Sunday, August 26, 2012

KOCHA BARCELONA ASEMA PIGA UA, ALEX SONG LAZIMA ACHEZE LEO

 

Kocha wa Barcelona, Tito Vilanova amemjumuisha Alex Song katika kikosi cha timu yake kitakachocheza ugenini leo katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Osasuna itakayoanza saa 2:00 usiku.

Song alijiunga na Barcelona wiki iliyopita akitokea Arsenal, lakini Vilanova amesema kuwa kiungo wake huyo wa kimataifa kutoka Cameroon ameonyesha kiwango cha juu mazoezini na hivyo anastahili kuwemo katika kikosi chake cha leo.

"Amekuwa na siku chache sana za kufanya mazoezi na sisi, lakini tulikuwa na muda wa kutosha kumuonyesha aina mbalimbali za uchezaji wetu... atacheza katika nafasi ya beki wa kati (Na.5) au kiungo (mkabaji)," amesema Vilanova.

"Ameonyesha kiwango kizuri sana mazoezini-- anatoka katika klabu inayofanya mazoezi yanayofanana na yetu na kujaribu kukaa na mpira," ameongeza Vilanova.

Song alitua Barca kwa ada ya uhamisho ya paundi za England milioni 15 (Sh. bilioni 37)
ERIC ABIDAL AANZA KUJIFUA ILI APIGANIE NAMBA YAKE BARCELONA
Eric Abidal anavyoonekana katika siku ya utambulisho rasmi wa kikosi cha Barca 2012-13.
Abidal akijifua
Eric Abidal... hapa pia akijifua
Eric Abidal akisoma Qur-an ndani ya ndege wakati yeye na wachezaji wenzake wa Ufaransa wakiwa safarini.
'Jembe' Eric Abidal... hapa anaomba dua kabla ya kuanza kwa mechi mojawapo ya timu yake ya Barca. Hapa ni kabla ya kupata matatizo ya ini na kufanyiwa upasuaji uliomabatana na kuwekewa ini jingine alilomegewa na binamu yake.
Nakuombea 'jembe' letu Eric Abidal upone haraka... Lionel Messi akiwa na fulana yenye ujumbe wa kumtakia kheri Abidal.
Abidal (wa tatu kutoka kulia)akiwa na wenzake wa kikosi kipya cha Barca 2012-13
BARCELONA, Hispania
Beki wa Barcelona, Eric Abidal ametangaza kuanza kujifua vikali kwa mazoezi binafsiwakati akiendelea kujiweka fiti baada ya kuendelea vizuri kiafya kufuatia upasuaji uliofanikiwa wa kumpandikizia ini jingine mwilini .

Mchezaji huyo wa kimataifa kutoka Ufaransa alifanyiowa upasuaji Aprili, na kulikuwa na hofu kwamba beki huyo wa kushoto asingerudi tena uwanjani.

Hata hivyo, Abidal amepania kucheza tena soka, na sasa ameanza kujifua vikali katika "gym" ya klabu yao na pia kufanya mazoezi binafsi akiwa mbali na wenzake wa kikosi cha kwanza.

"Enyi ndugu na marafiki zangu, natumai kwamba nyote ni wazima, nawaandikia ili kuwapa habari njema: Nimeanza tena kufanya mazoezi ya ndani, kwa siku kadhaa sasa," taarifa kupitia ukurasa wa mtandao wake rasmi wa kijamii wa Facebook ilisomeka.

Beki huyo mwenye miaka 32 alikaribishwa kwa kushangiliwa sana Jumatatu wakati wa kutambulishwa rasmi kwa kikosi cha Barcelona kabla ya mechi yao ya kirafiki ya kuwania Kombe la Joan Gamper dhidi ya Sampdoria, na Abidal alifurahishwa na upendo ulioonyeshwa kwake na mashabiki.

"Na ninapenda kuwashukuru sana wana Catalans (mashabiki wa Barca) kwa kunipokea vizuri sana kwenye Uwanja wa Camp Nou wakati wa utambulisho wetu rasmi! Nawashukuru kwa kuniunga mkono."

Katika taarifa nyingine, Eric Abidal ambaye ni muumini wa dini ya Kiislamu alieleza namna anavyomshukuru Mungu kwa kuendelea kumpa uzima, akisema: "Allah Akbar!"




Baada ya kusumbuliwa na kivimbe cha ini, Abidal alifanyiwa upasuaji na Aprili mwaka huu akapasuliwa tena na kupandikiziwa kipande cha ini alichopewa na binamu yake.

XAVI: BARCELONA TUTAWACHAPA TENA REAL MADRID NA KUBEBA TAJI LA SUPER COPA JUMATANO

Nimewaziba mdomo na pua...! Xavi wa Barca akishangilia goli alilofunga dhidi ya Real Madrid wakati wa mechi yao ya kwanza ya kuwania taji la Super Copa kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona, Alhamisi.
Natishaaaa...! Xavi akishangilia goli lake dhidi ya Real Madrid wakati wa mechi yao ya kwanza ya kuwania taji la Super Copa kwenye Uwanja wa Camp Nou, Alhamisi.
BARCELONA, Hispania
GOLI la Xavi dhidi ya Real Madrid katika mechi yao ya kwanza ya kuwania taji la Super Copa limeihakikishia Barcelona faida ya goli moja kabla ya mechi yao ya marudiano kwenye Uwanja wa Bernabeu, na kiungo huyo wa timu ya taifa ya Hispania anaamini kwamba watashinda tena na kumpa kocha wao mpya, Tito Vilanova kombe la kwanza tangu aanze kazi ya kuwaongoza.

Barca walilazimika kwanza kusawazisha baada ya kutanguliwa kutokana na goli la kichwa la Cristiano Ronaldo, na Xavi alipongeza uwezo waliouonyesha Barcelona wa kurudi mchezoni haraka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Xavi amesema: "Tulianza mechi vizuri, lakini tulionyesha ungangari pia kwa kurudi mchezoni.

"Tulicheza soka safi, na kushinda ilikuwa muhimu kwani imemaanisha kuwa sasa tunajua ni kitu gani cha kufanya tukiw akwenye Uwanja wa Bernabeu. Ikiwa tutacheza vilevile tukiwa Madrid (kama tulivyofanya kwenye Uwanja wa Camp Nou) basi kombe tutalibeba."

Xavi pia ametoa kauli ya kumfariji Victor Valdes, ambaye makosa yake kuelekea mwisho wa mechi yao ya kwanza iliyochezwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Camp Nou yalimzawadia Angel Di Maria goli rahisi kabisa ambalo limeifanya mechi hiyo iendelee kuwa ngumu kutokana na ushindi mwembamba wa 3-2 walioupata Barcelona wakiwa nyumbani.

"Victor (Valdes) ni mchezaji wa kulipwa na tena ni kipa bora kabisa tunayemhitaji," aliongeza Xavi.

Zote, Real Madrid na Barcelona zitarudi katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa kucheza kesho kabla mahasimu hao wa jadi hawajarudiana Jumatano katika mechi yao ya 'el clasico' kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jijini Madrid

No comments: