Saturday, April 14, 2012

Saturday, April 14, 2012

WAISLAMU WAMVUA HIJAB LULU

Lulu
SIKU chache baada ya kufikishwa mahakamani kwa msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael 'Lulu' kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha msanii mwenzake Steven Kanumba, waislamu wamelaani msanii huyo kutoka mahakamani akiwa amevalia vazi la Hijab.
Kwa mujibu wa mamapipiro blogspot, tamko hilo lililotolewa jana katika msikiti wa Ngazija jijini Dar es Salaam wakati wa Swala ya Ijumaa ambapo waumini hao walidai kuwa msanii huyo anaudhalilisha uislamu.
Walisema hawakupendezwa na kitendo hicho na kama atapandishwa tena mahakamani katika mavazi hayo wataandamana.

RAGE AMSUTA KOCHA TP MAZEMBE



Aden Rage
SIKU chache baada ya kuwepo kwa utata juu ya ujio wa klabu yaTp Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na klabu ya Simba, uongozi wa Simba umewatoa hofu mashabiki wa Simba na wa soka kwa ujumla juu ya ujio huo.

Hivi karibuni aliyewahi kuwa mdhamini wa Simba na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo Azim Dewji alitangaza kuileta Tp Mazembe kwa ajili ya kuipa makali Simba ambayo inatarajiwa kucheza mechi ya kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan.

Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage ameiambia mamapipiro blogspot leo kuwa  yeye na makamu mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Azim Dewji wamekuwa wakifanya mawasiliano ya mara kwa mara na mmliki wa TP Mazembe Mose Katumbi.

Alisema anashangazwa na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari zikimnukuu kocha msaidizi wa Tp Mazembe Lamine Ndiaye  kutokuwa na taarifa za ziara hiyo kitu ambacho hakina mantiki yoyote kwa kuwa kocha kazi yake ni kufundisha tu.

“Kama mtu anataka uhakika awasiliane na Katumbi ama katibu wake Kitenge, sisi tunafanya mazungumzo wenyewe kwa wenyewe (viongozi) na mambo yakiwa tayari wanapewa taarifa wengine ndiyo maana hata baadhi ya viongozi wenzangu wea Simba hawana taarifa rasmi,”Alisema Rage.

Rage aliongeza kuwa mipango kuhusiana na ujio wa timu hiyo ambayo nayo inatarajiwa kukwaana na El Mereikh ya Sudan katika Ligi Ya mabingwa barani Afrika yanakwenda vema na kama kutakuwa na mabadiliko yoyote watatoa taarifa rasmi.Katika hatua nyingine, Rage amempongeza Dewji kwa kutimiza ahadi yake ya kuwakabidhi wachezaji wa timu hiyo kitita cha shilingi milioni 15 baada ya kuitoa Es Setif ya Algeria na kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).

RASMI SASA TBL WADHAMINI WAPYA TAIFA STARS

Meneja wa Kilimanjaro Beer, George kavishe kushoto
BIA ya Kilimanjaro Premeum Lager rasmi ndio mdhamini mpya wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, bongostaz imeipata hiyo.
Bia hiyo inayozalishwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), wiki hii itafanya hafa maalum ya kuutangaza rasmi udhamini huo.
Chanzo cha habari kutoka TBL, kimesema hafla hiyo itafanyikia katika hoteli ya Serena, iliyokuwa Royal Palm Movenpick, Dar es Salaam wiki hii.   
Tangu mwaka 2006, Taifa Stars imekuwa ikidhaminiwa na Serengeti Breweries Limited ambao wameshindwa kuingia mkataba mpya na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa sababu ya kupandishiwa dau.  
Baada ya mkataba wao (SBL) kufikia tamati Desemba, mwaka jana, TFF ikaipandishia dau la udhamini kutoka Sh. Bilioni 1.2 hadi Bilioni 3.6, ambayo ni zaidi ya asilimia 300.
TBL imekubali kuidhamini Stars kwa dau la Sh. Bilioni 3.6 kwa mwaka.
Kilimanjaro pia ni wadhamini wa watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga na mashindano ya Kombe la Taifa, Kili Taifa Cup.

AL AHLY SHANDY TAYARI KUUA SIMBA WETU

Wachezaji wa Simba SC
AL Ahly Shandy ina fungu la kutosha na mikakati mizito kuhakikisha inaing'oa Simba katika mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho, lakini kwenye Ligi Kuu Sudan bado inapepesuka.
Al Ahly inayoshiriki kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa tangu ianzishwe ikiwa ni timu changa kama Azam, itacheza na Simba jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza Aprili 29 kabla ya kurudiana jijini Khartoum Mei 11.
Mwandishi Mwandamizi wa Redio Sudan, Yousif Mohamed Yousif, aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kwa njia ya simu kwamba timu hiyo ni changa kwenye ligi ya Sudan na sasa inashikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi 10, ingawa iko makini.
"Wamejipanga kifedha na wana bajeti ya kutosha, wana wachezaji wazuri chipukizi na wazoefu, ni timu ya watu wenye fedha ndiyo maana nakwambia wana nafasi kubwa ya kusonga mbele," alisema.
"Maandalizi yao ni mzuri, ninavyoongea na wewe wanaendelea na ligi ya hapa Sudan. Wanacheza kwa ushirikiano mkubwa ingawa bado wako kwenye nafasi za chini.
"Bado hawajataka kuzungumzia sana mambo ya Simba, wanajipanga vizuri wenyewe kwanza katika maandalizi ya ndani.
"Lakini nadhani wiki ijayo watakapoingia kambini rasmi kujiandaa na Simba tutajua mambo mengi zaidi."
Mtangazaji huyo ni miongoni mwa wachambuzi wanaosifika sana jijini Khartoum na hakosekani katika safari yoyote ya timu ya taifa ya Sudan.
Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Sudan yenye timu 14, timu zote zimecheza mechi saba mpaka sasa na wapinzani hao wa Simba wapo kwenye nafasi ya tano wakiwa na pointi 10.
Wameshinda michezo miwili na kutoka sare minne huku wakipoteza mmoja. Wamefunga mabao saba na kufungwa matano. Al Hilal inaongoza msimamo kwa pointi 19, ikifuatiwa na El Merreikh yenye pointi 15.
Katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho, timu hiyo iliifunga Ferroviario bao 1-0 mjini Maputo na katika marudiano ikaisulubu mabao 2-0.
GAZETI LA MWANASPOTI LEO

YANGA WAPIGA DILI LIKIFELI WAMEUMIA

YANGA inacheza penalti ya mwaka nje ya uwanja na ikiikosa hiyo basi itafunga hesabu na kukabidhi kila kitu kwa Simba na Azam, lakini Fred Minziro amesisitiza Yaw Berko amerudi uwanjani vizuri kujiunga na makipa wenzake, Shabaan Kado na Said Mohammed.
Uongozi pia umetoa tamko zito kwamba kocha Kosta Papic haendi kokote na atakaa kwenye benchi la ufundi mpaka msimu wa Ligi Kuu Bara umalizike Mei 5, 2012.
Simba inaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi 50 ikifuatiwa na Azam yenye 47 na Yanga 43. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ambaye pia ni bosi wa Kamati ya Fedha na Mipango wa Yanga, Salum Rupia, amesema: "Hii rufaa tuliyokata kwa Kamati ya Nidhamu ya TFF ni kama penalti, tukikosa hapo ubingwa basi.
"Ni kitu cha wazi kabisa, Simba watakuwa mabingwa. Pengo la pointi litakuwa kubwa watakuwa wametuzidi mbali, lakini tukishinda rufaa tutakuwa na tofauti ya pointi nne ambazo ni rahisi kuzifuta, kwa sababu tukikutana nao tutawapiga.
"Simba hawawezi kutufunga, kwani safari hii tuko fiti sana na huwa wanatuzidi vitu vidogo tu, tulishawajulia na kuwadhibiti siku nyingi ndiyo maana siku hizi hawatuwezi."
Rupia anakiri kuwa uwezekano wa Simba kushinda mechi tatu kati ya nne ilizobakiza ni mkubwa ndiyo maana wao wanategemea rufaa waliyokata kupinga kupokwa pointi tatu kwenye mechi dhidi ya Coastal Union walipomchezesha Nadir Cannavaro aliyekuwa na kadi nyekundu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema: "Kamati ya Nidhamu ya TFF iliyokuwa ikutane Jumamosi (leo) kujadili rufaa ya Yanga, imeahirisha mkutano wake hadi Jumanne ya Aprili 17."
Kamati hiyo iko chini ya uenyekiti wa Kamishna Mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana.
Yanga inapiga hesabu kwamba endapo ikirudishiwa pointi tatu itafikisha 46 na kubakiza pengo la pointi nne na Simba ambao wamedai wataifunga watakapocheza nayo Mei 5.
Rupia alisema: "Kama mambo yatashindikana inabidi kutafuta nafasi ya Kombe la Shirikisho, lakini tutashinda mechi zote tano tulizonazo mkononi, ikiwemo Simba, hilo halina mjadala, tunajiamini kwa kusema hivyo na tunajua tutapataje hizo pointi."
Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa amesema: "Kuhusu suala la Papic, ninakuhakikishia haendi kokote, mkataba wake nimeusaini mimi una kipengele kinachoeleza atakuwa kocha wa Yanga mpaka mwisho wa msimu wa Ligi hata kama ikimalizika mwakani.
"Kila kitu kipo kwenye maandishi na nakala anayo, yeye anajua haya ninayosema."
Papic, ambaye amesisitiza kwamba mkataba wake unamalizika Aprili 24, hayupo na Yanga iliyopo Mwanza kujiandaa na mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Toto Africa kwa maelezo kuwa ni mgonjwa na Mwesigwa amethibitisha anatibiwa.
Kocha Msaidizi Fred Minziro alizungumza na Mwanaspoti jana Ijumaa kutoka Mwanza na kusema: "Wachezaji wote wako safi, tunataka kushinda kwanza hizi mechi mbili dhidi ya Toto na Kagera huku ugenini halafu mambo mengine yaendelee.
"Tumeshazungumza na wachezaji kwamba sisi tunacheza mechi zetu zote tushinde, hatuangalii mambo ya Simba, Azam wala timu nyingine. Mwisho wa siku tukimaliza kazi na pointi zetu mkononi ndiyo tutajua nani mbabe."
Minziro amethibitisha kuwa Berko anaendelea vizuri na kwamba ana uwezo wa kucheza kama wenzake baada ya kuwa nje muda mrefu.
GAZETI LA MWANASPOTI LEO

MASWALI 10 YA KUJIULIZA KIFO CHA KANUMBA

Marehemu Kanumba
WAKATI Watanzania wakiwa bado katika simanzi kutokana na kifo cha msanii wa filamu, Steven Kanumba, kuna maswali ambayo yamekuwa yakiwatatiza wengi na yanahitaji majibu.

Mdogo wa marehemu, Seth Bosco alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kifo hicho, lakini zilitofautiana huku pia kukiwa na taarifa ya Polisi wa Mkoa wa Kinondoni.

Kauli mbili tofauti za Seth

Alipohojiwa na waandishi wa habari, Jumamosi asubuhi, Seth alisema Kanumba alifika nyumbani akiwa na Lulu saa sita usiku wa kuamkia siku hiyo wakiwa wanazozana wakaingia chumbani lakini hazikupita dakika tatu, Lulu akatoka na kumfuata Seth na kumwambia Kanumba amejipigiza ukutani amedondoka chini.

Seth alisema alikwenda na kumkuta Kanumba akiwa chini huku povu likimtoka mdomoni akampigia daktari simu, ambapo baada ya kumpima, daktari huyo akashauri apelekwe Hospitali Muhimbili.

Seth anasema wakati anakwenda hospitali alimwacha Lulu nyumbani na aliporudi hakumkuta na hajui alishikwa vipi na polisi.

Akihojiwa na vyombo vya habari mchana huo wa Jumamosi, Seth anasema baada ya kula chakula cha jioni, Kanumba alimwambia ajiandae waende klabu.

Seth anasema alimwambia Kanumba kuwa tayari amejiandaa, Kanumba akasema nisubiri. Kanumba akaingia chumbani, ghafla akasikia mlio wa gari, Lulu akashuka na kuingia ndani, akapitiliza moja kwa moja chumbani kwa Kanumba, baada ya muda mfupi, Seth akasikia mzozo chumbani, akaona kimya.

Lulu akatoka akiomba msaada kwa Seth kuwa Kanumba kaanguka, aliingia akamkuta akiwa amelala chini hivyo akampigia simu daktari.

Akasema wakiwa njiani wakapitia Kituo cha Polisi cha Oysterbay wakiwa na Lulu, baada ya maelezo, polisi wakamwambia Lulu abakie kwa ajili ya maelezo zaidi.

Maswali ya kujiuliza

1. Kwa mujibu wa Kamanda Kenyela kifo hicho kilitokea saa 9 usiku, Je, Kanumba alimwambia mdogo wake wajiandae kwenda klabu muda huo?

2. Seth amezungumza kauli mbili tofauti za tukio hilo. Je, ipi ni taarifa sahihi?

3. Ni saa ngapi Seth na Kanumba walikuwa wanapata chakula cha jioni?

4. Kanumba alikuwa amerudi akitokea klabu au ndiyo alikuwa anataka kwenda klabu?

5. Hivi karibuni, Lulu alikaririwa na vyombo vya habari akisema hana mpenzi. Je, Kanumba alikuwa mpenzi wake?

6. Siku zote Kanumba alikuwa akidai hatumii kilevi chochote. Je, ni nani alikuwa anakunywa Jack Daniel's chumbani?

7. Je, Lulu alikimbia baada ya kifo cha Kanumba au aliambatana na Seth kwenda Muhimbili kabla ya Polisi kumshikilia katika kituo cha Oysterbay walipokwenda kufuata PF3?

8. Je, Lulu na Kanumba waliingia pamoja nyumbani kwa Kanumba au Lulu alikuja baadaye?

9. Lulu alikuwa anazungumza na nani kwenye simu na ni nini kilikuwa kinazungumzwa?

10. Lulu alikamatwa na polisi akiwa wapi?

KIFO CHA KANUMBA, ALI KIBA AHOJIWA NA POLISI

Ali Kiba
MSANII wa muziki wa Bongo Flava, Ali Kiba, anadaiwa kuhojiwa na polisi kwa maelezo ndiye aliyempa Elizabeth Michael Lulu msaada wa usafiri (lifti) baada ya kutoka kwa Steven Kanumba.
Lulu ndiye anayetuhumiwa kuhusika na kifo cha Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Kachelo aliyemhoji Lulu Jumatatu wiki hii, amedai kuwa msanii huyo alihojiwa katika kituo cha Polisi cha Oysterbay kutokana na kutajwa na mtuhumiwa kuwa ndiye aliyempatia lifti baada ya kutoka kwa Kanumba.
Mwanaspoti lilimtafuta Ali Kiba ili azungumzie taarifa hizo, alipopatikana kwa njia ya simu, msanii huyo alisema: �Samahani kaka siwezi kuzungumzia chochote kuhusu mambo hayo.� Kisha akakata simu.
Lulu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jumatano wiki hii na kutotakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji.
Lulu alitoa maelezo yake polisi Jumatatu ikiwa ni saa 65 tangu kutokea kwa kifo cha Kanumba., ambapo alizungumza na kachero wa Makao Makuu ya Polisi ambaye pia ana taaluma ya saikolojia.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kachero huyo (jina tunalo) aliyetoka makao makuu alifanikiwa kufanya mahojiano na binti huyo ambaye awali aligoma.
Imeelezwa kuwa, alitumia takribani sasa tatu kumlainisha Lulu azungumze.
Katika mahojiano na gazeti la The Citizen Jumanne, kachero huyo ambaye alitoka katika Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai alisema tayari amemhoji mtuhumiwa namba moja Lulu pamoja na msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya kufuatia kifo cha Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia Jumamosi.
Akimnukuu Lulu katika mazungumzo yake, kachero huyo alisema Lulu aliitwa na marehemu Kanumba ili waweze kutoka (out) kwenda kwenye bendi ya Mashujaa ambayo ilikuwa inapiga kwenye kiwanja chao cha nyumbani, Vingunguti.
Mtuhumiwa alionekana kutokuwa tayari, lakini marehemu �akamlazimisha�.
Kachero huyo alisema: �Lulu anadai alifika nyumbani kwa marehemu saa tano usiku, lakini akiwa ameweka msimamo wa kutokwenda sehemu yoyote usiku ule, lakini Kanumba alikuwa akilazimisha ndipo yakatokea mabishano na marehemu akafunga mlango kwa funguo.
"Hata hivyo, baada ya ugomvi wa kama nusu saa hivi, Lulu alifanikiwa kuondoka chumbani humo na alifungua mlango kwa taharuki na kuondoka bila kujua kilichotokea nyuma, huku akimweleza ndugu wa marehemu kwamba Kanumba ameanguka."
Mpashaji habari wetu huyo alisema, kumekuwa na jumbe fupi za maneno kutoka kwa wanasiasa ambazo zimekuwa zinaingia kwenye simu ya kiganjani ya Lulu, zikiahidi kumsaidia.
Alionya kuwa kama wanasiasa wataanza kuingilia uchunguzi wa Polisi katika kesi hiyo ambayo imevuta hisia za watu wengi, wanaweza kuharibu mambo. Lakini yeye mwenyewe akionyesha kwamba yuko imara na anafahamu anachokifanya.
Kuhusu msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba, kachero huyo alisema kwamba alihojiwa kutokana na kutajwa na mtuhumiwa kama mtu aliyempatia msaada wa usafiri (lifti) baada ya kutoka kwa Kanumba.
Kachero huyo alisema kutokana na taarifa ambazo wanaendelea kuzipata, kuna uwezekano watu wengi zaidi wakahojiwa ili kujiridhisha kabla ya �watuhumiwa� kuanza kupandishwa kizimbani baada ya upelelezi kukamilika.
GAZETI LA MWANASPOTI LEO:

No comments: