCHIKA: Mnaosema Unyago hauna umuhimu, mkome na muache..

Mbunge wa Newala mjini (CCM) Mhe. George Mkuchika, akichangia jambo katika kikao cha bodi ya barabara.



Mbunge wa viti maalum (Chadema), Tunza Malapo, akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kikao cha bodi ya barabara wiki mbili zilizopita mjini Mtwara.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

 MBUNGE wa Newala mjini (CCM), Mhe. George Mkuchika, amepingana na sehemu ya taarifa iliowasilishwa na sekta ya kilimo katika kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) inayoeleza kuwa sherehe za unyago hazina ulazima hivyo zinachangia matumizi mabaya ya chakula.
Akizungumza mbele ya mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuchika alidai kuwa kipengele hicho kilimchefua kwasababu kila kabila katika nchi hii lina mila na desturi zake, hivyo sio vizuri kukosoa mila za kabila Fulani pasipo kujua faida zake.
“Nataka niwaambie, wiki mbili zilizopita kulikuwa na hotuba ya baba wa Taifa na alikuwa anasema juu ya waandishi wa habari, akasema wasomaji tunapenda kusoma habari zilizoandikwa vizuri na zenye elimu nzuri, na mwalimu akasema ipo elimu nyingine hauipati kwenye magazeti na akasema kwa mfano elimu ya jandoni..kwahiyo Baba wa Taifa wan chi hii anajua kuwa Jandoni kuna elimu..” alisema na kuongeza:
“Leo mumekuja kuleta ‘paper’ hii mlijua hapa kuna Wamakua, Wayao, Wamakonde, Wamwela ambao wana mila na desturi za unyago..naombeni sana mtukome na muache..” aliongeza.

Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katan Ahmed, akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kikao cha bodi ya barabara wiki mbili zilizopita mjini Mtwara.


Alitumia muda mrefu kuwaeleza wajumbe wa kikao hicho mambo mbalimbali yanayohusu jando na unyago ambapo alisema katika makabila ya Mtwara na Lindi wanapitia katika hatua zaidi ya Tano kwa watoto wanaokuwa kwenye Jando ikiwa pamoja na kupelekwa Jandoni, Kualuka na Kuolewa ambapo kunaambata na kikao cha kumfunda yeye na mume wake vie watakavyoishi katika ndoa yao.
Alisema kuwa majukumu hayo yanatekelezwa na watu wazima na kudai kuwa hata kwa wajumbe ambao walikuwepo kwenye kikao hicho hakukuwepo ambaye ana umri unaofanana nao, na kwamba hata yeye alikaa porini kwa ajili ya unyago kwa kipindi cha miezi Miwili.
“Anatoka Jandoni motto anaambiwa ni marufuku kwenda chumbani kwa baba na mama..ndio maana mdogo wako ukigombana naye ambaye hajaaluka anakuchokoza alafu anakimbilia chumbani kwa baba na mama ni kwasababu anajua wewe uliyealuka huwezi kuingia kule, sasa jamani mambo haya ni kuheshimiana, mimi nina uhakika Wanyamwezi wana taratibu zao kuelimisha watoto wao na Wasukuma na wengine.” Alisema.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akizungumza katika kikao cha bodi ya barabara.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego, alimshukuru Mkuchika kwa maelezo yake na kusema kuwa kwa kiasi kikubwa makabila mengi hapa nchini taratibu zao zinafanana na kwamba wale ambao hawazifuati madhara yake wanayajua, na kile kilichowasilishwa katika kikao hicho kutoona umuhimu wa jando na unyago, ni kwamba labda mwandishi aliteleza wakati wa uandishi katika kabrasha.
“Nafikiri ni mwandishi tu aliteleza kuliweka vizuri, kuna shughuli zingine tunazifanya kwa kusherehesha ambazo zinasababisha kaya kuingia kwenye njaa pasipo sababu za msingi lakini sidhani kama yupo mtu mzima hapa atadharau maana ya jando na unyago, na watoto wetu wanakosa kwa kiwango kikubwa ndio maana wanapungukiwa kwenye mengi lakini kwa wengine ambao tumepita huko tunaelewa maana yake Mheshimiwa..kwahiyo tuko pamoja, kweeeeeli tumekoma” alisema.  




No comments: