| John Mnyika |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, anatarajiwa kuzinduwa kanda ya kusini ya
chama hicho mkoani hapa Aprili 12 mwaka huu.
Akizungumza
na NEWS ROOM jana, Afisa wa chama hicho kanda ya kusini, Filbert Ngatunga,
alisema katika uzinduzi huo, Mnyika ataambatana na baadhi ya viongozi wengine
wa Kitaifa na kuungana na viongozi wa kimkoa na kanda, na wataanza na vikao vya
ndani Aprili 11 kabla ya kufanya mkutano wa hadhara utakaoanza saa nane mchana
katika viwanja vya mashujaa.
Mwanzo kanda
ya kusini ilikuwa inaundwa na mikoa mitatu ambayo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma
ambapo makao makuu yalikua mjini Songea, mkoani Ruvuma.
Alisema,
kutokana na maboresho yaliyofanywa na chama, waliamua mkoa wa Ruvuma
kuuhamishia katika nyanda za juu kusini ambapo umeungana na mikoa ya Njombe,
Mbeya, Iringa na Rukwa na kufanya kanda hiyo kuundwa na mikoa mitano.
“Kanda ya
kusini sasa itakuwa imebaki na mikoa ya Lindi na Mtwara, ambapo sasa viongozi
wengi wa hiyo kanda ya kusini walikuwa wanatoka mkoa wa Ruvuma..kwahiyo baada
ya kuuhamishia nyanda za juu kusini, tunatakiwa sasa tuunde uongzi mpya wa
kanda ambao utaweza kutuvusha kuanzia sasa mpaka kipindi cha uchaguzi utakapoisha.”
Alisema Ngatunga.
Akifafanua
zaidi alisema, kutokana na mfumo wa kanda kuwa haujakamilika katika katiba ya
chama, kamati kuu iliazimia na kuunda timu maalum zitakazoshughulikia masuala
ya chama kwa kipindi maalum, kwahiyo kanda hizo zimeundwa ikiwa bado
hazijawekwa katika mfumo wa kikatiba wa Chadema.
Aidha,
alisema kuanzia Ijumaa ya April 3 mwaka huu wataanza kufanya mikutano ya
hadhara katika kata mbali mbali za mtwara manispaa na mtwara vijijini na
wataanzia katika kata ya Railway, na ajenda zitakuwa ni kuwaelimisha wananchi
kuhusu katiba inayopendekezwa, kutoa elimu kuhusu daftari la mpiga kura na
changamoto zilizojitokeza katika zoezi la kujiandikisha katika daftari hilo
mkoani Njombe.
……………………………………mwisho………………………………………………………………
No comments:
Post a Comment