Friday, December 12, 2014

RUSHWA YAICHAFUA TANZANIA KIMATAIFA






Na Juma Mohamed, Mtwara.

Tanzania imeendelea kushuka kimataifa katika kupambana na Rushwa na Ufisadi kutoka nchi ya 111 hadi kufikia kuwa nafasi ya 119 kidunia.

Hayo yaliezwa na Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Saint Agustine University of Tanzania (SAUT), tawi la Mtwara Dr. Aidani Msafiri, wakati akitoa mada katika maadhimisho ya siku ya Maadili kitaifa yaliyofanyika Dedesemba 10, mwaka huu katika viwanja vya Mashujaa hapa mkoani Mtwara.

Dr. Msafiri aliyetoa mada iliyosema kuwa “Uhuru na Maadili kama nguzo kuu za ustawi na amani kwa Watanzania wote,” alisema kuwa sakata la Novemba mwaka huu la Tegeta Escrow ni kielelezo bayana cha hulka na utamaduni wa rushwa kubwa hapa nchini. “Malumbano ya wabunge hasa katika kuwatetea wezi na watuhumiwa wakuu katika sakata hilo ni kiashiria bayana cha saratani ya kansa, ambayo imeshawakumba viongozi waandamizi wa serikali na vyama mbalimbali katika nchi yetu.”Alisema Dr. Msafiri.

Kwa upandewake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambae ndiye aliekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Ponsiano Nyami, alisema kuwa mwaka 2005 serikali ya Tanzania iliamua kwa makusudi kuwa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kupambana na rushwa nchini yatakuwa yanafanyika tarehe 10 Desemba, ambapo mwanzo yalikuwa yakifanyika tarehe 9 Desemba ambayo ni siku ya Uhuru.

“Nawaombeni kila mwaka, basi sisi sote hapa tujitokeze kwa wingi pamoja na wananchi wengine. Kimantiki siku hii ni maalumu kwa serikali na jamii ya Watanzania yani kuthamini alafu kutathmini nini ambacho tumekifanya, nini tunafanya na nini tutafanya ili kuhakikisha tunaimarisha, kuendeleza na kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa.” Alisema Nyami.

Aidha aliongeza kuwa, serikali inajitahidi kila siku kuimarisha Takukuru, dawati la maadili katika jeshi la polisi, ulinzi shirikishi na mambo mengine mengi ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa. “Ukienda polisi ni wazi, maana katika bwawa la samaki kuna viluilui vidogvidogo..ndio hivyo vichache vinavyoweza kuliharibu jeshi la polisi, serikali na mahakama pia, sasa hivyo viluilui ndivyo viondolewe ili visizidi kuichafua serikali.” Aliongeza Nyami.

Nae Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Edson Atanasi Makailo, alizitaja athari ambazo nchi inaweza kukumbana nazo kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa kuwa ni pamoja na kupunguza ustawi wa demokrasia na kusababisha kupatikana kwa viongozi wasio faa, kushuka kwa uchumi wa taifa, kuongezeka kwa umasikini na kuathiri misingi ya utawala bora.

Umoja wa Mataifa nnamo Desemba 9, 2003, ulipitisha kuwepo kwa mapatano ya kupambana na rushwa kupitia tamko namba 58/04 la Oktoba 31, 2003 yaliyosainiwa na nchi wanacha wa umoja huo ikiwamo Tanzania huko nchini Mexico.



………………………………mwisho……………………………………….

No comments: