Na Juma
Mohamed, Mtwara.
Shirika la
Hifadhi ya Jamii (PPF) limekabidhi msaada wa vyakula vyenye thamani ya shilingi
milioni 5, kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kwa lengo la kuwasaidia
waathirika wa mafuriko.
Ofisa Huduma
kwa Wateja Kanda ya Kusini, Liliani John Mhina amesema vyakula walivyokabidhi
ni Unga, Maharage na Mchele ambavyo vyote kwa ujumla vina thamani ya shilingi
milioni 5.
“Jumla ya
msaada wote tuliokabidhi ni tani tatu na nusu ambapo Unga ni mifuko 90, mchele
ni gunia 10 ambazo kila gunia moja lina kg 100 na maharage ni gunia nne ambazo
kila gunia moja lina kg 100.” Alisema Liliani.
Aidha kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara bwana Wilmani Ndile, baada ya kupokea
msaada huo alitoa shukrani zake kwa PPF na kusema kuwa waliamua kupeleka maombi
kutokana na kaya nyingi kuathirika na mafuriko na kuwasababishia kukosa chakula.
“Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ilipeleka taarifa ya kuomba msaada kutokana na mafuriko. PPF
walipokea na kulifanyia kazi, na ilichukuwa siku nne tu toka tupeleke maombi na
wao kuanza kuyafanyia kazi, kwahiyo Jumatatu tutapeleka barua rasmi ya kukiri
kupokea msaada. Na tulifanya hivyo baada ya kubaini kuwa waathirika wa chakula
ni wengi.” Alisema Ndile.
Ndile
aliongeza kuwa kaya zilizoathirika ni 900 na kwa mtu mmoja mmoja ni zaidi ya
wananchi elfu tatu (3,000) ambapo ameahidi kuwafikishia msaada huo walengwa.
“Tumepata
‘sapoti’ ya chakula kiasi cha tani 73.5 ambazo ni kama gunia 730 za mahindi
mpaka sasa ikiwa ni pamoja na kusafirishiwa, tumepewa fedha kiasi cha shilingi
milioni 36 za kununulia maharage kwa ajili ya chakula. Na wananchi wajue kwamba
kwanzia kesho (jana) tunaanza kugawa chakula” Aliongeza Ndile.
Akizungumzia
miundombinu ya Manispaa ya Mtwara, Ndile alisema bado wanasubiri msaada
mwingine kwa ajili ya kuboresha miundombinu kutoka kwa wahisani wengine ikiwa
ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu. Alisema kuhusu ujenzi wa mfereji mkubwa wa
maji uliopo kata ya Kiyanga, Manispaa ya Mtwara, ni kwamba wiki ijayo utakuwa
unakamilika na kwamba ni mradi mkubwa ambao una thamani ya shilingi 1 bilioni.
Manispaa ya
Mtwara ilikumbwa na mafuriko mwezi uliopita na kuathiri miundombinu ya mji,
pamoja na kaya zipatazo 900 ambapo ilipelekea wananchi kukosa baadhi ya
mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na chakula na malazi.
…………………………………….mwisho……………………………………………………
No comments:
Post a Comment