Sunday, April 8, 2012

SIMBA SC KUANZIA NYUMBANI TENA 16 BORA CAF

Kikosi cha Simba kilichofika fainali ya kombe la CAF mwaka 1993, je vijana wa sasa watajibu mapigo hayo mwaka huu? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
SIMBA SC itaanzia tena nyumbani mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya ama El Ahly Shandy ya Sudan au Ferroviario de Maputo ya Msumbiji.
Simba itacheza mechi ya kwanza Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Aprili 29 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa ugenini kati ya Mei 11, 12 na 13 mwaka huu.
Raundi ya Kwanza Simba ilianzia ugenini dhidi ya Kiyovu Sport ya Rwanda na wakaitoa kwa jumla ya mabao 3-2, sare ya 1-1 Kigali na ushindi wa 2-1 Dar es Salaam, wakati Raundi ya Pili ilianzia nyumbani dhidi ya ES Setif ya Algeria ambayo imeitoa jana kwa faida ya bao la ugenini. 
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura amesema hayo leo Dar es Salaam.
Wambura amesema TFF inatoa pongezi kwa uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa Simba kwa kufanikiwa kuingia raundi ya pili (hatua ya 16 bora) ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Bila shaka juhudi, ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali, wachezaji kujituma na kuzingatia maelekezo kutoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Milovan Cirkovic ndiyo msingi wa mafanikio ya Simba.
Tunaamini ushindi huo wa Simba ni changamoto kubwa kwa wachezaji na viongozi kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa kwa vile ina uwezo huo.
Licha ya Simba kufungwa 3-1 na ES Setif jana (Aprili 6 mwaka huu) mjini Setif imefanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo kwa faida ya bao la ugenini. Simba ilishinda mechi ya kwanza nyumbani mabao 2-0.

No comments: