Said Bahanuzi 'Spider Man', mshambuliaji mpya Stars |
Na Prince
Akbar
TIMU ya soka ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars Agosti 15 mwaka huu itapambana na Botswana ‘Zebras’ katika
mchezo maalumu wa Kalenda ya FIFA utakaofanyika jijini
Gaborone.
Tayari Kocha Kim Poulsen
alishatangaza kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Agosti 8 mwaka huu
tayari kwa mechi hiyo ya kirafiki ya kujipima
nguvu.
Wachezaji wote walioitwa Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambi
kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Agosti 8 mwaka huu saa 1 jioni tayari
kwa mazoezi yatakayoanza siku inayofuata.
Makipa walioitwa kwenye kikosi
hicho ni Deogratias Munishi (Azam), nahodha Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali
(Azam). Mabeki ni nahodha msaidizi Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam),
Kelvin Yondani (Yanga) na Shomari Kapombe
(Simba).
Viungo ni Athuman Idd (Yanga),
Frank Domayo (Yanga), Haruna Moshi (Simba), Mrisho Ngassa (Azam), Mwinyi
Kazimoto (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Ramadhan Singano (Simba), Salum
Abubakar (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco
(Azam), Mbwana Samatta (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Said
Bahanuzi (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
BINGWA BANCABC SUPER 8 KUPATA MILIONI 40
Azam FC; Itashiriki |
Na Prince
Akbar
BINGWA wa michuano ya BancABC
Super 8 inayoanza keshokutwa (Agosti 5 mwaka huu) katika miji ya Dar es Salaam,
Zanzibar, Mwanza na Arusha atapata sh. milioni 40 wakati makamu bingwa sh.
milioni 20. Pia timu mbili zitakazoishia hatua ya nusu fainali kila moja itapata
sh. milioni 15 wakati zilizobaki kila moja itapata sh. milioni
5.
Timu zimepangwa katika makundi
mawili ya A na B. Kundi A lina timu za Simba (mabingwa wa Tanzania Bara),
Jamhuri, Zimamoto na Mtende zote za Zanzibar. Kundi ni Super Falcon (mabingwa wa
Zanzibar), Azam, Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro zote za Tanzania
Bara.
Mechi za ufunguzi keshokutwa
(Agosti 5 mwaka huu) ni Simba vs Jamhuri (Dar es Salaam), Zimamoto vs Mtende
(Mwanza), Mtibwa Sugar vs Polisi Morogoro (Arusha) na Super Falcon vs Azam
(Zanzibar). Awali mashindano yalikuwa yaanze Agosti 4 mwaka huu lakini
yamesogezwa mbele kwa siku moja.
Hatua ya makundi itamalizika
Agosti 12 mwaka huu. Mechi za nusu fainali na fainali zote zitachezwa Dar es
Salaam. Nimeambatanisha ratiba.
Mdhamini bancABC atagharamia
usafiri wa ndege kwa timu zote kutoka kituo kimoja hadi kingine, malazi na jezi.
Yanga imejitokea kwenye mashindano hayo na nafasi yake imechukuliwa na Mtibwa
Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya Vodacom.
LIGI DARAJA LA KWANZA SASA TIMU 24
Na Prince
Akbar
LIGI Daraja la Kwanza Tanzania
Bara, (FDL) kuanzia msimu huu wa 2012/2013 itakuwa na timu 24 kutokana na
mabadiliko ya mfumo wa mashindano yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF).
Kamati ya Utendaji ya TFF
ilikutana Julai 29 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilifanya mabadiliko
ya mfumo wa mashindano ikiwemo FDL kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini
badala ya ule wa awali wa vituo.
Kutokana na mabadiliko hayo,
timu za FDL zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 12 kila moja kutokana na
ukaribu wa kanda na kucheza kwa mtindo wa nyumbani na
ugenini.
Timu ya kwanza kutoka kila
kundi itapanda kucheza Ligi Kuu msimu unaofuata wakati ya tatu itakayoungana na
hizo mbili itapatikana kwa mechi za nyumbani na ugenini kwa timu zilizoshika
nafasi ya pili katika kila kundi.
Ili kufikisha idadi ya timu 24
kwenye FDL, Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya
Mashindano imeamua timu tatu za juu kwenye Ligi ya Taifa kutoka vituo vyote
vitatu vya ligi hiyo zimepanda daraja.
Sasa timu 24 za FDL ni Ashanti
United (Dar es Salaam), Burkina Moro (Morogoro), Green Warriors (Dar es Salaam),
Kanembwa JKT (Kigoma), Kurugenzi Mafinga (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mbeya City
(Mbeya), Mkamba Rangers (Morogoro), Mlale JKT (Ruvuma) na Morani
(Manyara).
