Mfanyabiashara maarufu ya Uji Shuwea Salum, akisafisha vitendea kazi vyake baada ya kumaliza kazi. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
KUMILIKI
kiwanja katika manispaa ya Mtwara Mikindani kwa miaka hii sio kazi rahisi kwani
wapo vijana wengi na hata watu wazima ambao bado wanapambana kwa hali na mali
ili kuweza kufikia hatua hiyo amayo inaaminika kuwa ni hatua mojawapo kubwa ya
mafanikio katika safari ya maisha.
Ardhi
inapanda thamani kwa kasi na kwamba katika manispaa hiyo inakuwa sio kitu
rahisi kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na kasi ya maendeleo kutokana na
uwekezaji unaofanyika zaidi ukitokana na uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi
zilizopo katika mkoa huu wa Mtwara, kiasi cha kuwafanya wawekezaji kuhitaji
maeneo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, ofisi, shule, vyuo na viwanda.
Wapo baadhi
ya wajasiliamali wadogo ambao ukiambiwa kuwa wanamiliki ardhi ndani ya manispaa
hii kwa biashara zao ndogondogo za kila siku wanazozifanya pengine hutoamini
kwa haraka, lakini ukweli ni kwamba wapo na miongoni mwao ni wanawake.
Shuwea
Salumu Mpatane ‘Mama Uji’ ni mama maarufu sana katika mtaa wa Ligula hasa
katika eneo la kuzunguka uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, kutokana na
biashara yake ya kuuza uji wa ulezi kwa kutembeza mtaani ambayo licha ya kumpa
umaarufu huo, imemfanya kuwa miongoni mwa wanaomiliki viwanja ndani ya manispaa
hiyo chenye thamani ya sh. Milioni 1 na mwaka huu ujenzi unatarajiwa kuanza.
Anasema
katika harakati za kuanza kwa ujenzi huo katika eneo la nusu heka tayari
ameshapata bati 25 ambapo anataraji kuanza kujenga nyumba yake itakayokuwa na
uwezo wa kuwa na vyumba viwili na ukumbi.
Shuwea alianza biashara ya uji miaka sita iliyopita katika
eneo hilo la Nangwanda akianza kwa kuuza kikombe kimoja sh. 200 kabla ya
kupandisha mpaka sh. 300 na sasa ikiwa ni sh. 500 huku anadai sababu za
kupandisha bei ni kutokana na kupanda kwa gharama za mahitaji.
Anasema
mbali na kumiliki kiwanja hicho, mafanikio mengine anayojivunia kupitia
biashara hiyo ni kuweza kumudu kulipa pango ya mahala anapoishi sasa na kuweza
kuwasomesha watoto wake watatu huku mmoja akiwa amehitimu kidato cha Nne mwaka
jana katika shule ya sekondari ya Chuno, mwingine ndio anaingia kidato cha
kwanza mwaka huu na mwingine wa mwisho ana umri wa miaka tisa yupo darasa la
kwanza.
Shuwea Salum
|
“Kipindi
ambacho biashara ilikuwa nzuri kwasiku ilikuwa narudi na 40,000 lakini kwa sasa
hivi nimepunguza kipimo kutokana na uchumi wenyewe umeshuka na pesa imekuwa
ngumu, sasa hivi narudi na 25,000 au ikizidi sana 30,000..katika hiyo, nikitoa
gharama za manunuzi ya mahitaji, naweza kupata faida ya sh. 15,000 kutokana na
mahitaji yenyewe sasa hivi kuwa yamepanda bei..anasema Shuwea na kuongeza:
“Ulezi
nakuwa nasaga tu unga kama kilo 20 hivi natumia muda wa wiki mbili, kwa siku
nauza chupa 10 ambazo zinaingia vikombe saba, nauza na maandazi..sina biashara
nyingine zaidi ya uji.” Anaongeza.
Kutokana na
kufanya kazi na watu ambao miongoni mwao wapo wa kila aina ya tabia, yani zile
zenye kuwa njema na zile ambazo humkwaza na kuwa kikwazo katika biashara,
anasema wapo anaogombana nao juu ya malipo na wengine hata kumdhurumu ambapo
anaamua kuachana nao na kuwakwepa kwa kutowapitishia tena siku nyingine.
Anasema
akili ya kufanya biashara hiyo ilimkuta mara baada ya kuachika kutoka kwa
aliyekuwa mume wake ambaye ndio alizaa naye watoto hao watatu, na kwamba
alianza kwa kujaribu ili aone kama ataweza kuyamudu maisha huku akiwa hana
mume.
“Wakati
nimeanza ni pale baada ya kuachika na kuona ugumu wa maisha ndio nikaona nianze
hii biashara, yani kujaribu kama nikifanya hii biashara je nitauza au..lakini
baadae nikaona nina wateja, na hapa Umoja (Nagwanda) nilipoanza sijui kulikuwa
na mabanda Matano tu ndio yalikuwa yamefunguliwa, hakukuwa na watu wengi
kwakweli kama ilivyokuwa sasa hivi..na nilianza na uji chupa mbili kabla ya
sasa kufikia hizo chupa 10..” anasema Mama Uji.
Mama Uji
anasema malengo ambayo amejiwekea hapo baadae ni kubadilisha biashara kutoka
kuuza uji na kuamua kufanya biashara ya kuuza nguo za kike aina ya Madera
ambazo atakuwa akizifuata jijini Dar es Salaam na kwenda kuziuza huko vijijini.
Shuwea
anasema katika familia yao wamegawanyika katika kufanya shughuli mbalimbali za
kujiingizia kipato ambapo wapo wafanyakazi na wafanyabiashara, huku yeye akiwa
na ndugu yake mmoja wakuzaliwa nayeshirikiana naye katika majukumu mengine
tangu mama yao mzazi alipofariki dunia mwaka 1995.
Anasema
kutokana na kuachika katika ndoa mbili katika mazingira magumu na kunyanyasika,
kwa sasa hafikilii suala la kuolewa tena labda mpaka pale atakapojiridhisha juu
ya kujiweka sawa kimaisha ili hata akiamua kuolewa awe tayari ana vitu vyake
mwenyewe na miradi ya kumuingizia kipato.
“Kwa sasa
hivi kwasababu nilishapata changamoto za wanaume kunitelekeza, sitokubali mpaka
pale nitakapofanikisha malengo yangu, kwasababu mume wakwanza ambaye ndio baba
wa watoto wangu aliniacha katika mazingira magumu sana na ndio kisa cha kuanza
kuuza huu uji..” alisema na kuongeza:
“Aliniacha
kwenye mazingira ya utata nikawa naishi maisha ya shida nikasaidiwa tu na watu wakanilipia
pango marafiki zangu ambao naongea nao vizuri, nikaolewa tena ndoa yapili
vilevile ikawa mtihani kwahiyo nimejifunza kwamba sitoolewa mpaka mambo yangu
yawe safi na akinusumbua niweze kuishi kwangu..” aliongeza.
Nilipata
kuzungumza na mmoja wa wateja wake wakubwa wa biashara yake, Charles George,
ambaye ni katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (Mtwarefa), ambaye
ana zaidi ya miezi Minne tangu aanze kupata huduma hiyo alisifia na kudai kuwa
kadiri siku zinavyoenda mama huyo ndio anazidi kuboresha huduma zake.
Anasema
licha ya kupata huduma, muda mwingine anatumia utu uzima wake na uteja wake wa
muda mrefu kuweza kumshauri namna ya kuishi vizuri na wateja wake ili azidi
kuwavutia wengi zaidi.
“Kwa uzoefu
wangu na kwasababu ni mtu mzima na najua maana ya biashara au uteja, mara
nyingi huwa najitahidi kumpa maelezo ambayo yatamsaidia kuweza kuvuta wateja
wengi, na kikubwa ambacho namshauri mara nyingi ni kuwa na lugha nzuri kwa
wateja wake..” alisema.
Pamoja na
jitihada anazozifanya Shuwea za kuhakikisha anafikia malengo yake, lakini bado
anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kukosa ofisi kwa ajili ya
biashara yake na kukosa msaidizi ambaye anaweza kumsaidia iwapo atapatwa na
dharura.
Anasema
anajitahidi kufanya bidii za kumpata msaidizi lakini changamoto anayoipata ni
wale anaowaomba kwa ajili hiyo kudai kuwa hawawezi kufanya kazi hiyo kwasababu
ni ngumu kwao, ukizingatia hana ofisi maalumu hivyo itawalazimu na wao
watembeze uji kama anavyofanya.
Kutokana na
jitihada zinazofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini za kuanzisha mafao
mbalimbali ya kuwainua wajasiliamali wadogo, bado ‘Mama Uji’ hajatambua fursa
za kujiunga na mifuko hiyo ambapo miongoni mwa faida anazoweza kunufaika nazo
ni pamoja na kuwa na bima ya afya ambayo inaweza kumsaidia akipatwa na ugonjwa.
“Nilikuwa
nae Bima ya Afya ila huyo mume ambaye nilikuwa naye alikuja kuninyang’anya..siku
aliyokuja kuninyang’anya alisema inabidi zibadilishwe alafu atanirudishia lakini
mpaka leo nikimkumbusha hakuna anachonieleza cha maana na mimi nikaamua
‘kupotezea’ lakini nilishamwambia kwamba mimi ni mzazi mwenzako na endapo
nitafariki basi na wewe jukumu la watoto utakuwa nalo..” alisema.
Anasema bado
hajawahi kuhudhuria mafunzo yoyote ya ujasiliamali na hata zinapotokea semina
zinazoendeshwa na mifuko ya hifadhi ya jamii juu ya namna ya kuwafikia
wajasiliamali wadogo, hajabahatika kuhudhuria kwahiyo hana elimu yoyote ya
kuweza kunufaika na mafao yanayotolewa na mifuko hiyo.
Wiki mbili
zilizopita nilipata bahati ya kuhudhulia semina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa
PPF ambapo pamoja na mambo mengine, ilikuwa na lengo la kutambulisha mafao
mapya mawili ambayo ni fao la Uzazi na fao la Wote Scheme ambalo linawanufaisha
wajasiliamali wadogo.
Meneja Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF kanda ya kusini. |
Meneja wa
PPF kanda ya Kusini, Kwame Temu, anasema kutakuwa na programu maalumu ya
kukutana na wadau wa sekta zisizo rasmi miongoni mwao ni hawa wajasiliamali
wadogo hapo baadae lakini wameona ni bora kupitia semina hiyo kutoa elimu juu
ya mafao hayo ambapo aliwataka wanachi wa Mtwara kuchangamkia fursa za kujiunga
na mfuko huo.
Shuwea iwapo
ataamua kujiunga na mfumo wa Wote Scheme wa PPF, miongoni mwa huduma atakazo
faidika nazo ni pamoja na kupata kadi ya bima ya afya na kuweza kupata mikopo
ya Elimu au Timiza Ndoto Yako kupitia benki ya posta, huduma ambazo zinatolewa
kwa kuchangia kiasi kinachoanzia sh. 20,000 kwa mwezi.
Pia nitoe
rai kwa mifuko hii kuweza kupanua wigo wa kuwafikia hawa wajasiliamali wadogo
na kuhakikisha wanapata taarifa na elimu ya kutosha juu ya namna watakavyoweza
kunufaika na huduma wanazozitoa.
No comments:
Post a Comment