Monday, October 5, 2015

150 manispaa ya Mtwara kupatiwa semina juu ya fursa za gesi asilia.



Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akifungua semina ya siku tatu juu ya kutambua faida za rasilimali ya gesi asilia, uwekezaji na fursa zitokanazo na uwekezaji huo, inayoendeshwa kwa vijana 150 kutoka manispaa ya Mtwara Mikindani


 Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego

Na Juma Mohamed
 
VIJANA wapatao 150 kutoka katika manispaa ya Mtwara mikindani wanapatiwa semina maalumu kwa ajili ya kutambua faida za rasilimali ya gesi asilia, uwekezaji na fursa zitokanazo na uwekezaji huo.
Semina hiyo iliyoandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, imelenga kuwawezesha vijana kutambua fursa na kupata taarifa sahihi juu ya mambo mbalimbali ya kimaendeleo yanayoendelea mkoani hapa hususani uwekaji wa viwanda na miradi mingine.
“Lengo la semina hii limetokana na hali halisi ya maisha yetu baada sisi viongozi wenu kubaini vijana wengi na jamii kukosa taarifa sahihi juu ya mambo Fulani tukaona kuna haja ya kukutana na kukumbushana na kupeana habari juu ya vitu ambavyo vinaendelea..” alisema mkuu wa Mkoa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Alisema, semina hiyo ambayo imeanzia manispaa ya Mtwara, itaendelea katika wilaya zote za mkoa wa Mtwara ili kuweza kuwafikia vijana ambao ndio kundi kubwa katika jamii ukilinganisha na makundi mengine.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego

Alisema, semina hiyo imewahusisha pia waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali mkoani hapa kwasababu mchango wao unafahamika katika kuandika habari mbalimbali zinazohusu rasilimali hizo, hivyo uwepo wao utasaidia kuwaongezea ujuzi wa masuala mengine ambayo walikuwa hawayafahamu.
“Kikubwa ni kuwa wasikivu na kuwasikiliza watoa mada, lakini uzuri wa semina hii sisi sote tumekuja na vitu kichwani..kila mmoja hapa anauelewa wake kadiri mwenyez mungu alivyomjaalia, kwahiyo watoa mada matumaini yangu watukua wanachokoza tu na sisi tutakuwa tunashiriki kwa kujitoa na kuhakikisha kwamba tunawekana sawa na tukitoka humu ndani tunakuwa na utimamu na taarifa zote zilizo sahihi..” aliongeza.

Vijana kutoka manispaa ya Mtwara Mikindani, wakiwa katika semina ya siku tatu juu ya kutambua faida za rasilimali ya gesi asilia, uwekezaji na fursa zitokanazo na uwekezaji huo,iliyoandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego

Kwa upande wao, washiriki wa semina hiyo walisema wanatarajia kupata uwelewa mkubwa juu ya masuala mbalimbali ikiwemo hatima yao katika ukosefu wa ajira ambao ndio umekuwa kilio kikubwa kwa vijana katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Saidi Hassan, mkazi wa Chikongola, alisema kupitia semina hiyo itakayoendeshwa kwa siku tatu, anatarajia kujua mengi kuhusu rasilimali hiyo na kwamba ataitumia kuweza kupata majibu ya maswali yake ambayo yalikua hayana majibu kwa muda mrefu.
“suala la kwanza kuuliza ni kuhusu ajira kwa vijana, je tunaandaliwa vipi kutokana na kukaa bila ajira..kwahiyo hilo ni miongoni mwa maswali nitakayouliza katika semina hii kwasababu vijana wengi hatuna uelewa juu ya namna tutakavyopata ajira kupitia gesi yetu..” alisema.
Naye, Shabani Juma, alisema semina hiyo itasaidia vijana wengi kuelewa namna gani watanufaika na rasilimali zao na kwa muda gani wataanza kuziona hizo faida kwasababu wengi miongoni mwao wanajua ni jambo la muda mfupi kuanza kuziona faida zitokanazo na gesi.

No comments: