Waamuzi wakiwaongoza wachezaji wa timu za Ndanda na Stand Utd kuelekea uwanjani tayari kwa kuanza mchezo wa ligi kuu katika uwanja wa Nangwanda Sijaona juzi mkoani Mtwara. |
Kiungo wa Stand Utd, Jackob Masawe, akimtoka mshambuliaji wa Ndanda Fc, Thomas Morris wakati wa mchezo wa ligi kuu juzi katika uwanja wa Nangwanda, Mtwara. Timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0 |
Mshambuliaji wa Ndanda Fc, Atupele Green, akijaribu kumtoka mlinzi wa Stand Utd, katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara juzi katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. |
Baadhi ya watazamaji waliojitokeza katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara juzi kushuhudia mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara, kati ya Ndanda na Stand Utd. |
Baadhi ya watazamaji waliojitokeza katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara juzi kushuhudia mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara, kati ya Ndanda na Stand Utd. |
Na Juma
Mohamed.
CHAMA cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), kimelalamikia mapato finyu
yanayopatikana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani hapa, yanayotokana na
michezo mbalimbali ya ligi kuu ya Tanzania Bara inayoihusisha timu ya soka ya
Ndanda Fc.
Akizungumza
leo ofisini kwake, katibu wa chama hicho, Charles George, alisema uchache huo
wa mapato unatokana na idadi ndogo ya watazamaji wanaoingia uwanjani wakati
timu ya Ndanda inacheza hasa na timu ambazo hazina majina makubwa kama ilivyo
kwa Simba, Yanga na Azam.
Alisema,
MTWAREFA inajikuta ikiingia katika madeni na baadhi ya wadau na taasisi kadhaa
kutokana na ukosefu wa mapato, ambapo hadi sasa ni zaidi ya sh. 500,000 wanadaiwa
kwa kukosa fedha katika mechi za Ndanda dhidi ya Toto Africans, Azam na Stand
Utd.
“Sisi kama
Mtwarefa kwakweli tunapata wakati mgumu sana kuweza kukamilisha taratibu zote
za maandalizi ya mchezo, tunafanya kazi kwa kusuasua kwakweli, hata hizi asilimia
8 za mchezo ambazo tunapata ni hela ndogo sana kiasi kwamba tunashindwa kulipa..kwasababu
katika gharama za mchezo, inatakiwa ulipe polisi, huduma ya kwanza, gari la
wagonjwa, waokota mipira, wauzaji na wakaguzi wa tiketi na vituo vya kuuzia
tiketi..” alisema.
Alisema,
katika madeni wanayodaiwa hadi sasa kutokana na gharama za michezo kuanzia mchezo
wa Ndanda na Toto Agricans na Azam na Stand Utd ni zaidi ya sh. 500,000 ambapo
katika mchezo dhidi ya Toto deni lilikuwa ni sh. 282,000 huku mchezo wa juzi
dhidi ya Stand wanadaiwa sh. 242,000.
“Tutapata
wapi hatujui, lakini hawa watu walifanya kazi walionekana na sisi tunakubali
kama tuliwaandaa kwa ajili ya kufanya shughuli ya maandalizi ya mchezo, kwahiyo
lazima tutafute fedha za kuwalipa, lakini tutawalipa lini hiyo tutaangalia kadri
ya uwezekano utakavyokuwa..” alisema.
Aidha,
katibu huyo amekiri kuwa na changamoto ya kukosa vyanzo mbadala vya mapato
tofauti na kutegemea mapato ya mlangoni, na kwamba chama kinajitahidi kupitia
vikao vyao kuandaa vyanzo vingine vitakavyosaidia kupata fedha nje ya
viingilio.
Aidha,
akizungumzia mapato yaliyopatikana katika michezo miwili iliyopita kati ya
Ndanda na Azam, na ule wa Ndanda na Stand, alisema michezo hiyo jumla iliingiza
kiasi cha sh. Milioni 6.9.
Ndanda na
Azam uliingiza sh. 5,041,000 ambapo klabu mwenyeji ambayo ni Ndanda ilipata sh.
1,192,000 huku Azam wakiambulia kiasi
cha sh. 851,000, na kwamba katika mchezo wa juzi dhidi ya Stand timu hizo
ziliingiza kiasi cha sh. Milioni 1.9 huku klabu mwenyeji ikipata sh. 359,000 na
wageni walipata sh. 256,000.
Wakati huo
huo, Mtwarefa iliwataka makatibu wa vyama vya soka vya wilaya zote kuwasilisha taarifa
zao za ligi za wilaya ikiwa ni pamoja na idadi ya timu shiriki, msimamo na
mabingwa mapema ambapo mpaka kufikia Novemba 5 mwaka huu wawe wameshawasilisha.
“Taarifa za
simu sio sahihi, walete kwa maandishi, mwisho tarehe 5 saa 10 jioni, wilaya
yeyote ambayo haitoleta ‘ripoti’ ya ligi ya wilaya ifikapo saa 10:01 siku hiyo
hatuwezi kuipanga kwenye ratiba ya ligi ya mkoa.
Alisema,
kwamujibu wa kalnda, ligi ya mkoa ilitakiwa iwe tayari imeshaanza kama ilivyo
katika mikoa mingine, lakini imechelewa kutokana na wilaya zote kuwa bado
hazijawasilisha taarifa zake za ligi zao.
“Wanitumie
haraka iwezekanavyo ili kamati ya utendaji ikianzia katika kamati ya ligi ya
mkoa iweze kukaa hara na kupitia hizo taarifa kwa ajili ya kuanza kuchezesha
hiyo ligi ya mkoa..” aliongeza.
No comments:
Post a Comment