Monday, December 28, 2015

Chikongola mabingwa michuano ya Amani Cup Mtwara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP-Henry Mwaibambe, akikabidhi kombe la michuano ya Amani Cup iliyomalizika juzi mjini Mtwara, kwa Nahodha wa timu ya kata ya Chikongola ambao ndio waliyoibuka mabingwa, Ally Bushiri. Chikongola waliwafunga kata ya Chuno magoli 2-1 katika mchezo wa fainali


Nahodha wa timu ya kata ya Chikongola, Ally Bushiri, akiinua kombe la Amani juu baada ya kukabidhiwa kutoka kwa kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, ACP-Henry Mwaibambe, ambae aliandaa michuano ya Amani Cup na timu ya Chikongola kuibuka mabingwa kwa kuichapa Chuno mabao 2-1 katika mchezo wa fainali.

Golikipa bora wa michuano ya Amani Cup, Elmanus Mbunju wa timu ya Chikongola, akipokea zawadi kutoka kwa kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, ACP-Henry Mwaibambe.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

TIMU ya kata ya Chikongola mkoani hapa imeibuka mabingwa wa michuano ya Amani Cup baada ya kuichapa Kata ya Chikongola kwa magoli 2-1 katika mchezo wa fainali uliofanyika juzi katika uwanja wa Polisi na kuhudhuliwa na vijana wengi waliohamasika na michuano hiyo.
Baada ya kuibuka mabingwa katika michuano hiyo ambayo iliandaliwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara ACP-Henry Mwaibambe, timu ya Chikongola ilikabidhiwa zawadi ya fedha tasilimu shilingi laki tatu (300,000), mpira pamoja na Kombe, huku mshindi wa pili timu ya kata ya Chuno ikipata fedha tasilimu shilingi laki mbili (200,000) na mshindi wa tatu kata ya Shangani ikiambulia shilingi laki moja (100,000).

Mashabiki wa timu ya Chikongola wakiwa wamembeba juu Nahodha wao, Ally Bushiri, baada ya kukabidhiwa kombe la ushindi wa michuano ya Amani Cup

Zawadi nyingine ambazo zilitolewa na kamanda wa polisi ni kwa mlinda mlango bora ambaye ni Elmanus Mbunju wa Chikongola aliyepata kitita cha shilingi elfu hamsini (50,000), mlinzi bora ni Ally Bushiri wa Chikongola, mfungaji bora Hussein Abdallah kutoka kata ya Shangani na mwamuzi bora Muksini Chibwana ambao wote walizawadiwa shilingi elfu hamsini (50,000).
Akizungumzia lengo la kuandaa michuano hiyo, kamanda Mwaibambe alisema ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kujenga na kuendeleza ukaribu baina ya wananchi na jeshi la polisi na kuwashukuru baada ya kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu kumalizika kwa amani mkoani hapa.

Heka heka katika lango la timu ya Chikongola.

“Nimefurahi mashindano yalikuwa na msisimko mkubwa sana, malengo ya mashindano yametimia kwamba malengo yetu ilikuwa ni kuwa karibu sana na jeshi la polisi tushirikiane katika kukomesha uhovu mbalimbali katika jamii yetu..uchaguzi uliopita ulikuwa nzuri, japo kulikuwa na changamoto nyingi sana wapo wachache walipata madhara na waliumia, lakini kwa ujumla wake uchaguzi ulikwenda kwa amani na utulivu..si kwa nguvu ya polisi bali ni ushirikiano wenu wananchi na jeshi la polisi, hatuna zawadi ya kuwapa zaidi yah ii burudani..” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP-Henry Mwaibambe, akikabidhi zawadi kwa Nahodha wa timu ya Chikongola, Ally Bushiri, baada ya kuibuka mabingwa wa michuano ya Amani Cup.

Aidha, aliwaahidi wananchi kuendelea kuwapatia burudani za aina hiyo kwa malengo yaleyale, ambapo ifikapo mwezi Machi 2016, ataandaa mashindano mengine ambayo yatakuwa bora zaidi ya haya ambayo yamemalizika.
Michuano hiyo ambayo ilianza wiki mbili zilizopita na kuchezwa kwa mtindo wa mtowano, ilihusisha jumla ya timu 20, ambapo timu 18 zilitoka katika kata zote 18 za Manispaa ya Mtwara huku timu mbili zikitoka katika kata za Halmashauri ya Mtwara vijijini.

No comments: