Tuesday, December 11, 2012

WACHEZAJI WA ZANZIBAR HEROES WAPORA MPUNGA WA CECAFA NA KUGAWANA WENYEWE

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar ' Zanzibar Heroes' wameingia katika kashfa nzito baada ya kudaiwa kumpora fedha Mkuu wa msafara kwa upande wa Chama cha Mpira wa Miguu Visiwani Zanzibar, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Kassim Haji Salum, ambaye aliambatana na kikosi cha Zanzibar Heroes kilichokuwa kikishiriki katika michuano ya chalenji iliyomalizika juzi jijini Kamapal, Uganda.

Inadaiwa kuwa fedha hizo ambazo ni dola 10,000 walizopewa Zanzibar baada ya kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo, wachezaji hao wlizikwapua kutoka kwa katibu huyo muda mfupi mara baada ya kuweka saini ya kukabidhiwa fedha hizo.

Akizungumza leo mara baada ya kuwasili visiwani Zanzibar, Nahodha wa Zanzibar Heroes, Nadir Haroub 'Canavaro' amekiri kuzichukua fedha hizo huku akisema ni haki yao wachezaji huku akitolea mfano kwa baaddhi ya timu kuwa wamefanya kama wao na haoni kama wamefanya kosa.

Wachezaji hao inadaiwa wamegawana dola 500 kila mchezaji.

Akizungumzia sakata hilo Mkuu wa Msafara kutoka Serikalini kupitia Baraza la Michezo la Taifa la Zanzibar, Mussa Abdulrabi Fadhil, amesema kwa sasa Serikali haiwezi kuzungumza chochote mpaka watakapokaa kikao na kulitolea ufafanuzi suala hilo, "Sisi kama Serikali ni kweli tumesikia suala hilo lakini kwa sasa hatuwezi kulizungumzia kwa sababu tumekubaliana tutakutana na baadae tutao ufafanuzi juu ya suala hilo" amesema Fadhil.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Salum Baus Nassor, amesema amepata taarifa hizo ingawa hana uhakika na hilo ila kama ni kweli amekitaka chama cha mpira wa miguu visiwani Zanzibar kuchukua hatua kali dhidi ya kitendo hicho cha utovu wa nidhamu kilichofanywa na wachezaji hao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ZFA Taifa, ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa chama hicho, Kassim Haji Salum, amekiri kupokonywa fedha hizo na kusema kikao cha kamati tendaji taifa ndio watakaoamua hatua zitakazochukuliwa dhidi ya kitendo hicho.

Akizungumza kwa hasira na kuahidi kuchukua hatua kali kwa viongozi wa kitendo ambao ni Nahodha wa Timu, Nadir Haroub 'Canavaro' na msaidizi wake Agrey Morris, Rais wa Chama cha Mpira wa miguu visiwani Zanzibar, (ZFA) Aman Ibrahim Makungu, amesema amesikitishwa na kitendo hicho kwa sababu yeye binafsi aliwasiliana na Canavaro kumsihi fedha wazirejeshe lakini akamjibu kuwa hawana imani na ZFA kwa madai kuwa wana kumbukumbu ya kutokupewa fedha zao.

Hata hivyo habari za ndani kabisa zinasema Serikali kupitia baraza la michezo la Zanzibar limewakataza kusema chochote viongozi walioondoka na timu kwa kutaka kuzuia sakata hilo kusambaa hususan kwa vyombo vya habari.

WAKATI HUO HUO: Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Zanzibar, Salum Bausi Nassor ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kwa madai ya kutekeleza ahadi aliyoiweka kuwa akishindwa kuchukua ubingwa anaachia ngazi.


SOURCE: SHAFFIH DAUDA

No comments: