Friday, April 3, 2015

NDANDA YAKABILIWA NA MADENI

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhwqJDeiyXYJojatgG8zifSIBDDb9yqnd9Ukvc30AgJ09LAtx1qOcObhcBxMQseb8fKazL7hwgfnA7ctmC7PW2JVLN6G1aiYW3Vx8PCTwWXQoN78ftSyXa6QR5bDcCqSCmXM9bmvNYXTOk/s1600/IMG-20140913-WA0029.jpg

Na Juma Mohamed, Mtwara.
Wadau wa soka na wananchi wa mkoa wa Mtwara kwa ujumla wametakiwa kuisaidia timu ya Ndanda Fc inayokabiliwa hali ngumu ya kiuchumi ili kuinusuru na madeni inayodaiwa kwa sasa.
Wito huo umetolewa hii leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Hawa A. Ghasia wakati alipotembelea kambi ya timu hiyo na kukabidhi posho ya wiki tatu kwa wachezaji.


Hawa A. Ghasia, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi posho kwa timu ya Ndanda



Athumani Kambi na Mhe. Waziri
Huo ni utaratibu wa Waziri huyo ambae aliahidi kuisaidia timu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara, kuwa atakuwa anatoa posho kwa wachezaji kila wiki kiasi cha sh. Milioni 1.2, mpaka ligi itakapomalizika mwezi mei mwaka huu.
 “Kwanza mimi nimesoma Ndanda sekondari, kidato cha kwanza mpaka cha sita..kwahiyo naweza nikasema kwamba Ndanda ninapoiona naona kama niko shuleni kwangu, kwahiyo niliamua kujitoa kama mimi kwamba lazima nitoe kamchango kangu..sio kama nina uwezo ila najibana natafuta na nawasaidia.” Alisema Waziri.


Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoani Mtwara (MTWRAEFA) Athumani Kambi, akipokea posho za wachezaji


Alisema amekuwa akipata malalamiko kutoka kwa viongozi wa timu hiyo kuhusu ukata walionao kiasi cha kuchangishana pesa za kuiokoa timu kutatua baadhi ya mahitaji kambini, na kumfanya ajisikie aibu kwa niaba ya wanamtwara wote.


Nahodha wa Ndanda, Wilbert Mweta akitoa shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake kwa Mhe. Waziri, kwa msaada waliopewa.

 Naye Nahodha wa timu hiyo, Wilbert Mweta, pichani hapo juu ametoa shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake kutokana na kupokea msaada huo, lakini akisisitiza kuomba kusaidiwa zaidi kutokana na madeni yanayoikabili kambi ya timu ambayo inakadiriwa sio chini ya sh. Milioni 4, pamoja na hali ngumu ya chakula.
Mweta alimtoa hofu Waziri, ambae amekuwa ni kama mlezi wa timu kwa sasa, kwa kumuhakikishia kwamba timu haitashuka daraja na mikakati yao ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo iliyosalia wakianza na mchezo wa kesho dhidi ya Mbeya City na ule wa wiki ijayo dhidi ya Tanzania Prisons.
Timu hiyo inateremka dimbani kesho Aprili 4, kuwakabili Mbeya City ya mkoani Mbeya, katika mchazo ambao ni muhimu na mgumu kutokana na timu hizo kupishana alama moja Ndanda ikiwa na alama 23 wakati wapinzani wao wakiwa mbele kwa alama moja.

………………………mwisho………………………………………………………………………..

No comments: