Monday, December 8, 2014

WAFANYAKAZI WA BANDARI WATAKIWA KUONGEZA UFANISI





Na Juma Mohamed, Mtwara.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA, wametakiwa kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, na kuto bweteka kwa kudhani kwamba mamlaka hiyo imefikia kiwango cha juu.

Hayo yamezungumzwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Ponsiano Nyami wakati akitoa Hotuba ya kufunga Michezo ya nane ya Bandari Inter-Ports Games, kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mwara.

“Ni vyema mkatambua kwamba TPA inakabiriwa na mahitaji makubwa ya kuboresha utendaji kazi wake, lakini bila kusahau maendeleo ya rasilimali watu wake”. Alisema Nyami.

Aliongeza kuwa, “kwa kuwa na michezo hii nawapongezeni hasa kwani inafufua ari ya kufanya kazi kwa bidii na kwa tija miongoni mwa wafanyakazi wenu”. Alisema.

Aidha, Nyami aliwasihi wote kulibaini suala la kuboresha utendaji kazi na mustakabali wa taasisi hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa, na jambo hilo liwe somo, hivyo waondoke nalo na kuwapelekea wenzao ambao hawakupata fursa ya kushiriki katika michezo hiyo.

“Mrudi katika vituo vyenu vya kazi mkiwa na hamasa, mkawahamasishe wenzenu ili matokeo ya kazi yenu ya msingi yawe ya ushindi kama ambavyo wote mmekuwa mkishindana kwa ari na kwa moyo dhabiti kabisa katika kusaka ushindi. Kama ilivyo katika michezo, na katika kazi tusioneane aibu, tupendane, turekebishane na kupongezana pale inapobidi.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utumishi wa TPA, Peter Gawile, alisema michezo hiyo ya nane imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kufikia malengo kama ilivyotarijiwa na wachezaji walionesha nidhamu na mshikamano.

Wanamichezo zaidi ya 400 walishiriki katika michezo hiyo ilioshirikisha timu za Bandari zote za Tanzania Bara.



………………………………..mwisho…………………………………………

No comments: