Tuesday, October 6, 2015

Mgombea ubunge Mtwara mjini kuboresha afya kwa wazee, akina mama na watoto.





Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maftaha Nachuma, akinadi sera za chama chake na kuomba kura kwa wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Shangani, manispaa ya Mtwara juzi.



Maftaha Nachuma


Juma Mohamed.

MGOMBEA Ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, amesema iwapo wananchi watamchagua kuwa mbunge wa jimbo hilo atahakikisha huduma ya afya inatolewa bure kwa akina mama wajawazito, watoto wachanga na wazee.
Akizungumza juzi mkoani hapa katika mkutano wa hadhara wa kunadi sera na kuomba kura uliofanyika katika kata ya Shangani, alisema kumekuwa na ubabaishaji katika baadhi ya hospitali juu ya kutekeleza mpango huo ambao ni agizo la serikali.
Alisema, wazee wana haki ya kutibiwa bure kupitia kadi zao wanazopatiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), lakini suala hilo halifanyiki na baadala yake wanaambiwa kuwa wakitoa dawa bure watakosa pesa za kununua dawa nyingine.

Wananchi wa kata ya Shangani, manispaa ya Mtwara, wakifuatilia sera za mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maftaha Nachuma, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo juzi.

“Kuna kadi zinasema ni bima ya afya ya wazee, ile bima ukienda hospitali unaambiwa hakuna dawa na mganga mfawidhi nimeongea naye ni rafiki yangu mmoja, aliniambia ya kwamba hatuwezi kutoa dawa kwa watu wanaotumia bima kwasababu nitakuwa sina pesa za kununulia dawa kwa ajili ya wagonjwa wengine..kwahiyo mwisho wa siku zile bima zinazotolewa mtu akienda anaambiwa hakuna dawa nenda kanunue famasi..” aliema.
Aliongeza kuwa, kutokana na Mtwara kuwa na rasilimali ya gesi na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ingeamua kuwekeza mkoani hapa na kuchakata gesi hiyo kasha kuiuza katika nchi jirani ambazo zinahitaji, basi fedha ambazo zingepatikana zingetumika kununua dawa na kuzisambaza hospitalini.
Hata hivyo, swala la kuchakata gesi asilia inayotoka Madimba mkoani hapa kwenda Kinyerezi, Dar es Salaam, linafanyika katika kiwanda cha kuchakata na kwamba zoezi hilo linaendelea na gesi tayari imeshafika jijini Dar es Salaam.

Maftaha Nachuma



Aidha, alielezea mkakati wake mwingine kuwa ni kuunda mabaraza ya wazee katika kila kata na tarafa, ambapo kupitia mabaraza hayo wazee watanufaika na asilimia tano ya fedha zinazotolewa na serikali kupitia halmashauri zao.
“Kuna pesa zinazoingia halmashauri ambazo ni za mfuko wa maendeleo ya jimbo, Mtwara mjini hamjawahi kuelezwa na mbunge kuwa ni kiasi gani cha fedha kinachoingia Mtwara mjini..ni kwasababu hana nia njema na wananchi wa jimb la Mtwara mjini, yuko kwa masilahi yake na biashara zake..Mtwara mjini zinaingia zaidi ya milioni 50 kwa mwezi ambazo ndani yake kuna kuna asilimia zinatakiwa zikahudumie wazee..” alisema.
Na kuongeza “kuna asilimia zinatakiwa zihudumie akina mama, kuna asilimia zinatakiwa kuhudumia vijana, ‘bodaboda’ na akina mama, kuna asilimia zinatakiwa ziboreshe maendeleo na miundombinu..” aliongeza.
Alisema, kutokana na utafiti aliowahi kuufanya katika sekta ya elimu, aligundua kuwa mikoa ya Mtwara na Lindi ndiyo ambayo inaongoza kwa walimu wake kuidai serikali kuliko mikoa na wilaya zote za Tanzania.
“Kama kuna mwalimu yeyote aende katika mtandao wa wizara ya elimu aangalie madeni na malipo yake kwa miaka mitano katika wilaya zote za Tanzania zikiwemo na za Dar es Salaam alafu afaninishe na madeni ya walimu wa Mtwara na Lindi, atakuja kuthibitisha kwamba walimu wa Mtwara na Lindi ndiyo wenye madeni mengi..ndugu zangu nimesimama ili na wao niende nikawatetee bungeni.” Alisema.

No comments: