Thursday, December 31, 2015

Simba wazichapa na mashabiki wa Ndanda, Mtwara.

Wachezaji wa Simba wakiwa katika harakati za kupambana na baadhi ya Mashabiki wa Ndanda ambao walionekana kuwashambulia kwa maneno ya kuudhi pamoja na lugha za matusi kwa muda wote waliokuwa mazoezini na hata baada ya mazoezi, kiasi cha kusababisha vurugu baina yao na kufikia kupigana na kurushiana mawe nje ya uwanja wa Nangwanda Sijaona ambao unatumika katika kwa mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wa Simba na Ndanda


Mchezaji wa Simba, Awadh Juma akitoka kukimbizana na mashabiki wa Ndanda.



Wachezaji wa Simba na kocha wao Dylan Kelly walipoanza kuzozana na mashabiki wa Ndanda ndani ya uwanja wa Nangwanda Sijaon


Kocha wa Simba Dylan Kelly, akijaribu kuwaondoa wachezaji wake waliokuwa wakigombana na mashabiki wa Ndanda mara baada ya kumaliza mazoezi ya asubuhi.



Hali ilivyokuwa nje ya uwanja wa Nangwanda Sijaona, katika vurugu za wachezaji wa Simba na mashabiki wa Ndanda



Mwenyekiti wa mashabiki wa Ndanda, Mohamed Jimbu (Mwenye fulana la Blue) akiwa ndani ya gari la Polisi wakielekea kituoni.


Askari wakiondoka na mashabiki wawili wa Ndanda waliohusika katika vurugu



Na Juma Mohamed, Mtwara.

WACHEZAJI wa timu ya Simba wamelazimika kupigana na mashabiki wa timu ya Ndanda ya mkoani hapa nje ya uwanja wa Nangwanda Sijaona na kurushiana mawe, kutokana na kukerwa na vitendo vilivyofanywa na mashabiki hao vya kuwazuia kutumia lango kuu la kuingilia na kutokea uwanjani, na baadala yake kuwataka watumie lango wanalotaka wao.
Vurugu hizo zilianzia ndani ya uwanja huo mara baada ya Simba kumaliza mazoezi yao ya asubuhi ambapo walitaka kutoka uwanjani kwa kutumia lango kuu ambalo awali wakati wanaingia mashabiki wa Ndanda walizuia lisifunguliwe kwa madai kuwa ni mbovu na Simba kulazimika kutumia lango lingine dogo ambalo kwa kawaida halitumiwi na timu wakati wa kuingia au kutoka uwanjani.

Golikipa wa Simba, Manyika Peter na kiungo, Abdi Banda, wakirejea kutoka katika harakati za kupambana na mashabiki wa Ndanda


Wachezaji wa Simba wakiwakimbiza mashabiki wa Ndanda.

Mashabiki wa Ndanda walionekana kuwarushia maneno ya kuudhi na lugha za matusi wachezaji wa Simba muda wote wakiwa mazoezini na hata baada ya kumaliza, jambo ambalo liliwafanya wahamaki na kuamua kwenda kuwashambulia baadhi yao, huku mwalimu wa Simba Dylan Kelly akihangaika kuwadhibiti wachezaji wake ambao leo wanaingia uwanjani kukipiga na Ndanda Sc.
Wachezaji hao walionekana kukimbizana na mashabiki nje ya uwanja huku baadhi ya mashabiki wakirusha mawe ambayo hata hivyo hayakuweza kumpata au kumuathiri mtu yeyote mpaka Simba walipoondoka eneo la tukio.
Akizungumzia tukio hilo, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, Iddi Kajuna, alisema ni kitendo ambacho sio cha kiungwana na hakikubaliki mahali popote katika michezo na kwamba ameliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuliangalia kwa mapana suala hilo na ikibidi hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Mchezaji wa Simba, Mussa H. Mgosi, akiondolewa katika vurugu na Iddi Kajuna.

“Cha hajabu sasa wakati wachezaji wamemaliza mazoezi na wanajaribu kutoka sasa kupitia mlango mwingine ambao wao walikuwa hataki wapiti mlango ule na walitaka wapiti mlango ambao wameuandaa wao, ndipo walipoanza kuvamia wachezaji kwa kuwatusi, kuwapiga lakini tukajaribu kuwasihi wachezaji wakapata hasira sana ambayo kwakweli haikuweza kuvumilika lakini tulijitahidi sana kuwabana wachezaji tukiwa watu zaidi ya 20 kuwarudisha ndani ya basi huku wao wakiendelea kurusha mawe, matofali..sasa tukaona huu sio ustaarabu tukawaondoa na tukajaribu kwenda sasa kwenye chombo cha dola na baadhi yao wawili tayari tumewatia mikononi..” alisema Kajuna.

Mjumbe wa Kamati ya utendaji ya Simba, Iddi Kajuna, akizungumzia kuzuka kwa vurugu baina ya wachezaji wao na mashabiki wa Ndanda.

Alisema, wapo baadhi ya mashabiki wa Ndanda ambao walionyesha ustaarabu kwa kujaribu kuwaonya wenzao ambao walifikia hatua ya kumtolea lugha za matusi hata mzee Hassan Dalali ambaye ameambatana na timu hiyo.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mashabiki wa Ndanda, Mohamed Jimbu, akizungumza kwa ufupi kabla ya kukamatwa na askari, alisema Simba walishikwa na woga usio na msingi kutokana na vitisho ambavyo vilionyeshwa na mashabiki hao ambavyo havikuwa na nia yoyote mbaya.

Meneja wa Timu ya Ndanda, Martin Mwesiga, akizungumzia vurugu za mashabiki wa Ndanda na wachezaji wa Simba.

“Huo ni uwoga wao Simba, kwasababu wamekuja asubuhi wamekuta mashabiki wapo hapa na wao wenyewe wanataka kufanya mazoezi kwahiyo walivyoingia walikuta vitu vya ajabuajabu ambavyo mashabiki wenyewe hivyo vitu vilikuwa ni vya kuwatisha tu Simba, hao Simba wakawa wamekuja juu wanataka kuanzisha vurugu tokea asubuhi..kwahiyo walivyokuwa wameingia, mashabiki wakawa wanawazomea wachezaji wao viongozi wakapanda jukwaa kubwa kwenda kugombana na mashabiki..” alisema Jimbu kabla ya kukimbia baada ya kuona askari.

Wachezaji wa Simba wakiwa mazoezini, kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Ndanda Sc wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Kocha wa Simba, Dylan Kelly, akiwa katika mazoezi ya asubuhi na wachezaji wake, katika uwanja wa Nangwanda Sijaona

Naye, katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) Charles George, alisema Mtwarefa inalaani kitendo hicho kilichofanywa na mashabiki hao ambapo alikiri kuwa walitumia muda mwingi kuwakashifu wachezaji na viongozi wao, na kwamba watajaribu kukutana na viongozi wa Ndanda ili kuwaagiza wake na viongozi wa mashabiki hao kuwasihi juu ya vitendo hivyo ambavyo vinaweza pia kuigharimu timu yao.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Mrakibu mwandamizi wa Polisi, George Salala, alikiri kupokea taarifa za malalamiko kutoka kwa viongozi wa Simba wakilalamikia vitendo hivyo vya kufanyiwa vurugu, na kusema kuwa wameshaanza kulifuatilia tukio hilo ambalo sio la kiungwana.

Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Charles George, akizungumzia tukio la vurugu za mashabiki wa Ndanda na wachezaji wa Simba.

Aliwaomba viongozi wa Ndanda kukaa na mashabiki wao kwa ajili ya kuwatuliza ili mchezo huo unaofanyika leo uweze kuchezwa kwa amani na utulivu.

“Mpaka sasaivi nimekwishawaagiza maofisa wangu na wakaguzi wanaanza kulifuatilia hili na tutakapo baini wale waliohusika, kwa hakika tutachukuwa hatua kali..na kesho (Leo) ulinzi utakuwa wakutosha tutatumia nguvu zote za kiusalama tulizonazo kuhakikisha kwamba pale uwanjani hapatokei uvunjifu wa amani..” alisema.

No comments: