Na Juma Mohamed, Mtwara.
Timu ya soka
ya Ndanda Fc ya Mkoani Mtwara imeendelea kupata matokeo yasiyoridhisha katika
uwanja wake wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona, baada ya hapo jana kujikuta
wakibanwa mbavu na Stand United ya Shinyanga na kulazimishwa sare ya kufungana
goli 1-1, katika mchezo wao wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
bara.
Ndanda
waliuanza mchezo huo taratibu kama kawaida yao huku wakiwasoma wapinzani wao
ambao walionekana kucheza kwa kasi kutafuta goli la mapema ambalo walifanikiwa
kulipata kunako dakika ya tisa mfungaji akiwa ni Chidiebele Abasilim, baada ya
uzembe uliofanywa na walinzi wa Ndanda kwa kushindwa kumzuia mfungaji wakijua
atakuwa ameotea ndipo alipomlamba chenga golikipa na kuukwamisha mpira kimiani.
Baada ya
hapo Ndanda walijaribu kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Stand wakitaka
kusawazisha lakini ilishindikana na kujikuta wanakwenda mapumziko wakiwa nyuma
kwa goli hilo moja.
Baada ya
mwamuzi Michael Magori aliyekuwa akichezesha mchezo huo akisaidiwa na Omari
Kambangwa na Kasimu Mpanga, kupuliza filimbi ya kuanza kipindi cha pili,
iliwachukuwa dakika nane tu Ndanda kusawazisha goli lililofungwa na Nassoro
Kapama akiwazidi ujanja walinzi wa Stand United.
Ndanda walionekana
kucheza kwa kasi na kuutawala mchezo kipindi cha pili ambapo walifika mara
kadhaa langoni mwa wapinzani wao lakini mashambulizi yao yaliishia mikononi mwa
golikipa Mohamed Makaka wa Stand United na mengine kuokolewa na walinzi huku
shuti moja likigonga mwamba na kutoka nje.
Timu zote
mbili zilijaribu kufanya mabadiliko, Nanda waliwatoa Masoud Ally, Gideon Benson
na Kiggi Makasi na nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahim Mwaipopo, Saidi Issa na
Rajabu Isihaka, huku Stand United wakiwatoa Mathias Thabit, Hery Mohamed na
Hamis Shengo na nafasi zao zikachukuliwa na Abou Ubwa, Danny Manyenye na Shabani
Kondo, lakini licha ya mabidiliko hayo y timu zote mbili, mchezo huo mpaka
dakika 90 zinamalizika matokeo yalibaki kuwa goli 1-1.
Baada ya
mchezo kumalizika, makocha wa timu zote mbili walizungumza, kwa upande wa kocha
wa Stand United, Mathias Lole, alisema mchezo ulikuwa mzuri na akisifu pia
waamuzi kuchezesha vizuri. “kwa mara yangu ya kwanza, naona waamuzi
wakichezesha vizuri sana..kwa upande wa Ndanda walikuwa vizuri, walikuwa na ‘sistimu’
mzuri..tulifunga kwanza wao wakaja wakasawazisha, ila kiujumla mchezo ulikuwa
mzuri.” Alisema Lole.
Aliongeza
kuwa “kupoteza nafasi ni kawaida na kila mtu anaweza kupoteza nafasi, kwakuwa
mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo wa makosa.” Alisema.
Akizungumzia
mabadiliko yao ya mwisho waliyoyafanya katika dakika nne za nyongeza ambapo
mchezaji aliyetakiwa kutoka alikuwa ni Reina Mgungira mwenye jezi nambari 16,
lakini akajifanya hajui kama yeye ndio anaetakiwa kutoka licha ya kibao cha
mwamuzi wa mezani kuonesha kuwa yeye ndio anaetakiwa kutoka, baadala yake wakalazimisha
atoke Hamisi Shengo mwenye jezi nambari 28, na ilichukuwa karibu dakika moja na
nusu mpaka Shengo kutoka uwanjani, Lole alisema hiyo ilikuwa ni mbinu tu ya
mchezo “yalikuwa ni maandalizi tu yakiufundi ambayo tuliyaandaa..na
tulilazimika kufanya vile kwakuwa presha ilikuwa kubwa.” Aliongeza Lole.
Aidha kwa
upande wake Kocha wa Ndanda Fc Meja Mstaafu Abdul O. Mingange, alisema mechi
ilikuwa ni ngumu sana kwa upande wao na kwamba ni bora hata ucheze na Yanga au
Simba. “ni mechi ngumu..lakini na madharau tu ya wachezaji wangu kama
ulivyoona, wachezaji wanadharau mechi wanaona kama ni timu ndogo..na hili ni
tatizo la wachezaji wa Tanzania, hawaelewi na hawajui umuhimu wa kucheza ligi
nyumbani na ugenini.” Alisema Mingange.
Kuhusu
mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha wanayoyapata katika uwanja wa nyumbani,
kocha huyo alisema haoni kama ni matokeo mabaya sana, kwasababu amepata pointi
moja katika mchezo huo na walishawahi kushinda huko nyuma katika mechi dhidi ya
Azam.
Kwa upande
wa mashabiki wa Ndanda Fc wameonesha kutofurahishwa na matokeo ambayo timu yao
inayapata katika uwanja huo na kuyaita matokeo ya aibu na hayafai kuyapata
katika uwanja wa nyumbani.
“Mimi
namuomba kocha wangu ajipange, aiandae vizuri timu ili tufanye vizuri katika
mechi zijazo kwasababu hapa ni nyumbani..kwa matokeo tunayoyapata hapa kwakweli
ni aibu, tatizo labda ni wachezaji wetu wakiwa hapa ‘hawakazi’ tofauti na
ugenini au labda kuna vitu vingine ambavyo havijulikani havijioneshi ndani
nyake..mimi nahisi tu labda ni u-siasa siasa tu labda unaingia.” Alisema
shabiki mmoja wa Ndanda aliejitambulisha kwa jina moja la Nurudini.
Aliongeza
kuwa “labda ushindani tu wa wanasiasa, kwasababu hapa inasemekana kuna
ushindani wa wanasiasa wawili maana mara ya kwanza mmoja alikuwa anaimiliki
timu ambaye ni mheshimiwa Mbunge (Asnain Murji) na mara ya pili kuna Mbunge
mwingine anaisaidia timu (Hawa A. Ghasia), sasa labda ni hao..wote wanaisaidia
timu ila naona kama kuna mvutano..sasa kama tatizo ni hao basi tunawaomba
wajirekebishe kwakweli, kwasababu kila tukija hapa tunaambulia matokeo ya sare
au kufungwa, mashabiki inatuumiza kwakweli.” Alisema Nurudini.
Mtandao huu unafahamu kuwa awali Mbunge wa Mtwara Mjini Asnain Murji alikuwa anaisaidia
Ndanda Fc kwa kutoa mabasi yake kuwasafirisha mashabiki kwenda kuishangilia
timu pindi inapokwenda kucheza ugenini lakini kwa sasa huduma hiyo ameisitisha
japo haijafahamika sababu za msingi za kufanya hivyo. Pia Mtandao huu unafahamu
kuwa timu hiyo kwa sasa inasaidiwa na Mbunge wa Mtwara Vijijini na Waziri wa
Tamisemi, Mhe. Hawa A. Ghasia ambae anatoa posho kwa wachezaji kila wiki kiasi
cha sh. Milioni 1.2. Tunaahidi kulifuatilia kwa kina suala hili la u-siasa
unaotajwa kuingia ndani ya timu ya Ndanda na kuwasababishia kupata matokeo
yasiyoridhisha katika uwanja wa nyumbani.
Kiuhalisia,
timu ya Ndanda haijapata matokeo yakuridhisha katika mechi zake zote ambazo
imecheza katika uwanja wa nyumbani wa Nangwanda Sijaona isipokuwa mechi moja
pekee waliocheza Novemba 01, mwaka jana dhidi ya Azam na kushinda goli 1-0.
Mechi ya
jana dhidi ya Stand United ilikuwa ni mechi yao ya 14 katika mechi zote za Ligi
Kuu walizocheza msimu huu, na kati ya hizo mechi sita wamecheza nyumbani na
kushinda moja tu dhidi ya Azam, mechi tatu wamefungwa ambazo ni dhidi ya Ruvu
Shooting 3-1, JKT Mgambo 1-0 na Simba 2-0. Mechi walizotoa sare ni mbili,
ambazo ni dhidi ya Polisi Moro 1-1 na Stand United 1-1.
Katika
mchezo wa jana Ndanda waliwakilishwa na Wilbert Mweta, Azizi Sibo, Paul
Ngalema, Kasian Ponera, Hemed Khoja, Omega Seme, Jacob Masawe, Masou Ally,
Nassoro Kapama, Gideon Benson na Kiggi Makasi.
Stand United
walikuwa, Mohamed Makaka, Revocatus Richard, Yasin Mustapha, Iddy Mobby, Peter
Mutabuzi, Reina Mgungira, Hanuna Chanongo, Hamisi Thabit, Chidiebele Abasilim,
Hery Mohamed na Hamis Shengo.
............................................mwisho...............................................................
No comments:
Post a Comment