Tuesday, December 8, 2015

Mkurugenzi wa halmashauri Mtwara awashukia waandishi kwa kuripoti taarifa za 'Magofu' ya nyumba za walimu.




Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mtwara vijijini, Tamimu Kambona.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

KUFUATIA baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kutoa taarifa za uchakavu na uhaba wa nyuma za walimu katika shule za msingi za Mkubiru na Msangamkuu katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara vijijini, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tamimu Kambona, amekuja juu na kuwataka waandishi wa habari kuacha kufanya kazi na halmashauri hiyo.
Akizungumza katika sherehe za kumuaga mwalimu mstaafu wa shule ya msingi Mkubiru, Ally Mpomo, zilizofanyika shuleni hapo, Kambona alisema kitendo hicho kilichofanywa na waandishi wa habari ni “Ujinga na Ulofa,” akinukuu maneno ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin W. Mkapa aliyoyasema wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Alisema, waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele zaidi kuandika mabaya yanayotokea kuliko mazuri yanayofanywa, huku akikiri kuwa yale mabaya yanayoandikwa ni kero kwa wahusika hivyo yanahitaji kupatiwa msaada kwa kuyatatua.
“Lakini tatizo tu la nyumba ya mwalimu kuwa mbovu ndio walioliona wao lakuongea, nawaomba waandishi wa habari, kama mtapenda kuandika habari zetu andikeni, kama msipopenda hachaneni na sisi..lakini lazima eti kwasababu amesema tutumbue majipu, mimi nasema na ninasema hili waandishi wa habari kote waliko kuanzia wale wa Chanel Ten na wengine waliokuwa wanapenda kuongea hayo, ukipenda kuongea mabaya kumuka na yale mazuri tunayoyafanya kwanini baya letu moja mulizungumze lakini mema yetu elfu mbili hamzungumzi?..” alihoji Kambona ambaye pia ni afisa elimu ya Msingi katika halmashauri hiyo.

Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya msingi Msangamkuu, Zaitun Mkamumba, akiwa mbele ya moja ya nyumba za walimu zilizopo katika shule yake.

Alisema, taarifa hizo zilirushwa kwenye vyombo vya habari mbalimbali karibu wiki nzima kwa mfululizo na kwamba alipigiwa simu na kuambiwa aangalie chaneli moja mabayo ilikuwa ikirusha taarifa hiyo.
“Nawaambia waandishi wa habari mliokuwepo hapa na wasiokuwepo mkawaambie, na ikiwezekana mimi sitokuwa tayari kutoa ushirikiano na wao kama wataendelea na tabia hii..naomba niishie hapo, lakini itakuwa vibaya au ni vizuri nikisema kama alivyosema Rais wa awamu ya tatu alivyosema mzee Benjamin William Mkapa, wakati wa uzinduzi wa kampeni, ni ujinga naa....mshamalizia..” aliongeza.
Wiki mbili zilizopita, walimu wa shule hiyo walipaza sauti zao kulalamikia ugumu wa maisha wanaoupata kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha ambazo haziendani na kipato wanachokipata kwa mwezi, na kujikuta wanakabiliwa na madeni.
Wakizungumza na Nipashe, walisema kuna mambo mengi ambayo yamekuwa ni changamoto katika mazingira yao ya kazi, ikiwa ni pamoja na miundombinu mibovu katika shule yao kiasi cha kuzidi kuyafanya maisha yao kuwa magumu.
Moja ya changamoto ambazo walizieleza ni kukosekana kwa nyumba za walimu shuleni hapo na kusababisha walimu wengi kuishi maeneo ya kijijini ambako wanalazimika kupanga na kulipa kodi kila mwezi huku wakikabiliwa na changamoto nyingine ya usafiri wa kutoka huko wanakoishi mpaka kufika shuleni kiasi cha kulazimika kutumia pesa kwa ajili ya nauli ya pikipiki za kubeba abiria (Bodaboda).
“Hali ya mshahara na maisha yalivyopanda haviendani, na hii ndio maana inasababisha baadhi ya walimu kujihusisha na biashara labda zingewza kuwakwamua..mshahara nalipwa sh. 350,000 na matumizi yangu kwa mwezi yanafika sh. 520,000, kwahiyo mwisho wa mwezi najikuta nakabiliwa na madeni sana mpaka inafikia wakati tunagombana na wenye nyumba maana kama majengo unavyoyaona hakuna nyumba za waalimu sisi tuliokuwa wengi tunaishi mitaani kwa kupanga..” alisema mwalimu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa.
Alisema, kuna mahitaji ambayo analazimika kuyapata kila siku na yanahitaji pesa ikiwa ni pamoja na kununua samaki wanaopatikana kwa sh. 5,000 ambao ndio mboga kubwa kutokana na kijiji hicho kuwa katika mazingira karibu na bahari na mchele ambao wananunua sh. 2,200.
“Mahitaji mengine ambayo nalazimika kutumia pesa kila siku ni vocha kwa ajili ya mawasiliano (Hakutaja anatumia kiasi gani) pamoja na viungo kama nyanya, vitunguu na vingine, kwasababu samaki siwezi kupika bila viungo..” aliongeza.
Alisema, kutokana na kubanwa katika majukumu yao ya kufundisha, wanajikuta wanakosa hata muda wa kufanya shughuli nyingine ambazo labda zingeweza kuwapatia kipato mbadala tofauti na mshahara wao, huku akisema kuwa mpaka sasa anakabiliwa na deni la sh. 126,000.

Moja ya nyumba za walimu katika shule ya msingi Mkubiru, halmashauri ya Mtwara vijijini ambayo hata hivyo mwalimu aliyekuwa akiishi amehamishwa kutokana na kuhofia usalama wake kutokana na ubovu wa nyumba.

Kwa upande wake, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hazzam Nambunga, alikiri kukumbwa na changamoto hizo na kusema kuwa nyumba za walimu zilizopo ni mbili ambazo moja anaishi mwalimu mkuu na nyingine anaishi mwalimu mwingine mmoja.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkubiru, halmashauri ya Mtwara vijijini, Hazam Nambunga, akielezea changamoto alizonazo shuleni kwake.

Aidha, alisema, shule hiyo nakabiliwa pia ukosefu wa ofisi ya waalimu ambapo ambayo ilikuwa ikitumika jingo lake lipo katika hali mbaya na halifai kutumika tena kiasi cha kulazimika kutumia darasa moja kama ofisi ya waalimu na kwamba wanafunzi wa darasa la awali ambao walikuwa wakisomea katika chumba hicho kusomea chini ya miti.
“Tunamwomba Mhe. Rais wa awamu ya tano, pamoja na mambo mengine, aangalie sana na kuboresha masilahi ya walimu zaidi kuboresha miundombinu kwa kutujengea nyumba bora za walimu” alisema.


No comments: