Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, aliyedaiwa kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana, amelazika kupatiwa rufaa na kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
Akizungumza ofisini kwake hii leo, mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara ya Ligula, Dkt. Mhuza Mdoe, alisema wamelazimika kumpatia rufaa hiyo ili apatiwe vipimo zaidi na kuweza kubaini tatizo alilonalo ndani ya mwili wake, ambapo mpaka sasa halijafahamika.
“Tukio lenyewe ilivyokuwa ni kwamba inahitajika vipimo vya ziada, kwahiyo ni vyema kwamba aende kwenye hospitali kubwa ili kuweza kugundua kama kuna shida yeyote kubwa ndani ya mwili wake..nachoweza kusema ni kwamba sisi tumefanya uchunguzi katika kiwango chetu na tumempatia matibabu katika kiwango chetu..” alisema.
Hata hivyo mganga huyo hakutaka kuweka wazi juu ya tatizo alilotibiwa kwa siku moja aliyolazwa hospitalini hapo, na kusema kuwa ni siri za mgonjwa ambazo hazipaswi kuelezwa.
“Siri za mgonjwa hizo hatuwezi kuziongea lakini tumemtibia kuhakikisha kwamba anapata nafuu kwa matatizo ambayo alikuwa nayo..na hakukuwa na mabadiliko makubwa na sio kwamba ilikuwa inaenda kwenye hali mbaya..” aliongeza.
Kwa upande wake, kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara ASP Henry Mwaibambe, alipotafutwa kwa ajili ya kueleza taarifa za kutekwa kwa mgombea huyo, alisema yuko kwenye majukumu mengine, hivyo mazingira aliyopo hawezi kulizungumzia swala hilo.
Joel Nanauka |
Kufuatia kuzagaa kwa uvumi wa takribani siku nne zilizopita kuwa mgombea huyo alitoweka ghafla na kutofahamika aliko huku wengine wakienda mbali zaidi na
kudhani kwamba ametekwa na watu wasiojulikana, hatimaye alionekana katika
Zahanati ya Bursa ilyopo manispaa ya Mtwara akipata matibabu.
Kwa mujibu
wa daktari wa Zahanati hiyo aliyempokea na kushughulika na huduma ya kwanza kwa
mgombea huyo kabla ya kumpatia rufaa ya kwenda hospitali ya mkoa ya Ligula,
Dkt. Pendo Mmbando, alisema alipokelewa hospitalini hapo alfajili ya leo akiwa
mwenyewe bila ya kuambatana na mtu.
Dkt. Pendo Mmbando |
Alisema,
walimfanyia vipimo na kubaini kuwa sukari yake ilikuwa iko chini pamoja na
malaria, na kuamua kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kumkatia rufaa ya kwenda
hospitali ya Ligula.
“Alikuja
mwenyewe alfajiri na alipokelewa kama mgonjwa wa kawaida kwasababu tulikuwa
hatujui chochote kinachoendelea, alipimwa sukari, malaria na mkojo..baadae
akabainika kuwa sukari ipo chini, malaria ipo lakini akawa analalamika kuwa
anasikia maumivu ya mbavu na shingo..” alisema.
Baada ya
kupata huduma ya kwanza, alichukuliwa na baadhi ya ndugu zake na marafiki zake
na kumpeleka katika hospitali ya Ligula, ambako alipokelewa na kufikishwa
wodini na baadae kuchunguzwa na daktari.
Hata hivyo,
hakukuwa na uwezekano wa kuzungumza naye kutokana na waandishi kuzuiwa na
askari polisi kwa madai kuwa hawezi kuzungumza kutokana na maumivu na kupoteza
baadhi ya kumbukumbu ya tukio lililomtokea, jambo ambalo limekuwa gumu kutambua
undani na chanzo cha tukio la kupotea kwake katika mazingira ya kutatanisha.
Joel Nanauka |
Baadae
waandishi waliruhusiwa kuingia wodini humo lakini kwa mashariti ya kutozungumza
naye na baadala yake, wapige picha na kuondoka.
Kwa upande
wake, mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Mdoee Muhuza, alisema kwa mujibu
wa maelezo yake ni kwamba aliokotwa mahali ambapo alihisi kuwa alipewa dawa za
usingizi na baadae kupelekwa katika Zahanati ya Bursa kabla ya kufikishwa
hospitalini hapo ambako alifanyiwa uchunguzi ambao hata hivyo hawakubaini kuwa
na majeraha yeyote mwilini mwake.
Dkt. Muhuza Mdoe |
“Kuna maeneo
ambayo anasema alikuwa ansikia maumivu lakini kwa maelezo yake ni kwamba kadiri
muda unavyokwenda na dawa ambazo alikuwa amepatiwa basi maumivu yanakuwa
yanapotea taratibu..zaidi anachokielezea kwa sasa ni kwamba mwili tu hauna
nguvu na anajisikia kuchoka..” alisema.
Naye, baba
mzazi wa mgombea huyo, mzee Grey Nanauka, alisema taarifa za kutoonekana kwa
mwanae alizipata siku ya Jumatatu, Oktoba 5 mwaka huu, na alikuwa wilayani
Newala, ambapo alipigiwa simu na mke wake.
Alisema
aliamua kujaribu kudadisi kujua mazingira ya kutoweka kwake, ambapo aliambiwa kuwa
aliondoka asubuhi na hakuna mtu mbaye alimuaga, na kwamba walijaribu kusubiri
mpaka jioni kabla ya kuanza kumtafuta kwa simu lakini simu zake hazikuweza
kupatikana.
Grey Nanauka |
“Kwahiyo wliendelea
kumtafuta kwa simu mpaka majira ya saa tano za usiku pamoja na kwenda kumtafuta
katika baadhi ya maeneo ambayo anaenda kwa ajili ya shughuli zake za siasa
lakini hakuweza kupatikana..kwahiyo kilichoamuliwa ni kwenda kutoa taarifa
kituo cha polisi..mpaka siku iliyofuata hakupatikana na mimi nilirudi jana saa saba mchana nikaungana na wenzangu pamoja na askari ambao walikuwa
wanajaribu kuwahoji watu ambao aliwasiliana nao kwa siku hiyo..” alisema.
Aidha,
alisema taarifa za kuonekana kwake alizipata leo asubuhi baada ya kupigiwa simu
na rafiki wa mgombea huyo aliyemtaja kwa jina moja la Daudi, na kumuambia kuwa
Joel alimpigia simu na kumuambia kuwa yupo Zahanati ya Bursa, akisema kuwa hata
simu aliyeitumia aliazima kutokana na simu zake kutokuwa na chaji.
Alisema,
baada ya kupata taarifa hizo, aliamua kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kwa
askari ambao walishirikiana katika hatua za kumtafuta na kuamua kwenda Zahanati
hapo kwa ajili ya kuthibitisha ambapo waliamua kuacha askari waendelee na kazi
yao ya kupeleleza juu ya tukio hilo.
“Leo
nilipopata taarifa za ghafla juu ya kuonekana kwake ni jambo la furaha kubwa
kwasababu ni kitu ambacho sikukitarajia, kwa hali ya kawaida mtu anapokamatwa
au kutekwa na mtu ambaye humjui huwezi kujua kwamba anaweza kumfanyia jambo
gani..kwahiyo kuna mambo mawili kumpokea akiwa hai au akiwa maiti.” Alisema.
Alisema,
kutokana na hali ambaye alikuwa nae wakati alipomuona hakuweza kumuhoji
chochote juu ya kutoweka kwake kwasababu alichoka na hata kumbukumbu zake
hazikuwa sawa na kusubiri mpaka hapo atakapopata nafuu.
Hata hivyo,
mzazi huyo hakutaka kulihusisha moja kwa moja tukio hilo na maswala ya kisiasa
ukizingatia na mvutano wa jimbo uliopo baina ya vyama vitatu kati ya vine
vinavyowakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA
na Chama cha Wananchi (CUF).
“Kuna mambo mawili
yanatokea wakati wa siasa, mtu mwingine anaweza akawa na jambo lake la pembeni
lakini akatumia nafasi ya wanasiasa au migogoro ya kisiasa kuingiza jambo lake ili
lionekane ni la kisiasa..kwahiyo ukisema linahusika na siasa naweza nikasema ni
ndio au hapama..” aliongeza.
Alisema,
haliwahi kumfuata na kumuambia juu ya kuwepo kwa vitisho anavyovipata juu ya
shughuli zake za siasa lakini hakuwahi kuweka wazi anavipata kutoka wapi.
“Kuna siku
alishawahi kuniambia kwamba kuna watu wanasema kwamba likitokea hili basi
watakuja kukuchomea nyumba moto..hilo alishawahi kuniambia lakini hakusema ni
nani na wakati mwingine wanamtumia ujumbe wa simu na wengine wanaongea nae ana kwa
ana kumuambia kuwa akifanya hivi tutafanya hivi, lakini kwenye siasa ni vitu
vya kawaida.” Alisema.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe, alithibitisha kupokea taarifa za
kupotea kwa mgombea huyo ambapo zilipokelewa ofisini kwake juzi saa saba mchana
zikidai kuwa aliaga nyumbani kwake kuwa nakwenda maeneo ya Mnarani kwa ajili ya
kukutana na jamaa zake na hakuonekana tena baada ya hapo.
“Kwahiyo
polisi tukaanza uchunguzi lakini hatimae leo (jana) amepatikana akiwa katika
hali ambaye sio nzuri sana, yupo katika kituo cha afya anatibiwa na kwamba
akipata fahamu tutajua nini kilichomtokea, lakini anaendelea vizuri..lakini
kabla ya hapo mgombea huyu alikuwa na mambo ya hajabu kidogo, aliwahi kwenda
katika vyombo vya habari na kusema kwamba amejitoa na hata gombea tena.
Alisema na
kuongeza, “lakini wakati huo huo wenzake kwenye chama chake cha Chadema,
waksema hawezi kujitoa kwasababu chama ndicho kinaweza kutangaza kujitoa..”
aliongeza.
Aliwataka
wanasiasa kuwa watulivu na kufanya kampeni zao kwa amani na kwamba swala la
mgombea kugombea au kuto gombea ni la hiyari yake, hivyo wahepuke kuzua
mitafaruku isiyo ya lazima ili mchakato upite salama.
No comments:
Post a Comment