Nyingine ni Moro United (Dar
es Salaam), Mwadui (Shinyanga), Ndanda (Mtwara), Pamba (Mwanza), Polisi
(Arusha), Polisi (Dodoma), Polisi (Iringa), Polisi (Mara), Polisi (Tabora),
Rhino Rangers (Tabora), Small Kids (Rukwa), Tessema (Dar es Salaam), Transit
Camp (Dar es Salaam), Villa Squad (Dar es Salaam)
Timu nne zitashuka daraja
kurudi Ligi ya Mkoa. Timu hizo ni mbili zilizoshika nafasi za mwisho kwa kila
kundi. Timu nne zitakazopanda kucheza FDL zitapatikana kwa mchujo utakaohusisha
mabingwa wa mikoa.
Kwa mfumo huo mpya wa
mashindano, ligi za mikoa zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa zinatakiwa kuwa na timu zisizopungua 16 na zisizozidi 20. Ligi
za mikoa pia zitachezwa mwaka mzima kwa mikondo miwili (nyumbani na
ugenini).
Ligi ya mkoa itashusha timu
mbili na kupandisha nyingine mbili kutoka ligi ya wilaya. Ligi za wilaya
zitakazosimamiwa na kuendeshwa na vyama vya mpira wa miguu vya wilaya zinatakiwa
kuwa na timu zisizopungua 10 na zisizozidi 20.
Kwa wilaya zenye timu zaidi ya
20, chama husika cha mpira wa miguu kitapanga utaratibu wa kuzichuja kwa
mashindano ili kupata zile bora 20 zitakazocheza ligi rasmi ya
wilaya.
Mabingwa wa wilaya katika mkoa
husika watacheza mechi za kuchujana (play offs) ili kupata timu mbili
zitakazopanda daraja kucheza ligi ya mkoa husika.
Kutokana na mabadiliko hayo ya
mfumo wa mashindano, sasa madaraja rasmi ya ligi ni Ligi Kuu, Ligi Daraja la
Kwanza, Ligi ya Mkoa (Ligi Daraja la Tatu) na Ligi ya Wilaya (Ligi Daraja la
Nne).
TFF inasisitiza kuwa kwa
mujibu wa kalenda yake ya matukio, kipindi cha usajili wa wachezaji kwa madaraja
yote ni kimoja, na ligi zitachezwa kwa wakati
mmoja.
Usajili wa hatua ya kwanza ni
kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu wakati kipindi cha pili cha usajili ni
Agosti 21 hadi Septemba 4 mwaka huu. Usajili wa dirisha dogo ni Novemba 15 hadi
Desemba 15 mwaka huu.
Ligi kwa madaraja yote
zitaanza Septemba. Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, Ligi Daraja la
Kwanza ni Septemba 15 mwaka huu, Ligi ya Mkoa na ile ya Wilaya zenyewe zitaanza
Septemba 8 mwaka huu.
Mechi za kufungua msimu kwa
madaraja yote (Ngao ya Jamii) ambazo kwa sasa zinakutanisha bingwa na makamu
bingwa zitachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati michuano ya Kombe la FA itaanzia
wilayani Septemba 24 mwaka huu.
FIFA yamuita darasani Nsajigwa
Nsajigwa |
Na Princess
Asia
NAHODHA wa zamani wa timu ya
soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele, ni
miongoni mwa wadau wanaotarajiwa kushiriki Kozi ya Uongozi na Utawala ya
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) itafanyika katika ukumbi wa Msimbazi
Center, Dar es Salaam kuanzia Agosti 6-11 mwaka huu ikiwa na washiriki
30.
Kwa ujumla, washiriki wa kozi
hiyo itakayonedeshwa na wakufunzi kutoka FIFA ni viongozi kutoka TFF, Chama cha
Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, klabu za Ligi
Kuu na viongozi wa mpira wa miguu wa
wanawake.
Walioteuliwa kushiriki ni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, Rais wa ZFA Amani Makungu,
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF; Ahmed Mgoyi, Blassy Kiondo, Stanley
Lugenge, Khalid Abdallah, Hussein Mwamba na Eliud
Mvella.
Wengine ni Katibu Mkuu wa ZFA,
Kassim Salum, Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai, wenyeviti wa vyama vya mpira
wa miguu vya mikoa ya Kagera (Jamal Malinzi), Dodoma (Nassoro Kipenzi) na Pascal
Kihanga (Morogoro).
Makatibu wa vyama vya soka vya
mikoa ya Mara (Mugisha Galibona), Mtwara (Vincent Majiri), Morogoro (Hamisi
Semka), Kagera (Salum Chama), Tanga (Beatrice Mgaya) na Dodoma (Stuart Masima).
Pia yumo Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Hilal na Makamu Mwenyekiti wa Yanga,
Clement Sanga.
Washiriki wengine ni Katibu
Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni, Ofisa Habari,
Boniface Wambura, Mkurugenzi wa Masoko na Matukio, Jimmy Kabwe, Mkurugenzi wa
Mashindano, Saad Kawemba, Ofisa Sheria wa TFF, Neema Lucumay, Ofisa wa Mpira wa
Miguu wa Wanawake, Grace Buretha, Amina Karuma (Mpira wa miguu wa wanawake) na
nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa.
No comments:
Post a Comment