Friday, April 13, 2012

Friday, April 13, 2012


TANGA CEMENT WAIPA BASI COASTAL UNION



Basi walilopewa Coastal Union
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, 1988, Coastal Union ya Tanga, maarufu kama ‘Wagosi wa Kaya’, wamekabidhiwa basi lenye thamani ya Sh Milioni 45 na kampuni ya Tanga Cement.

Akikabidhi basi hilo kwa viongozi wa Coastal, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement, Erick Westerberg, alisema, basi hilo wamelitoa kutokana na juhudi zilionyeshwa na timu hiyo katika Ligi Kuu msimu, inayoelekea ukingoni.

Hata hivyo, Westerberg, alitoa rai kwa viongozi wa klabu hiyo watambue kuwa, basi hilo ni kwa matumizi ya timu tu na sio mengine binafsi, huku akiwataka kulitunza kwa maendeleo ya timu yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Coastal Union, Ally Ahemed ‘Aurora’, alisema, msaada kampuni hiyo waliyoutoa, ni wa kwanza katika kipindi hiki na hiyo ni kutokana na kikosi hicho kufanya vizuri katika ligi.

Aurora, aliomba kampuni nyingine zenye moyo wa kizalendo, kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri zaidi katika mechi za ligi ijayo, kwani hii ya sasa iko mwishoni.

Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Said Sued, aliwahakikishia mashabiki wao kuwa, watahakikisha wanabaki nafasi ya nne mwishoni mwa ligi kuu, huku akisisitiza umoja na mshikamo kwa viongozi na wachezaji wenzie, kuwa ndio siri kubwa ya mafanikio.

Timu hiyo, kwa sasa inaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa maandalizi ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Villa Squad utakaochezwa jijini Dar es Salaam wiki hii.

Thursday, April 12, 2012


TIMU LA KINA SAMATTA LAENDA MASHINDANONI ULAYA

Kocha wa timu ya taifa ya DRC, Le Roy akizungumza na wachezaji wa U-20 ya TPM

KIKOSI cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 cha Tout Puissant Mazembe kinaendelea na maandalizi ya ziara yao ya Ulaya baada ya Jumapili kuifunga Ravens 4-1 kwenye Uwanja mpya wa Lubumbashi Sport Kamalondo.

Mabao ya Maisha, Ushindi (mawili) na Nasri yaliipa ushindi U-20 ya TPM mbele ya macho ya kocha wa timu ya taifa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Claude Le Roy.

Waandaaji wa michuano itakayofanyika Uswisi na Ujerumani wamekwishatoa ratiba na inafahamika U20 ya TPM itacheza na timu gani.

Michuano hiyo iliyopewa jina Blue Star Cup, mjini Zurich Jumatano ya Mei 16, saa 9:30 kwa saa za huko, Mazembe itacheza na wenyeji FC Blue Stars na siku hiyo hiyo saa 12:30 itacheza na Borussia Moenchengladbach.

Alhamisi ya Mei 17, saa 3:15 asubuhi,  Mazembe itacheza na Grasshopper Club Zurich na saa 4:50 itacheza na Panathinaikos.

Klabu sita Afrika zimepeleka timu zao za vijana kwenye michuano hiyo ya FIFA Blue Stars, ambazo na TPM, nyingine ni Al Ahly ya Cairo, Nania FC na Dwarfs za Ghana, Abuja Boys ya Nigeri na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Jumamosi ya Mei 26, saa 8:45 litafanyika gwaride rasmi la utambulisho wa timu katika ufunguzi wa michuano hiyo.

Saa 10.50: Mazembe itacheza na FSV Mainz 05, Jumapili ya Mei 27, saa 12:45, Mazembe itacheza na TUS Ergenzingen na saa 11:55  Mazembe itacheza na timu ya taifa ya U-19 ya Bulgaria wakati Mei 28, saa 4:00 fainali zitaanza.
Kumbuka kwenye kikosi cha wakubwa cha Mazembe kuna wachezaji wawili wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu.

BALOTELLI AZIKANA INTER MILAN, AC MILAN, ASEMA ANATAKA KUBAKI MAN CITY



Mancini kulia na Balotelli mazoezini City
MSHAMBULIAJI Mario Balotelli anataka kubaki Manchester City, licha ya kocha Roberto Mancini kusema nyota huyo mtata atapigwa bei mwishoni mwa msimu.

Kadi nyekundu ya nne aliyopewa Balotelli ndani ya misimu miwili kwenye klabu hiyo, imemkatisha tama Mancini juu ya nidhamu ya mchezaji huyo, lakini waka wa Mtaliano huyo, Mino Raiola amesema mteja wake anataka kubaki Eastlands.

"Huu si wakati wa kurudi Italia. Mario lazima aendelee na kujifunza England. Hatujaomba uhamisho wa Mario," Raiola alisema alipozungumza na Sky Sport baada ya kuulizwa kama Balotelli atarejea Inter Milan au kujiunga na AC Milan.

"Mancini amekanusha kwamba hataki kufanya chochote tenana Mario. Alitarajia adhabu kali na hawezi kumtumia tena msimu huu."

Kadi nyekundu ya mwisho ya Balotelli alipewa mwoshoni mwa wiki iliyopita City ikilala 1-0 mbele ya Arsenal kupewa kadi ya pili ya njano, akianza kumchezea vibaya Bacary Sagna na baadaye Alex Song.

"Kulikuwa kuna wakati wa jazba, lakini sasa hali imetulia (kwa Mancini)," alisema Raiola.

JUVE WAPIGWA FAINI, ONYO KALI KWA UBAGUZI

Mashabiki wa Juve


VINARA wa Serie A, Juventus wamepigwa faini ya Euro fined 30 000 na onyo kali baada ya mashabiki wake kukutwa na hatia ya kufanya vitendo vya kibaguzi juzi wakishinda 2-1 nyumbani dhidi ya Lazio.

Zomea ya kejeli za kibaguzi ilisikika sehemu tano katika mechi hiyo, lakini klabu hiyo na mashabiki wengine walijaribu kuzima hali hiyo, Serie A imesema katika taarifa yake.

Juve ililazimika kucheza milango ya Uwanja wake imefungwa miaka mitatu iliyopita baada ya kumfanyia kejeli za kibaguzi, mshambujliaji wa Inter Milan wakati huo, Mario Balotelli.

VILLARREAL YAJIKONGOJA TARATIBU

Perez


BAO la Hernan Perez dakika za majeruhi usiku wa jana, liliipa Villarreal ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Malaga, ushindi ambao unawaongezea matumaini ya kutoshuika daraja La Liga.

Timu hiyo ambayo inajulikana kama 'The Yellow Submarine', ambayo inashika nafasi ya 17, imefikisha pointi saba kamili za kuwaweka salama kutoka eneo la hatari, baada ya kufikisha pointi 35 zikiwa zimebaki mechi sita.

Villarreal ilimaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita na kucheza Ligi ya Mabingwa, lakini imeshuka mno msimu huu na sasa ina kocha wa tatu kwa msimu huu mmoja pekee, Miguel Angel Lotina anayejaribu kuiepusha na balaa la kushuka daraja.

Kiungo wao wa Paraguay, Perez alifunga bao dakika ya 94 kuiwezesha kuchukua pointi hizo, katika mchezo ambao kipa wa Malaga, Mcameroon Carlos Kameni alilimwa kadi nyekundu dakika ya 81.

Kipa huyo wa Cameroon, alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumuangusha Perez kwenye eneo la hatari na Marcos Senna akafunga la kusawazisha kwa penalti.

Mwanasoka wa kimataifa wa Hispania, Santi Cazorla, aliyekuwa chachu ya mafanikio ya Villarreal msimu uliopita, aliifungia bao la kuongoza Malaga dakika ya 65, lakini hakushangilia kukwepa kuwaudhi mashabiki wa timu yake ya zamani.

Malaga, ambayo inamilikiwa na mtu wa Qatari, inabaki nafasi ya nne kwa pointi zake 50 na imeshindwa kuipiku Valencia yenye pointi 52 katika nafasi ya tatu. Valencia iliifunga Rayo Vallecano 4-1 juzi.

KIONGOZI YANGA AFARIKI DUNIA



MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Wakili Theonist Rutashoborwa amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, nyumbani kwake, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameaimbia bongostaz asubuhi hii kwamba bado wanawasiliana na familia ya marehemu ili kujua zaidi na saa 5:00 asubuhi watafanya Mkutano na Waandishi wa Habari.

Rutta ni mwanachama ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa klabu hiyo kupata ufadhili wa Yussuf Manji mwaka 2006, kutokana na harakati alizoanzisha za Harambee ya Yanga kufuatia hali mbaya ya kifedha ndani ya klabu hiyo chini ya uongozi wa Francis Mponjoli Kifukwe enzi hizo.

MRENO, MROMANIA WAWANIA KUMRITHI PAPIC YANGA

Papic
MABINGWA wa Tanzania, Yanga wapo mbioni kumnasa kocha kutoka Ureno kuja kurithi mikoba ya Mserbia Kostadin Papic anayemaliza mkataba wake wiki ijayo Aprili 18.
Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakutaka kuweka hadharani jina lake alisema kuna makocha wawili ambao CV zao zipo mezani mmoja kutoka Ureno na mwingine kutoka Romania, huku wa Ureno akipewa nafasi kubwa ya kuongoza jahazi hilo la Yanga.
Chanzo hicho cha habari kilisema kuwa wameamua kuachana na Papic kwa kile walichodai kuwa hana jipya katika timu yao huku wakimtuhumu kuwasiliana na marafiki wa Simba 'Friends of Simba' kila mara.
"Hatuwezi kumvumilia kocha ambaye mara kwa mara anawasiliana na Friends of Simba, kwanza nidhamu ya wachezaji wetu imeshuka sana tofauti na mwanzo, tunasubiri mkataba wake uishe alipwe chake aondoke," kilidai chanzo hicho.
Alisema,"kwa kifupi ni kwamba tumeshapata CV za makocha wawili mmoja wa Ureno na mwingine wa Romania, tunasubiri mkataba wake uishe tumalizane naye aondoke zake, mechi yake ya mwisho ni mechi ya Kagera Sugar, hawezi kukaa tena benchi wakati mkataba wake utakuwa umeshamalizika."
Kufuatia hali hiyo, katika mechi ya marudiano na mahasimu wao Simba itakayochezwa Mei 5, Mserbia huyo hatakaa katika benchi la Yanga na huenda Mreno akaongoza jahazi.
Zipo taarifa kwamba Papic hajaongozana na timu yake kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya Toto Afrika kwa kuwa anaumwa ila ni mgomo baridi baada ya kucheleweshewa mshahara wake wa miezi mitatu hata hivyo habari hizo zimepingwa vikali na Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa.
"Papic hadai chochote, kila mwezi tunampa fedha zake, alidai mshahara wa mwezi mmoja tu hapa alipiga kelele, iweje avumilie mshahara wa miezi mitatu? na hilo la mkataba wake muulizeni mwenyewe kama ataendelea au la, mimi siwezi kuuzungumzia mkataba wake wakati bado haujaisha,"alisema Mwesigwa
Hata hivyo, chanzo kingine cha habari kilisema kuwa Yanga ambayo inapokea Sh 26m kila mwezi kutoka kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kama wadhamini wao ipo kwenye matatizo makubwa ya mtikisiko wa uchumi baada ya kulipa fedha nyingi kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo raia wa Uganda, Sam Timbe waliyemfungashia virago mapema mwaka jana huku akiwa na mkataba wa miaka miwili.
Yanga walilazimika kumlipa Timbe mamilioni ya fedha kitu ambacho kimesababisha mpaka leo klabu hiyo kuyumba kiuchumi na mapema mwaka huu wachezaji wa klabu hiyo walitishia kugoma hadi walipwe fedha zao za mishahara huku Papic akitangaza kubwaga manyanga iwapo uongozi hautamalizana na wachezaji na kwamba asilaumiwe kwa matokeo ya uwanjani. 
Wakati huo huo; mabingwa hao wamesema mapambano ya kutetea ubingwa msimu huu bado yanaendelea licha ya kuachwa kwa pointi saba na Simba wanaoshikilia usukani wa ligi hiyo.
Yanga wamesema pamoja na kupokonywa pointi tatu bado wana uhakika wa kuutetea ubingwa huo kama ilivyokuwa mwaka jana, ambapo timu hiyo ilifanya mapinduzi katika hatua za mwisho za ligi na kufanikiwa kutwaa kombe hilo.
Katibu Mkuu wa timu ya Yanga, Celestin Mwesigwa alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba bado mapambano yanaendelea ili kutetea kombe lao, ambapo mwaka huu watani wao wa Jadi Simba wameonyesha dalili na nia ya kulitwaa mapema.
"Hatuwezi kukata tamaa licha ya kuwa tumenyang'anywa pointi tatu, matumaini ya kutetea ubingwa wetu yapo na hilo linawezekana," alisema Mwesigwa.
Mwesigwa alihoji kama mwaka jana waliweza kutwaa ubingwa huokwanini mwaka huu washindwe?, huku akisisitiza kwamba mechi tano walizobakisha kabla ya kumaliza ligi hiyo ndiyo zitawafanya walitwae kombe hilo kwa mara nyingine tena.
"Ninachoweza kusema ni kwamba mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi, tuliachwa kwa pointi nyingi mwaka jana na bado tukachukua kombe iweje tushindwe mwaka huu?," alihoji tena Mwesigwa na kuongeza kuwa bado ligi inaendelea hivyo mashabiki wao wajiandae kucheka na kushuhudia timu yao ikitwaa ubingwa.
Akizungumzia suala la rufaa yao kupinga maamuzi ya Kamati ya Nidhamu kuwapokonya pointi tatu za mechi dhidi ya Costal Union, Mwesigwa alisema suala hilo liko chini ya Kamati hivyo anaichia ili ifanye maamuzi.
"Nimesikia kwenye vyombo vya habari kwamba Kamati itakutana Jumamosi, lakini mimi sijaambiwa chochote juu ya kukutana huko hivyo nasubiri taarifa kutoka kwao, jambo la msingi ni kusubiri maamuzi ya Kamati,"alisema Mwesigwa.
Yanga inashika nafasi ya tatu nyuma ya Simba inayoongoza Ligi Kuu ikifuatiwa na Azam inayoshika Vicky Kimaro na Imani Makongoro (GAZETI LA MWANANCHI LEO)nafasi ya pili hadi sasa.

MAN UNITED YATENGEWA TUZO KIBAO



Uwanja wa Old Trafford unaotarajiwa kuipa tuzo Man United FC
KLABU ya Manchester United imeingizwa kwenye kinyang’amyiro cha tuzo nne kutokana na kuboresha, bidhaa na maendeleo kwa ujumla na kupanua soko lake.

Tuzo tatu za awali ni Tuzo za Biashara ya Uwanja, ambazo zitafanyika mjini Turin, Italia, Mei 15. Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2010, zinahusu mafanikio, ukarabati na fikra safi zinazoendana na dunia ya viwanja, utawala na uboreshaji wa maeneo ya michezo.

Manchester United imeingizwa kuwania tuzo ya Mradi Bora wa Mwaka kwa kuendeleza eneo la jukwaa la vyumba la West Stand.

Ubora wa mradi huo kwamba ni wa kisasa mno na umefanywa kuwa na vifaa ambavyo vinawawezesha mashabiki kujisikia raha wawapo eneo hilo na kuanzisha pia jukwaa lingine la maraha kwa ajili ya ‘watu wazito’ lenye mazingira ya kuvutia ile mbaya.

Klabu hiyo pia imetajwa katika kuwania tuzo ya Ubora wa uhakika, ambayo inahusu mafanikio kwa ujumla, mafanikio ya uongozi katika matukio mbalimbali.

Manchester United inatumai kukomba tuzo zote hizo tatu na kuwa klabu ya kwanza  Uingereza, Uwanja wake kumiliki heshima zote kubwa hizo tatu.

Gwiji wa Manchester United, Gary Neville, ambaye hivi karibuni alipewa heshima ya Balozi wa Mazingira wa klabu, alisema: “Ni babu kubwa kuona Manchester United imepata heshima hii katika utawala wa mazingira. Nafahamu klabu ina jukumu kubwa la kuboresha zaidi mambo,”alisema.

MSAMA PROMOTIONS KUSAIDIA WAJANE

Rebecca Malope mmoja wa nyota waliotumbuiza tamasha la Pasaka


KAMPUNI ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha la Pasaka, inatarajia kuanza kutekeleza ahadi yake ya kuwasaidia wanawake wajane na watu wasiojiweza fedha za mitaji ya biashara.

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema kwa njia ya simu jana kutoka Dodoma kuwa Kamati ya Maandalizi ya Pasaka inatarajia kwenda Mtwara Jumatatu kufanya tathmini ya maeneo ya kutoa msaada.

"Kamati inatarajia kwenda Mtwara Jumatatu kufanya tathmini ya maeneo gani ya kusaidia wasiojiweza... safari hii walengwa hasa ni watu wa vijijini.

"Kama ilivyo ada, kamati yetu haitoa msaada kwa kubagua itikadi za kidini, awe Mkirsto au Muislamu, wote tunawapa msaada na ndiyo maana hata Serikali imekuwa mstari wa mbele kutuunga mkono.

"Tunasaidia wasiojiweza wote wakiwamo wanawake wajane, watoto yatima na walemavu bila kujali udini... watu wa imani zote za dini tunawatendea haki kwa vile hata kwenye matamasha ya Pasaka, wanaohudhuria ni watu wa imani zote za dini," alisema Msama.

Alisema wamekusudia kutimiza ahadi waliyoitoa wakati wa maandalizi ya tamasha la Pasaka lililofanyika Aprili 8 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na lile la Jumatatu ya Pasaka, Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Msama juzi alitoa taarifa ya kuwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha tamasha hilo kwa hali na mali.

Katika tamasha la Uwanja wa Taifa, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye pamoja na marafiki zake alioongozana nao jukwaani walichangia sh. milioni 10, Rais Kikwete aliahidi kuchangia sh. milioni 10 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda sh. milioni 5, hivyo kufanya jumla kuwa sh. milioni 25, zitakakazotumika kusaidia wasiojiweza.

Pia katika tamasha la Dodoma, Naibu Spika, Job Ndugai alichangia sh. milioni 2 kwenye mfuko huo.

Mwaka jana, wanawake wajane waliokabidhiwa fedha za mitaji walitoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ambapo sh. milioni 4 zilitumika. Fedha nyingine zilitumika kusaidia kusomesha watoto yatima.

YANGA KUMREJESHA KOCHA WA MATAJI SAM TIMBE, PAPIC KUBEBESHWA VIRAGO VYAKE

Papic


UONGOZI wa mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Yanga uko mbioni kumrejesha kukinoa kikosi hicho aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mganda Sam Timbe.

Timbe ambaye aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2010/2011 na kombe la Kagame, mkataba wake ulivunjwa msimu uliopita kwa madai ya kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo na nafasi yake kujazwa na Mserbia Kostadin Papic.

Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na Twiga zinaeleza kuwa Timbe atarejea kukinoa kikosi hicho wakati wowote kuanzia sasa akirithi mikoba ya Papic.

Imeelezwa kuwa mkataba wa Papic umebakiza siku chache kumalizika na uongozi hauna mpango wa kumuongeza mkataba mkataba mpya,kutokana kutomuhitaji tena.

Mmoja ya viongozi wa Yanga ambaye hakupenda kutajwa jina lake aliliambia gazeti hili kwamba hawana mpango tena na Papic kutokana na kutokuwa na jipya ndani ya klabu hiyo hivyo wanaendelea na mikakati ya kumrejesha Timbe.

“Mimi nashangaa huyu kocha anazungumza na vyombo vya habari kuwa hajalipwa miezi mitatu, huo ni uzushi ambao hauna maana yoyote...ninachoona ni kutaka kuudanganya umma ili adanganye kuwa kaondoka kwa kutolipwa wakati mkataba wake ulishakwisha,”Aliongeza.

Baadhi ya vyombo vya habari leo viliripoti kocha hutyo kutoambatana na timu Kanda ya Ziwa kutokana na kuugua Tumbo na mafua huku pia ikidaiwa kocha huyo hajalipwa mshahara wake kwa miezi mitatu hali inayomuweka katika mazingira magumu ya ufundishaji wake.

Hata hivyo ofisa habari wa Yanga Louis Sendeu alisema jana kuwa taarifa za Papic kudai mshahara hazina ukweli wowote na kukiri kuwa kocha huyo ni mgonjwa ndio maana hajaambatana na timu katika safari hiyo , lakini kama hali yake itatengemaa huenda akaungana na timu hiyo leo.

Alisema kikosi cha timu hiyo kinanatarajiwa kuondoka Kahama leo kwenda Mwanza tayari kwa mechi yao ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara ambapo jumapili kitashuka kwenye dimba la CCM Kirumba, jijini humo kukwaana na wenyeji Toto African.

SIMBA WAMSHITUKIA AZIM DEWJI NA AHADI ZAKE

Dewji


UONGOZI wa klabu ya Simba umeshangazwa na taarifa zinazotolewa na aliyewahi  kuwa mfadhili wa timu hiyo, Azim Dewji kuhusiana na kutoa fedha kwa wachezaji wa timu hiyo, sambamba na kuileta timu ya Tp Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) .

Hatua hiyo inafuatia hivi karibuni Dewji kukaririwa na vyombo vya habari kutoa shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuipongeza Simba kutokana na kutinga hatua ya pili ya kombe la Shirikisho Afrika (CAF) baada ya kuitoa Es Setif ya Algeria wiki, pia kuileta TP Mazembe kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na Simba.

Mmoja ya viongozi wa Simba (jina tunalo) amesema leo kuwa Dewji amekuwa akifanya mambo kinyemela hali ambayo inasababisha kuwepo kwa mvurugano usio na maana ndani ya klabu hiyo.

Akifafanua zaidi, kiongozi huyo alisema kuwa hata zile fedha za awali (sh.mil.15) ambazo ilidaiwa kuwa amewapa wachezaji hazikuwa na ukweli wowote kwani fedha hizo zilitolewa na uongozi.

“Nakumbuka Azim alikuja kuongea na wachezaji baada ya mchezo wetu na Es Setif hapa nyumbani na kuahidi kutoa mil.15 lakini hakuzitoa na matokeo yake wachezaji walipomfata alidai kuwa hana fedha mpaka mwisho wa mwezi.

“Hata hivyo Dewji hakutoa hiyo hela na tuliposhinda Algeria alidai atawapa wachezaji Mil.15 pindi watakaporejea, lakini timu imerejea tangu jumatatu na mpaka hii leo (jana) hakuna kitu kama hicho hata taarifa za viongozi kukabidhiwa hizo hela ni uongo mtupu,”Aliongeza.

Aidha kiongozi huyo aliongeza kuwa hata taarifa za Dewji kuileta TP Mazembe kwa ajili ya kuja kuipa makali Simba kabla ya mechi yake ya kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan hawana taarifa nazo zaidi ya kuzisoma tu kwenye magazeti.

IBADA YA KANUMBA JUMAPILI ILALA, KARIBUNI SANA



Marehemu Kanumba
MTANDAO wa wasanii Tanzania (SHIWATA) umeandaa ibada maalum ya kumwombea aliyekuwa muigizaji wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba itakayofanyika Jumapili Aprili 15, 2012 kwenye ukumbi wao wa Ilala, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Shiwata, Kassim Taalib amesema leo kuwa amewaomba wanachama wote wahudhurie ibada hiyo ambayo ni moja ya matukio ya mtandao huo katika kuwaombea wanachama waliofikwa na vifo akiwemo mwanachama wao Kanumba aliyeshiriki kwa ukamilifu, uadilifu na mchango mkubwa katika shirikisho hilo katika harakati za kujikomboa kiuchumi.

Alisema Kanumba ambaye alikuwa mwanachama wa Shiwata alikuwa mchapakazi, mpenda maendeleo na aliyewahi kushiriki kikamilifu katika kutafuta mashamba na maeneo ya makazi ambako alikwenda Bagamoyo, Kisarawe na hatimaye kufanikiwa kupata eneo wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani, katika mashamba hayo wanachama zaidi ya 1,000 wamefanikiwa kupata maeneo ya makazi marehemu Kanumba akiwa mmojawapo.

Alisema Shiwata inakusudia kujenga makumbusho makubwa ya wasanii waliofariki wakiwa katika harakati za kuendeleza kazi za wasanii katika kijiji cha Mwanzega.

"Katika makumbusho hayo pia zitawekwa kumbukumbu za kazi za sanaa ikiwemo ya Waziri Mkuu wa zamani marehemu, rashida Kawawa aliyeacheza sinema ya Muhogo Mchungu pamoja na wengine kama marehemu Fundi Saidi (Mzee Kipara),wasanii 13 wa Five Stars na Kanumba"alisema Talib.

Aliongeza kuwa Shiwata pia  inakusudia kuandaa mashindano ya sanaa ya vikundi mbalimbali wakianzia mkoa wa Dar es salaam, mashindano kama hayo yaliwahi kufanyika mwaka 2003 kati ya vikundi vya Kaole,Splendid, Savanna, Nyota Academia,Mambo hayo, Kidedea,Black Eagle na kuibua vipaji mbalimbali akiwemo Cheni, Muhogo Mchungu na marehemu Kanumba.

Lengo la mashindano hayo ni kuinua vipaji vya wasabii wa bongo Flava, Sarakasi, filamu, ngoma, taarabu na muziki wa dansi.

No comments: