Monday, July 4, 2016

Aliyekuwa DC MTWARA aacha majonzi kwa wananchi.




Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally, akiagana na baadhi ya viongozi na wakazi wa manispaa ya Mtwara Mikindani baada ya hafla ya kukabidhi ofisi leo.



Fatma Ally akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waandishi wa habari wa mkoa wa Mtwara, baada ya hafla ya kukabidhi ofisi. Kushoto ni mwanidshi wa Juma News, Juma Mohamed.


Juma Mohamed, Mtwara.

Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Mtwara Mikindani wameeleza masikitiko yao juu ya kuondoka kwa aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally, ambaye ni miongoni mwa wakuu wa wilaya ambao hawakuteuliwa tena katika uteuzi mpya uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Magufuli.
Wakizungumza baada ya hafla fupi ya kukadhi ofisi kwa mkuu wa wilaya mpya Dokta Khatibu Kazungu, walisema Fatma alikuwa na mahusiano mazuri na jamii na kwamba miongoni mwa mambo yatakayokumbukwa ni wepesi wake katika kusuluhisha migogoro mbalimbali inayowahusu wananchi wake.
“Dada Fatma ukimwambia kuna tatizo yupo tayari, kuna mgogoro kuhusu ardhi yuko tayari kwa kujitoa anaacha kazi zake anatukimbilia wananchi..kama juzi juzi kulikuwa na mgogoro huko Naliendele kati ya Jeshi na wananchi, lakini alikimbia haraka sana aliposikia tu alijitoa..” alisema Hadija Salum, mkazi wa Majengo.
Naye, Fatma Msele, alisema kiongozi huyo alikuwa karibu sana na wananchi pamoja na kutii kila hitaji la wananchi wake lililo ndani ya uwezo wake hivyo kupelekea kuwa kipenzi cha wanamtwara walio wengi, na kwamba kuondoka kwake atakumbukwa kwa mengi.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Dkt. Khatibu Kazungu, (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Fatma Ally na katibu Tawala wa wilaya hiyo Theofil Ndomba. Wengine ni viongozi mbalimbali wa wilaya.



Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Fatma ambaye aliwahi kuongoza wilaya za Nanyumbu na Chamwino kabla ya kuhamishiwa Mtwara, alisema katika uongozi wake amesaidia kuirejesha amani ya Mtwara ambayo wakati anaanza kazi haikuwa kwa kiasi kikubwa pamoja na kupunguza kasi ya uvuvi haramu uliodumu kwa kipindi kirefu.

"Tutakukumbuka dadaetu Fatma"



“Lakini hapa Mtwara nilipokuja nilikutana na changamoto kubwa mbili pamoja na changamoto zingine ndogondogo, kwanza amani ilikuwepo lakini haikuwa ya kutosha yani mahusiano hayakuwa ya karibu sana kati ya wananchi na serikali..lakini leo nakukabidhi ofisi ikiwa wananchi wako wa Mtwara ukiwahitaji muda wote utawapata na kuna ushirikiano mzuri sana kati ya wananchi na serikali na mshikamano mkubwa na wananchi wamekuwa wenye mshikamano wa hali ya juu..” alisema.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya hiyo Dokta Kazungu akiongea kwa ufipi, aliwataka wananchi na viongozi wenzake kushikamana katika kazi ili kufanikisha maendeleo.
“Kikubwa Zaidi, naomba ushirikiano wenu ili kuipandisha Mtwara yetu iweze kutoka hapa tulipofikia sasa hivi..kwasababu hiki ndio kikao changu cha kwanza sitokuwa na mengi lakini naendelea kujifunza kwahiyo nichukuwe fursa hii kuwashukuru sana kwa kuweza kuhudhuria hafla hii..” alisema Kazungu.
Pamoja na mambo mengine, Fatma alikabidhi michango ambayo alifanikiwa kuikusanya kutoka kwa wananchi kupitia kampeni yake ya ‘Haba na Haba’ katika kutatua uhaba wa madawati ambayo ni fedha kiasi cha sh. Milioni 25.5, huku wilaya ikiwa imekamilisha tatizo la madawati kwa asilimia 100.


No comments: