Saturday, July 25, 2015

Uchaguzi CHADEMA..Nanauka awaburuza wapinzani wake, lakini aanguka ukumbini na kupoteza fahamu..



 

Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini anaesubiri maamuzi ya UKAWA Joel Nanauka, akiwa katika moja ya harakati zake.

Wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa CHADEMA wilaya ya Mtwara mjini wa kuchagua wagombea ubunge, wakishangilia matokeo baada ya Joel Nanauka kutangazwa kuwa mshindi.


 Na Juma Mohamed, Mtwara.
Hatimae Joel Nanauka amefanikiwa kupata baraka za wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) wilaya ya Mtwara mjini ambao ni wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa kura ya maoni, kwa kuchaguliwa ili kuwa mgombea wa jimbo hilo, baada ya kuwagaragaza wapinzani wake aliokuwa akichuana nao katika kinyang'anyiro hicho.

Akitangaza matokeo hayo, mwenyekiti wa Chadema kanda ya kusini, Hamisi Namangaya, alisema Nanauka aliokuwa akichuana na wagombea wengine katika nafasi ya ubunge wa jimbo la Mtwara mjini ambao ni Ibrahim Mandowa, Dastan Mulokozi na Mohamed Hassan Hanga, alijikusanyia jumla ya kura 116 huku aliemfuatia Ibrahim Mandowa akipata kura 50.

Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya kusini Hamisi Namangaya, akiongea jambo na Mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini, Joel Nanauka baada ya kumtembelea nyumbani kwake kwenda kujulia hali baada ya kuugua, kuanguka na kupoteza fahamu katika ukumbi wa mkutano wa uchaguzi hapo jana.

 
Wagombea wengine katika nafasi hiyoMohamed Hassan Hanga alipata kura 9 huku Dastan Muolokozi akiambulia kura 4, hivyo mwenyekiti kumtangaza Joel Nanauka kuwa ndio mshindi wa mchakato huo ambapo sasa atasubiri maamuzi ya vikao vya UKAWA ili kujua kama atateuliwa kugombea au laa.

Aidha, Namangaya akitangaza matokeo ya waliowania nafasi ya ubunge wa viti maalum ambao hupigiwa kura na wajumbe wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), alisema mshindi katika nafasi hiyo iliyowaniwa na watu wawili ni Tunza Issa aliyepata kura 20 akimshinda mpinzani wake Anna Deo.

 

Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya kusini Hamisi Namangaya, akitangaza matokeo ya uchaguzi wa wagombea ubunge jimbo la Mtwara mjini na wa viti maalum.

Akizungumza baada ya kujua matokeo, Nanauka ambaye aliugua ghafla na kuanguka ukumbini hapo na kupoteza fahamu, alisema anamshukuru mwenyezi mungu kwa matokeo yaliyotangazwa na anaamini wanachadema wamemchagua kiongozi waliemuhitaji na anaimani kuwa wataendelea kumuamini katika kuwawakilisha kama jimbo.
“Napenda kuwashukuru viongozi waliokuja leo kusimamia ambao ni viongozi wa kanda, kwakweli wameonyesha weledi wa hali ya juu sana..na imetusaidia kupunguza migongano ambayo ilitokea katika uchaguzi uliopita.” Alisema 

Akizungumzia tukio la kuugua na kuanguka kisha kupoteza fahamu ndani ya ukumbi wa uchaguzi, tukio ambalo lilimkuta baada ya kumaliza kujinadi kwa wajumbe kisha kuomba kura, alisema alijisikia kuishiwa nguvu na kisha kupatwa na kizunguzungu.

“baada ya hapo sikujua kilichoendelea mpaka nilipofika hospitali..lakini kwa mujibu wa daktari, ilionyesha kuwa sukari yangu ilikuwa chini sana pengine ni kutokana na pilikapilika ambazo tunazifanya kwa siku za karibuni katika kuelekea huu mchakato, lakini kwa sasa naendelea vizuri na naamini nitaendelea na shughuli zangu kama kawaida.” Alisema Nanauka.
Aidha, mgombea aliyeshindwa katika kinyang’anyiro hicho, Mohamed Hassan, alisema ameyapokea matokeo vizuri na yako sahihi kwakuwa uchaguzi ulikuwa wa huru na wa haki na kwamba asiye kubali kushindwa si mshindani na katika ushindani lazima mshindi apatikane.

……………………………………….mwisho…………………………………………….

No comments: