Saturday, July 14, 2012

NGORONGORO NA NYIGU WADOGO CHAMAZI LEO


Thomas Ulimwengu wa Ngorongoro

Na Princess Asia
TIMU ya taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Chamazi, kumenyana na vijana wenzao wa Rwanda katika mchezo wa kirafiki, kujiandaa na mechi dhidi ya Nigeria Julai 29, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika.
Rwanda ‘Nyigu Wadogo’, waliwawasili Dar es Salaam jana mchana Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la ndege la Rwanda kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ngorongoro Heroes.
Rwanda yenye msafara wa watu 27 wakiwemo wachezaji 20, imefikia katika hoteli ya Sapphire na baada ya mechi ya leo, timu hizo zitacheza tena keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ngorongoro Heroes iko kambini chini ya Kocha wake, Mdenmark Jakob Michelsen na msaidizi wake Mohamed Adolf Rishard.
Mechi dhidi ya Nigeria ambayo ni ya kwanza ya raundi ya pili kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Algeria itachezwa Julai 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

KOMBE LA KAGAME, YANGA YAKATA UTEPE LEO


Kikosi cha Yanga 2012

Na Prince Akbar
HATIMAYE pazia la michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, linapenuliwa leo, kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, Yanga SC dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10:00 jioni.
Mabingwa hao mara nne wa michuano hiyo, wanaingia kwenye mchezo wa leo, wiki moja tu tangu wapate kocha mpya, Mbelgiji Tom Saintfiet ambaye ni juzi tu alitaja wachezaji 20 atakaowatumia kwenye michuano hiyo.
Saintfiet aliwaacha kwenye kikosi chake wachezaji watatu nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo kwa sababu watakuwa na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu.
Aidha, pia aliwaacha beki mkongwe na Nahodha Nsajigwa Shadrack na kiungo Nurdin Bakari.
Saintfiet alisema kwamba Omega, Msuva na Damayo watakuwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa na mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29 dhidi ya Nigeria.
Kocha Tom Saintfiet
“Kwa mujibu wa kanuni natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi wanacheza na Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo watakuwa kwenye maandalizi ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao hata kwenye Nusu Fainali, kwa sababu hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia Nahodha wa klabu hiyo, Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji 20, lakini amesema mchezaji huyo ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi Kuu.
Wachezaji aliowateua baada ya kushauriana na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani kuwa ni; makipa Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan, Idrisa Assenga, Hamisi Kiiza na washambuliaji Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
Tangu aichukue timu, Saintfiet alicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu na kushinda mabao 2-0. Katika mechi hiyo aliwasilisha falsafa mpya ya uchezaji ya timu, ambayo ni soka ya utulivu zaidi mfano kama wa kupaki basin a kushambulia kwa kushitukiza.
Mtakatifu Tom alisema falsafa yake ni ushindi iwe wa 1-0 au 5-0 na timu inayoshinda ni ile ambayo kwanza inajilinda vizuri.
Hivyo wana Yanga waende uwanjani na leo, wakitarajiwa kuendelea kuona timu yao ikipaki basi na hawana budi kuuvmilia mfumo huo, kwa sababu Tom anataka uzoeleke ili autumie kwa ufanisi baadaye kwenye michuano mikubwa ya Afrika.
Tom alitolea mfano mafanikio ya Chelsea msimu uliopita kutokana na mfumo huo, uliowawezesha kuving’oa vigogo wakiwemo waliokuwa mabingwa watetezi Barcelona kabla ya kuifunga Barcelona kwenye fainali na kubeba ndoo ya Ulaya.
Mchezo kati ya Yanga na Atlecito, utatanguliwa na mechi baina ya mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, APR ya Rwanda dhidi ya Waw Salaam.

KIKOSI CHA YANGA KAGAME;
Makipa; Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji; Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.

No comments: