Sunday, December 13, 2015

MRENGO yawajengea uwezo vijana Mtwara juu ya uwekezaji wa Mafuta na Gesi.


Vijana kutoka vyuo mbalimbali mkoani Mtwara walioudhuria semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo juu ya masuala ya uwekezaji katika sekta ya rasilimali za Mafuta na Gesi yanayoendelea mkoani hapa.




Vijana wakifuatilia somo kutoka kwa mwezeshaji Justin Lusasi, Mhadhiri wa chuo cha Stella Maris-Mtwara

Na Juma Mohamed, Mtwara.

ZAIDI ya vijana 30 kutoka katika vyuo mbalimbali mkoani hapa wamepatiwa elimu juu ya masuala ya uwekeza katika rasilimali za Mafuta na Gesi asilia, katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la MRENGO kwa lengo la kuwajengea uwezo wa uelewa katika masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo.
Wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo, baadhi ya wanafunzi hao walisema imewasaidia kuweza kufahamu mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na namna rasilimali hizo zitakavyoanza kuwanufaisha wananchi ambao wengi wao wanatarajia kuona mafanikio kwa siku za karibuni.
Mshamu Nayopa, muhitimu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) tawi la Mtwara, alisema awali alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakitarajia kuona faida ya rasilimali hizo zikianza kuonekana mapema, lakini baada ya kupata elimu kupitia semina hiyo amepata ufahamu kuwa itachukua muda mrefu mpaka wananchi kuanza kuziona faida zake.
“Mtaani kulikua na mitazamo mingi kwa vijana, lakini baada ya kuja kupata mafunzo tumegundua mambo yapo tofauti sana, vijana wengi wanatarajia mambo mengi sana wanavyosikia ‘Issue’ ya gesi, kwamba gesi itawezesha maisha yao na kufanya kila kitu, kitu ambacho sidhani kama ni kweli..kwamujibu wa elimu ambayo tumeipata hapa ni sawa gesi italeta mafanikio kwa wananchi lakini itachukua muda mrefu sana tofauti na watu wanavyotarajia..” alisema.
Aliwataka vijana ambao wako mitaani, kuacha kuishi kwa kutojishughulisha na kutegemea gesi itawasaidia kwasasa, na baadala yake wajishughulishe na mambo mbalimbali ambayo yatawawezesha kupiga hatua kimaisha.
Kwa upande wake, mratibu wa mradi wa Mafuta na Gesi unaotekelezwa na shirika hilo kwa kufadhiliwa na shirika la Utunzaji wa Mazingira Duniani (WWF), Mustafa Kwiyunga, alisema lengo la kuwajengea uwezo vijana hao ni kutaka kuendeleza majadiliano mbalimbali hasa katika vyuo na pia waende kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu juu ya rasilimali hizo kwa wananchi.

Vijana wakifuatilia somo kutoka kwa mwezeshaji Justin Lusasi, Mhadhiri wa chuo cha Stella Maris-Mtwara



“Wamalizapo wawe mabalozi wazuri kule chini kuwza kuwaelimisha wananchi waweze kuwahamasisha watoto wao kupenda masomo ya sayansi ili waweze kupata ajira katika maeneo ya uchimbaji wa mafuta na gesi..lakini pia jukwaa hili tunalitengeneza kwa ajili ya kwenda kukutana katika vyuo na pia tutakua na ratiba ya kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kujua kinachoendelea na kupashana habari mbalimbali kuhusu mafuta na gesi..” alisema.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris (STEMMUCO) mkoani Mtwara, Justin Lusasi, aliwataka wazizi na walezi kuhamasika katika kuwapeleka shule watoto wao kwa ajili kuwatengenezea misingi bora ya maisha ambayo wataipata kupitia rasilimali hizo, na waache kupoteza muda katika masuala ya Jando na Unyago.


No comments: