Sunday, April 8, 2012

KANUMBA AFUNGA BARABARA, AIRUDISHA EAST COAST, HALI USALAMA SHAKA TUPU

Waombolezaji
BARABARA ya Mtaa aliokuwa anaishi msanii maarufu wa kiume Tanzania, Steven Charles Kanumba aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo imefungwa rasmi.
Barabara hiyo inayotokea Sinza Kijiweni na kwenda Magomeni, ikipitia Tandale Uzuri- pia hutumiwa na watu wanaokwenda Kijitonyoma, Kinondoni wakati mwingine huwa njia nzuri ya mkato kwa madereva wengi wakati wa foleni hususana siku kama leo Jumamosi.
Nyumba anayoishi Kanumba imepakana na hoteli maarufu ya Vatican, Sinza, Dar es Salaam.
Watu wanaoruhusiwa kuingia ndani ni wasanii na wanamuziki tu na wadau kama Waandishi wa Habari na wafanyabishara zinazohusiana na sanaa.
Bado umati ni mkubwa ndani na nje ya nyumba na hilo ndilo limesababisha barabara hiyo kufungwa.
HALI YA USALAMA
Wakati usiku unaingia, tishio kubwa ni usalama wa watu na mali zao na Kamati ya Mazishi chini ya Mwenyekiti wake, Gabriel Mtitu imeanza kuhaha kuhakikisha ulinzi unaongezwa kwenye eneo hilo.
Kwa sasa walinzi waliopo ni askari wawili wa usalama barabarani na Polisi wasiozidi wanne- zaidi ya hapo kuna walinzi wa kampuni binafsi, Maninja ambao ni maarufu kusimama milangoni kwenye kumbi za dansi.
Wakati dalili za vurugu kutoka kwa ‘Masela wa Sinza’ zikijitokeza, Mjumbe wa Kamati ya Mazishi, Ruge Mutahaba alionekana akijadiliana na Ofisa wa Jeshi la Polisi, Koba Kimanga juu ya kuongeza ulinzi.
Koba, ambaye ni bondia mstaafu wa ngumi za Ridhaa uzito wa juu nchini, alimshauri Ruge aagize askari wa kikosi cha mbwa na kuongezewa askari ambao ameshauri waje na gari la doria.
UIGIZAJI UNAENDELEA
Penye wengi hapakosi wengi, kuna vituko vya hapa na pale kwenye eneo la msiba.
Kikubwa ni waigizaji, watu wa fani moja na marehemu Kanumba kuendeleza uigizaji wao eneo la tukio.
Kwa mfano mtu anatoka alipotoka akiwa anafuraha anacheka na kurukaruka, lakini akiingia getini anajifanya ana majonzi sana na hajiwezi, anaangua kilio au kujiangusaha haswa kwa waigizaji wa kike.
Baadhi kwenye eneo hilo wameonekana kuanza kuishitukia hali hiyo na akitokea ‘mtu kituko’ wa aina hiyo nao wanaichukulia hiyo kama burudani na kuanza kucheka.  
BADO WANAZIMIA
Lakini bado wapo wenye hisia za kweli za majonzi ambao hakika wameshindwa kujimudu na kufikia hadi kuzimia.
Dada mmoja ambaye jina lake halikupatikana, aliyeingia analia, alipofika karibu na eneo ambalo kuna picha ya marehemu kwenye meza ya rambirambi, alianguka chini na kupoteza fahamu.
Zilipita dakika tano watu hawajui cha kufanya juu yake, lakini baadaye ukatolewa ushauri amwagiwe maji ndipo akafanikiwa kuzinduka.
WASANII NA KITU KIZITO
Ruge ambaye ni Mkurugenzi wa Clouds Media Group, amefanya kikao na wasanii mbalimbali kuwashauri wafanye kitu kizito kwa ajili ya kumuenzi msanii mwenzao huyo.
Ruge amewataka wasanii wenyewe kuketi chini na kufikiria cha kufanya kama kazi ya pamoja au kila mmoja kazi yake binafsi, lakini Jumanne siku ya kuuaga mwili wa marehemu kiwasilishwe mbele ya umma kwenye viwanja vya Leaders.
Prodyuza Lamar amejitolea studuo wasanii wakarekodi nyimno mbili na Diamond ameiambia bongostaz, yeye yupo tayari kutia sauti kwa ajili ya Kanumba.
EAST COAST TEAM IMERUDI?
Majira ya saa 10 jioni, kwa pamoja wasanii waliokuwa wakiunda kundi la East Coast Team lililokuwa na maskani yake Upanga, Dar es Salaam waliingia kwa pamoja nyumbani kwa marehemu na kusisimua watu.
Wakiongozwa na King Crazy GK, wengine walikuwa ni Mwana FA, AY, Snare na Benja ambao maana yake wimbo wa Hii Leo umekamilika na Ama Zao unaimbika.
Lakini ECT wote walionekana kutekwa zaidi na msiba- hivyo hawakuwa tayari kuzungumzia mustakabali wao zaidi ya kuiambia bongostaz wataingiza sauti kwenye wimbo kwa Lamar.
CHOKI BOSI WA DANSI BONGO:
Kwa moyo mkunjufu, Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) Asha Ramadhani Baraka amemteua Ally Choky, mwanamuziki wake wa zamani kwenye bendi ya Twanga Pepeta kuwa ‘bosi wa wasanii wa dansi nchini’ katika suala la msiba wa Kanumba.
Asha ameiambia bongostaz kwamba katika juu ya kitu gani watafanya wasanii wa dansi kwa ajili ya Kanumba, Choky atashughulikia suala hilo na kitu kitakuwa tayari Jumanne wakati wa kuuaga mwili wa marehemu.
KAMATI YA MAZISHI
Kamati ya Mazishi inaundwa  na Mwenyekiti Gabriel Mtitu, Makamu Mwenyekiti, Jacob Steven ‘JB’, Katibu, William Mtitu na Wajumbe Issa Mussa ‘Cloud’, Kimosa, Vincent Kigosi ‘Ray’, Single Mtambalike ‘Richie’, Dilesh Solanki, Adele Kanumba (dada wa marehemu), Hartman Mblinyi, Ruge, Ally Choky, Simon Mwakifamba, Eric Shigongo, Steve Nyerere, Mahsein Awadh ‘Dk Cheni’ na Mama Nassor, mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Kanumba.
Kamati hiyo Wajumbe wake wanaonekana kufanya kazi nzuri, kuhakikisha wanamsitiri kwa hadhi yake ‘The Great Steve Kanumba’.

No comments: