Friday, June 29, 2012

SIMBA WAPELEKA TIMU ZANZIBAR


 


Kikosi cha Simba msimu uliopita

Na Prince Akbar
MABINGWA wa soka Tanzania, Simba SC wamethibitisha kushirikimichuano ya Kombe la Ujirani Mwema Tanzania, iliyopangwa kuanza Jumapili wiki hii visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange, amesema maamuzi ya kushiriki katika mashindano hayo yamefikiwa baada ya majadiliano baina ya uongozi, benchi la ufundi na Kamati ya Ufundi ya Simba.
“Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kufanya hivyo wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Tanzania lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo kwa sasa,” alisema.
Makamu alisema zaidi ya kushiriki michuano hiyo, Simba pia itatumia fursa hiyo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la Kagame lililopangwa kufanyika kuanzia Julai 14 mwaka huu.
Pia, alisema Simba itatumia ziara hiyo kupeleka kombe la Ligi Kuu ya Vodacom kwa wana Simba wa Zanzibar ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ubingwa Vodacom na pia.
“Tusisahau pia kwamba kabla ya kucheza mechi yetu ya mwisho dhidi ya watani wetu wa jadi Yanga ambayo tulishinda kwa idadi ya mabao 5-0, Simba ilikwenda kuweka kambi Zanzibar,” alisema Kaburu.
Simba itaanza michuano hiyo siku ya Jumatatu ambapo itacheza na Mafunzo ya Zanzibar katika pambano lililopangwa kufanyika usiku. Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Jumatatu jioni lakini imesogezwa mbele hadi Jumatatu usiku.
Jumla ya timu nane zinashiriki katika michuano hiyo ambapo Waekundu wa Msimbazi wapo katika kundi A lenye timu za Simba, Azam, Mafunzo na timu ya soka ya taifa ya vijana ya Zanzibar wenye umri wa chini ya miaka 23 (Karume Boys).
Wakati huo huo: Mabingwa hao wa Tanzania, Simba SC, wanatarajiwa kucheza na mabingwa wa soka wa Uganda, Express FC, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, maandalizi yote kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika na kwamba kikosi cha Simba kitaundwa na wachezaji wapya na wa zamani.
Huu utakuwa mchezo wa pili baina ya timu hizo, katika ziara hii ya Tae Wekundu wa Kampala, baada ya awali kutoka sare ya 1-1 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

 

SIMBA KUANZA NA URA, YANGA NA WARUNDI KAGAME, AZAM WAPEWA WAZENJI


Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye kulia akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za TFF, mchana huu. Kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.

Na Prince Akbar
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame watafungua dimba na Atletico ya Burundi katika mchezo wa Kundi C wa michuano hiyo, Julai 14, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC waliowekwa Kundi A, wataanza na URA ya Uganda Julai 16, kwenye Uwanja huo huo.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, Azam FC wao wataanza na Mafunzo ya Zanzibar katika mchezo wa Kundi B, Uwanja wa Chamazi, Julai 15.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye amesema katika Mkutano na Waandishi wa Habari mchana huu, ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam kwamba, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) itashiriki kama timu mualikwa.
Aidha, habari za kusikitisha ni kwamba, Musonye amesema Sudan, Ethiopia, Eritrea na Somalia hazitaleta wawakilishi wao kwa sababu mbalimbali.
Wakati Ethiopia ligi yao inaanza wiki hii, Sudan wawakilishi wao wapo kwenye michuano ya Afrika na wameshindwa kuteua timu mbadala, Somalia wawakilishi wao Elman wamebadilisha uongozi, hivyo bado hawajajipanga na Eritrea kutokana na desturi ya wachezaji wao kuzamia kila wanapokuja kwenye mashindano, wameondolewa.
“Wameondolewa, kwa sababu mbili, kwanza nchi yao imeomba ipewe muda kulifanyia kazi sual hilo, na sisi pia (CECAFA) tunalitafutia ufumbuzi,”alisema Musonye.
Lakini Musonye amekiri kitendo cha kuyatoa mashindano hayo mwanzoni mwa mwaka hadi katikati ya mwaka kumechangia baadhi ya timu kutoshiriki na amesema tayari amewasilisha pendekezo kwenye Mkutano Mkuu, mashindano yarejee kufanyika mwanzoni mwa mwaka kama ilivyokuwa awali.
Kuhusu mechi ya ufunguzi ya Simba kuchezwa Julai 16, ambayo itakuwa Jumatatu badala ya Jumapili, Musonye alisema kwamba imetokana na kwamba Julai 15, Uwanja wa Taifa kutakuwa na fainali za Copa Coca Cola, ambayo maandalizi yake yote yamekamilika.
Yanga ndiye bingwa mtetezi wa mashindano, baada ya kuifunga Simba SC katika fainali mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

RATIBA KAMILI KOMBE LA KAGAME

No comments: